KWA wanaofuatilia taarifa za vyombo mbali mbali vya habari walishtuka kusikia Rais Jakaya Kikwete akinakiriwa akisema kuwa kama Chama Cha Mapinduzi ambacho yeye ni mwenyekiti kinaweza kuanguka kwenye uchaguzi wa mwaka 2015. Wengi walishangaa kusikia kuwa kumbe Kikwete hajui kuwa CCM kilianguka miaka mingi iliyopita sema imeinuliwa na mbinu chafu kama vile kuchafuana mingoni mwao kumpata mgombea wa urais kama ilivyotokea mwaka 2005.
Kitu kingine ambacho inaonekana Kikwete amesahau ni ukweli kuwa CCM kama si kuokolewa na tume yake ya uchaguzi kwa kuiruhusu ichakachue uchaguzi na matokeo yake, ingekuwa historia kama UNIP (Zambia), KANU (Kenya), NP (Afrika Kusini) na MCP (Malawi).
Je, ni kwanini rais wa nchi na mwenyekiti wa chama tawala anakosa habari kama hizi kiasi cha kujua kuwa kumbe chama chake kilianguka miaka mingi tangu kilipobinafsishwa kwa mafisadi na wasanii?
Hivi Rais Kikwete hajui kuwa chama anachokiongoza kilianguka tangu siku kilipozika maadili ya uongozi na kupwakia madili?
Hivi Kikwete hajui kuwa chama chake kilianguka siku kilipotoa ahadi lukuki kisitimize hata nusu?
Hivi kwanini Kikwete haambiwi na washauri wake kuwa CCM kilianguka zama zile kiliporidhia kutumia pesa ya wizi kutoka kwenye taasisi za umma kama BoT (ujambazi wa EPA) kuwahonga wapiga kura na kuchakachua matokeo?
Hivi kweli kujua haya kunahitaji shahada ya uzamivu kwenye masuala ya siasa? Je, Kikwete na wenye mawazo kama yake wanaishi nchi na dunia gani?
Ili kujionea rais anavyoishi kwenye dunia ya kufikirika, hebu angalia nukuu hii iliyomnukuu akipokea maadamano ya kuadhimisha miaka 35 ya CCM huko Mwanza.
Alisema: “Haiwezekani tukaendelea kuwa na watu wa hovyo, lazima chama kijipange na kujiweka sawa ili kisipoteze sifa kwa jamii,”
Hao watu wa hovyo zaidi anayewavumilia ni nani? Kwanini Kikwete awaone hao watu wake wa hovyo leo na si jana alipokuwa akitahadharishwa kuwa chama kinamezwa na mafisadi?
Tungeomba Kikwete atutajie hao watu wake wa hovyo kama kweli ameamua kuwa mkweli badala ya kupiga siasa kama kawaida yake.
Hivi kuna mtu wa hovyo kama aliyeahidi maisha bora kwa Watanzania wote akaishia kuwapa dhidi wote? Hivi kuna mtu wa hovyo kama yule aliyesimama jukwaani mchana kweupe kuwapigia kampeni watu wa hovyo kama watuhumiwa mbalimbali wa ufisadi ambao ni wabunge kwa sasa?
Hebu angalia janja ya Kikwete. “Hivi karibuni nikiwa na NEC hapo Dodoma, nilitumia kauli ‘Nyoka Kujivua Gamba’. Usemi huo ulienezwa tofauti kabisa. Kimsingi tulipitisha maazimio mengi, lakini wenzetu wameona azimio moja tu la kujivua gamba.”
Kuna jambo baya kama kauli hii isiyo na hata chembe ya ukweli? Kwanini Kikwete hasemi ukweli kuwa baada ya kuambiwa kuwa naye ni gamba hakuona haja tena ya kujivua gamba kwa maana aliyepaswa kuvuliwa kwanza ni yeye kabla ya kuwaambia wengine wenye magamba mepesi kujivua magamba?
