Monday, 26 December 2011

Petroli, dizeli yauzwa kwa Sh10,000 kwa lita na nchi bado inakalika

Juddy Ngonyani,Sumbawanga

BAADHI ya wamiliki na madereva wa vyombo vya usafiri vinavyotumia mafuta katika Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, wameuomba uongozi wa Serikali mkoani humo kuingilia kati tatizo la upatikanaji wa nishati hiyo ikiwa ni pamoja na kujua bei halali wanayopaswa kuuziwa.

Wakizungumza na gazeti hilo kwa nyakati tofauti baadhi ya wamiliki na madereva walisema kuna tatizo la kukosekana kwa mafuta katika vituo mbalimbali vya mji wa Sumbawanga.Waliolalamikia tatizo hilo ni pamoja na Issa Lubega, Justin Mballa, Chacha Mwita na Zacharia Nsangazila.

Wamesema kwa sasa mafuta a petroli na dizeli yanauzwa kwa bei ya kati ya Sh6,000 na Sh10,000 kwa lita moja na kwamba yanauzwa na wachuuzi ambao inaaminika kuwa wanayapata katika vituo vya mafuta.

Waliiomba Serikali kuingilia kati tatizo hilo na kuhakikisha kuwa bei zinashuka hadi kufikia kati ya Sh3,000 na Sh5000 kwa lita.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya aliwataka watumiaji wa nishati hiyo kuwa na moyo wa subira wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiendelea na uchunguzi kuhusu tatizo hilo.

Manyanya pia aliwaasa wafanyabishara ya mafuta kuwa wakweli kwa wateja wao, ili kuepuka malalamiko na usumbufu.
Chanzo: Mwananchi Desemba 26, 2011.

No comments: