NATUNGA kitabu. Najua wengi wakisoma hapa wataanza kucheka na hata kubeua midomo. Watasema mengi hasa wasiojua Mpayukaji ni kiumbe gani.
Watasema natafuta umaarufu kama jamaa yangu mtunzi mwenzangu na swahiba yangu Pio Kuchekwa aliyezindua buku lake la kujilisha ujiko kuwa alipata ukomavu toka kwa mzee Nchonga mwana wa Musa wakati si kweli.
Kama kuna mwanafunzi mzuri wa Mzee Nchonga si mwingine bali mimi Mpayukaji Nkwazi Nkuzi Mhango mtoto wa mzee Waambie Waipate bin Message Sent aka Mnenahovyo.
Mie ni mwanafunzi msikivu, mkweli na jabali wa mze Nchonga kwa sababu ya nifanyayo na kusema.
Ushahidi wa kwanza ni kwamba licha ya kupayuka mie si fisadi wala kilaza kama wale. Ndiyo maana katika tabu langu nililotunga liitwalo Kuambiana Ukweli sikugusia popote nilivyokuwa mwanafunzi hodari wa mwalimu.
Maana huwezi kuwa mwanafunzi wa kweli wa Mwalimu Nchonga ukakubali kujirahisi kulala kitanda kimoja na mafisi, mafisadi na wasanii. Never. Never on my dead body. you cannot be in bed with blood suckers and all hellbent thieves and whatnot as far as corruption is concerned.
Samahani nikichukia huwa naongea kiinglishi. Hivyo, msomaji nisamehe kwa kuzobokwa ung’eng’e sina maana ya kujionyesha kuwa nimechimba sana. Hata hivyo, si vibaya kuongea umombo kuonyesha nilivyochukia kama mwalimu wangu alivyokuwa akifanya akichukia.
Wengi hawatakisoma kitabu changu kutokana na wadanganyika kutokuwa na utamaduni wa kujisomea vitabu zaidi ya vya udaku. Kitasomwa na wenye pesa kwa vile kitakuwa ghali.
Hakitafundishwa mashuleni kutokana na wizara ya elimu kuamua kueneza ujinga badala ya elimu kwa kupiga marufuku vitabu mbali mbali kutumiwa mashuleni kama zamani.
Kitabu changu hakitapendwa na wengi kutokana na kutumia lugha kali na ya wazi kuwalenga walaji wa kaya hii.
kitabu changu kitapigwa marufuku na kama si kununuliwa na wabaya wa kaya na kukichoma moto ili mawazo yangu yasijulikane kwa wale wenye ujasiri na ustaarabu wa kujisomea ingawa si wengi.
Najua kitabu changu kitachomwa moto ingawa mawazo yangu hayataungua. Pesa ya ufisadi itatumika kununulia kitabu hiki na kukichoma bila kujua wanachoma pesa yao na si mawazo yangu adhimu.
Watashindwaje kukichoma ili watu wetu waendelee kusoma udaku na si mambo ya kuwapanua na kuwakomaza kiakili ili siku moja wajikomboe. Baada ya kutoa tabu hili nililowatajia hapo juu, napanga kutoa kingine kiitwacho Saa Ya Ukombozi. Samahani, msidhani naiba jina kutoka kwa kitabu kingine kama hiki ambacho nilikiona sehemu fulani. Huko mie siko.
Kitabu changu kitazinduliwa kimya kimya na makapuku maana sina pesa nyingi ya kuwahonga wazito kuja kukizindua. Watakizinduaje wakati kinawavua nguo kwa kuuzindua umma kuwafanyia kweli.
Kitabu changu hakipendwi kwa vile kinafichua siri za uongo usanii na wizi wanaofanyiwa walevi na wale waliowaamini wasijue ni mbwa mwitu na majoka.
Mie sihitaji wazito kuja kukizindua kwa vile najua huwa hawana muda wa kusoma ingawa wana pesa ya kununua vitabu. Wangekuwa wanasoma wasingefanya madudu wanayofanya.