“Wito wa kujivua gamba haujapewa mwitikio mzuri. Tumetupa mpira huo kwa wanachama kuwawajibisha viongozi hao, maana tunawafahamu. Sasa kazi kwetu sote,” anaongeza Kikwete.
Hivi Kikwete anataka kumdanganya nani kwa kuwatupia wanachama mzigo wakati wanachama walisharidhia vikao vya chama viwawajibishe magamba ambayo hayakutaka kujiwajibisha? sasa ni nini mantiki ya kupoteza pesa ya umma kufanya vikao iwapo jukumu lenyewe liliachwa kwa wanachama wasio na mamlaka yoyote kikatiba kuwawajibisha viongozi wao mafisadi?
Je, huku ni kuchanganyikiwa au kuishiwa kiasi cha kusema vitu vinavyopingana kwenye jukwaa moja na kwa wakati mmoja? Je, hapa wa hovyo ni nani? Nikijibu watasema Nkwazi Mhango siku zote ni mchochezi.
Kwa vile lengo la makala hii ni kutaka kuthibitisha kuwa watu wa hovyo ni viongozi wa CCM, tunatoa nukuu ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, ili wasomaji wapime pale alipokuwa akiongelea tuhuma za kujivua gamba.
Alisema: “Hata Waingereza wana tabia moja. Wakiona jambo linawasumbua, wanaunda Royal Commission, jambo hilo litachunguzwa kwa muda mrefu. Wakimaliza, watu wameshasahau.”
Mukama aliongeza: “Kufukuzana si dawa, si unaona jinsi jamii ilivyowageuka NCCR Mageuzi kwa kumfukuza David Kafulila au kufukuzwa kwa Hamad wa CUF? Sisi tumesema, kufukuzana si suluhisho, utakuwa unashughulikia tu dalili wakati ugonjwa wenyewe haujaufikia,”
Kwanza ni vigumu kuamini kuwa Mukama anaweza kujipayukia bila kujua anachosema ni nini na kinaweza kutafsiriwa vipi.
Sasa kama njama ya CCM ni hii ya kufanya mambo kijanjakijanja ili wananchi wasahau, Rais Kikwete analalamika nini au kutoa ushauri wa nini juu ya kufukuzwa watuhumiwa wa ufisadi. Huu si unafiki? Maana kama uongozi wa juu umeunda CCM royal commission ili kuwasahaulisha wananchi halafu mtu anakurupuka na kusema eti wananchi wataamua, wataamua nini iwapo wakubwa wamekwisha kuamua?
Je, hapa kama wananchi tufuate ya nani hasa ikizingatiwa kuwa Kikwete ana tabia ya kujipinga?
Rejea juzi juzi waziri mkuu Mizengo Pinda na Spika wa bunge Anne Makinda waliporipoti kuwa alikuwa ameidhinisha kulipwa nyongeza ya posho lakini baadaye akawageuka.
Kwa wanaoona CCM inavyozidi kuchanganyikiwa wakati ikipitisha hili na kulipinga hana sababu ya kuhofia kuwa haitaanguka kwenye uchaguzi ujao.
Wakati Mukama akisema hivi vigogo wengine wanasema vile. Hebu tumalizie kwa maneno ya waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye aliyesema sambamba na Mukama: “Hatuwezi kuwa na chama imara kama hatukuondoa magamba, mwenyekiti wetu wa chama taifa lazima tuyaondoe magamba yanayokipaka chama matope.”
Kama kuna kitu kitaiachia makovu ya kudumu CCM si kingine ni dhana ya kujivua gamba ambayo iliuawa baada ya rais mwenyewe kutajwa kuwa ni gamba, tena nene, ukiachia mbali magamba mengine kujua udhaifu wake na kugoma kuachia ngazi kama yalivyotakiwa. Je, kwa namna hii CCM ianguke mara ngapi?
Chanzo:Tanzania Daima Februari 15 , 2012.
No comments:
Post a Comment