Wednesday, 14 December 2011

Kijiwe toka Abidjan na The Hague kwa Ocampi

Ninapoandika niko mjini the The Hague Uholanzi nikila mikuku. Ila huku ni winter baridi usiambiwe. Tunavaa mikoti mirefu hata glovu mikononi ili kuepuka baridi kutuuma kama wasemavyo wazungu. The cold bites wanasema.

Nisiwacheleweshe mkaanza kusonya na kutukana gazeti utadhani ni mimi. Baada ya Lwisi Mreno Ocampi kutaka rais wa zamani wa Cote di Vwaa, Profesa Laurent Gba-gboy aletwe hapa The Hague, kwa vile nami ni mwanasheria mwenzake tuliyesoma pamoja na kufundisha pamoja pale Harvard, alinipa mwaliko kuja kushuhudia kimbembe.

Kilichotusikitisha mimi na Ocampi ni ile hali ya kugundua kuwa kumbe Gbad- boy in profesa mwenzetu tena wa historia ila asiyejua kuisoma hiyo historia anayofundisha! Tulishangaa sana kugundua kuwa kumbe na mkewe Simone ni daktari lakini asiye na busara wala visheni ya kumshauri mumewe vizuri. Naye kwa ujuha wake alijifanya rais kwa vile mumewe alikuwa rais asijue madaraka hutoka kwa watu na si mali ya aliye naye. Maskini Simone hakujua kuwa madaraka ni kama koti! Hata kale ka msemo kuwa cheo ni dhamana hakakuwa na nafasi kwenye ubongo wake mfinyu kama panya.

Tulipoingia kwenye korokoroni au cell ya Gbad-boy alimofungiwa kama fisi tunduni, tulimkuta Gbad-boy ametoa mimacho kama panya aliyenaswa na mtego. Ingawa alivaa suti, hakuwa sopu sopu kama tulivyozoea kumuona alipokuwa madarakani akipambwa na kupambika. Suti ilikuwa inampwaya na ndevu zake hazikuwa zimenyolewa vizuri. Kwa ujumla alikuwa shagrabagra. Kwa wanaokumbuka picha nzima ya siku aliponyakwa, wanakumbuka mkewe Simone alivyokuwa kachoka na kuzeeka tofauti na kimwana first lady tuliyezoea kumuona baada ya kuupara kwa vipodozi na vikodozi kama wafanyavyo wajilishaji pepo wetu madarakani. Usingeamini kuwa kiumbe huyu aliwahi kuitwa mtukufu rais. Alikuwa amekonda na kuchakaa haraka huku akionyesha wazi kuchanganyikiwa akiishi kwenye kale na si leo. Maana nilipomuuliza kwa kifaransa: comment allez vous monsieur le president? Alijibu kwa kutabasamu akidhani kuwa bado yu rais na kusema: “Waliniogopa hadi kunileta huku kwa kunihadaa kuwa walikuwa wakinipeleka Abdjan kukutana na wanasheria wangu.” Ce tres mauvais alisema kwa kifaransa chake cha hovyo.

Nilipiga swali jingine la kuuliza alipo mkewe. Alizidi kuchanganyikiwa asijue la kujibu. Ma femme? Yaani mke wangu, aliuliza? Baada ya kuona hili swali halina faida kwa wasomaji, nilibadilisha kibao na kumuuliza ni kwanini hakusoma alama za nyakati. Hili alilijibu vizuri. Kwani alikiri kuwa wapambe na waramba viatu wake walimchuuza na kumtumia asijue walikuwa na lao. Alisema: “Kaka Mpayukaji uliniambia ulipopita kwangu ukitokea Misri na Tunisia. Bado nakumbuka ushauri wako jadidi kuwa madaraka ni tunda la msimu hivyo nisiyachukulie kama urithi. Nakumbuka sana mon frère.”