Maana madudu mengine yanayofanyika hayahitaji kuwa na digrii kuyajua bali tabia ya kujisomea na kujielimisha. Msiseme nawasingizia. Hivi kujua kuwa kinachoendelea kwenye kaya chini ya uchukuaji unaopambwa kwa kuitwa uwekezaji wakati ni ujambazi kweli kinahitaji kuwa na shahada? Mbona mikataba yote ya kijambazi imesainiwa mbele ya wanasheria tena wenye shahada na mawaziri wao wenye shahada pia?
Hivi kujua kuwa na miji michafu ni uzembe wa kupindukia kuna hitaji shahada? Hivi kujua kuwa kaya ina vyanzo vingi vya nishati lakini inazidiwa na vijikaya visivyo na vyanzo hivi nako kunahitaji shahada? Hivi kuwawajibisha wezi wa Kagoda EPA, Richmonduli na Downs nako kunahitaji shahada yarabi?
Hivi kujua kuwa kupeleka wagonjwa ugabacholini wakati tuna wataalamu na hospitali ni aibu nako kunahitaji shahada? Kama ni hivyo basi mie sina haja na shahada za namna hii ambazo zinatolewa kama njugu ukiachia mbali kughushiwa kila uchao.
Narudia. Mimi Mpayukaji Nkwazi Mhango Nkuzi Msemahovyo sitaki shahada za namna hii. Sihitaji shahada za heshima wakati ni za dharau wala za kughushi kama za wale jamaa ambao walipotajwa wakaweka mkwara kuwa wangemshitaki Keinerugaba wakaishia kunywea. Shitakini mvuliwe nguo hadharani. Kwani nyie si vihiyo hata kama mko kwenye ulaji mliopewa na vihiyo wenzenu?
Kabla ya kusahau, inabidi niwaeleze ukweli kuwa ukiniondoa mimi, ima wanafunzi wa mwalimu Mchonga walikufa au kama wapo kiroho ni wafu. Kama wapo basi ni wale ambao hawakumwelewa.
Kama wapo ni aina ya kina njomba Tunituni Denjaman Ben che Makapu aliyeishia kumtia aibu mzee Nchonga pamoja na kumbeba tena kwa lawama lukuki.
Hawa ni wengi. Kimsingi, hata kama waliingia kwenye darasa la mwalimu hawakuelewa na kama walielewa ni wakati ule siyo sasa. Nionyeshe mwanafunzi wa Nchonga aliye hai kimaadili zaidi ya mimi nitajinyonga ni mfuate kuliko kuendelea kushuhudia anavyodhalilishwa na kila mchumia tumbo na mpenda sifa kama Pio kuandika mitabu ya kujisifu wakimhusisha.
Ningekuwa na mamlaka mwaka huu ningenyonga mtu kutokana na kuendelea kuwapo wezi wanaotaka kuchuma kupitia mgongoni mwa mzee wetu Musa.
Komeni na kama hamna la kufanya basi kauzeni nyanya badala ya kuuza uchafu wenu kwa kuuficha nyuma ya mzee Musa Mungu amweke mahali pema peponi gwiji huyu.
Ngoja kwanza nilie kidogo nikimlilia gwiji huyu anayedhalilisha na kila kinyamkera kwa kudai eti ni wanafunzi wake. Mngekuwa wanafunzi wake mngelala kitanda kimoja na genge la mafisadi waitwao chama cha mafisadi?
Mngekuwa wanafunzi wake mngejaza watoto wenu kwenye kazi nzuri ughaibuni kwenye balozi za kaya? Shame on you all. Kwa uchungu na majonzi niliyo nayo siwezi kuendelea. Acha niendelee kulia nikijililia kwanza kwa yatakayowakuta watu wa mzee Nchonga.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 15, 2012.
No comments:
Post a Comment