Aliendelea: “Naomba ukitoka hapa uwambie wote wanaoringia na kutumia madaraka vibaya wajue kuna mwisho. Tena waonye wawaonye wake zao wasipende kutumia madaraka yao kama mali ya familia wakiiba na kunyanyasa watu kana kwamba hakuna mwisho. Wakumbuke sana walipokuwa bado hawajaingia madarakani ili wasifanye kama tulivyofanya.”

Nilimuuliza kama ameishaonana na Chaz Teila. Alijibu kuwa yeye si mtu huru sawa na Teila hivyo kuonana si rahisi ingawa wamefungwa kwenye mahabusu jirani. Wakati akiendelea kuongea Ocampi alinionyesha sero iliyondaliwa kwa ajili ya Omari Bishkir wa Sudani atakapotiwa mbaroni. Hawa jamaa kweli wanajua kukomoana. Maana hiyo sero unayoambiwa ni chumba kimoja kidogo, kitanda kidogo, choo ndogo na meza ndogo kwishnei. Huwezi kuamini kuwa rais aliyewahi kujinoma kwenye ikulu ya mamia ya vyumba angeishi kwenye tundu kama bundi. Badala ya kulindwa na ma-body guards, sasa Gbad-boy analindwa na askari magereza tena wanoko kama nini? Ule wakati wa kubebewa kila kitu kuanzia kalamu hata kitabu umepita. Gazeti lenyewe analipata likiwa limechelewa na maafisa magereza wanamchagulia asome nini na si kama zamani ambapo alikuwa na washauri wa mambo ya kipuuzi kama avae au kusoma nini na kwa wakati gani.

Baada ya kuongea na Gbad-boy nilishika pipa kwenda zangu Abidjan kuomba kibali cha kumhoji Simone Gbad-boy. Baada ya kukubaliwa kwa sharti la kutotaja aliposhikiliwa, nilipanda chopa na kwenda kumfanyia mahojiano mama huyu aliyedanganywa kwa kuitwa Hillary Clinton wa Tropiki yaani Hillary Clinton des tropiques.

Hivyo, nilipofika kwenye jela ambalo siwezi kutaja, nilimkuta bibi kizee tofauti na kwini niliyezoea kumuona kwenye runinga na magazeti aking’aa kama taa. Mvi zilikuwa zinashindana kujitokeza huku uso wa Simone ukijaa kunyanzi.kwanza nilishangaa. Kumbe hawa jamaa wenye madaraka wanatuhadaa! Kumbe sura za kuvutia tuonazao si zao bali mikorogo ya kawaida! Sikuamini macho yangu kuwa yule niliyekuwa nimepelekwa kumuona ni shemeji first lady Simone Bbad-boy daktari wa lugha na historia kusema ukweli.

Sikuongea mengi na first lady huyu wa zamani kutokana na kuonekana alivyokuwa amepigika, hivyo nilimuuliza swali moja tu. “Una ushauri gani kwa ma-first ladies wengine wa Kiswahili?” Alitabasamu kwa shida na kujibu, “Wambie: madaraka yana mwisho na unaweza kuwa mbaya.” Nilimuuliza swali jingine kuhusu alivyokuwa akimtukana rafiki Barry Obby rais wa kwa Joji Kichaka akisema shame on you alimaanisha nini? Hakujibu. Nilimtolea picha yake akiwa amevaa matenge yaliyoshonwa mshono wa mwanamke nyonga. Aliziba uso wake kwa aibu na akaanza kulia kwa kwikwi na ukawa mwisho wa mahojiano yangu na Simone.

Kwa wanaojua vimbwanga vya wakubwa, huyu mama alikuwa na mamlaka kuliko hata rais wakati wa utawala wa mumewe. Alikuwa na biashara karibu kila kona kupitia NGO yake ya FPI. Aliiba kweli kweli. Lakini swali lililobakia, atakulaje hizo alizokwapua wakati yeye na mumewe wataozea gerezani huku mtoto wao mmoja akihukumiwa naye kwenda jela kwa kutumia madaraka ya dingi yake kama yake. Je wapo wangapi kama hawa huko vijiweni? Don’t quote me please when you name names.

Chanzo: Tanzania Daima Desemba 14, 2011.

No comments: