Tuesday, 7 February 2012

Mpayukaji aidhinisha posho na kuzikana

NI makosa ni vibaya mnafanya wazazi
Ni aibu ni huzuni iyo yoyoo
Iwapo mzazi humpendi mwanao,
Nasi wa pembeni tutampenda vipi?

Uchungu wa mwana aujuaye mzazi
Ni wazi mwaelewa lakini mwafanya hivyo

Ni makosa ni vibaya mnafanya walaji
Ni aibu ni huzuni iyo yoyoo
Iwapo mkuu huwajali watibu
Na wagonjwa watawaheshimu vipi?

Uchungu wa kodi aujuaye mlaji eehe
Ni wazi mwaipata lakini mwafanya hivyo

Mkuu wajua kila kitu ni hovyo
Lakini wajifanya hamnazo bure
Siku utakapokuja uona ukweli
Utakuwa uso kwa uso na pilatoee

Huwezi kuamini mzee Maneno aliingia kijiweni akiimba wimbo huu kunitupia vimondo asijue mie ndiye bingwa wa mipasho na vimondo. Alipoendelea kuimba bila kujali mie nilikuwa pale na namuona na kumsikia niliamua kuuliza ni kwanini alikuwa akinikosea adabu. Mzee huyu mshenzi kweli si alijitetea kwa kusema, ‘No’. ubeti wa pili nimekosea. Nilitaka kumaanisha wazazi na watoto na si wakuu, walaji na wa tiba na wagonjwa. Kwani nani mgonjwa hapa. Anyways, unayesoma, zingatia yote isipokuwa ubeti wa pili. Mzee huyu alipayuka msameheni hajui alilokuwa akifanya. Wakati mwingine njaa yaweza kusababisha kichaa. Hayo tuyaache. Kwanza huu muziki wa Les Wanyika wa zama zetu ushanitibua nyongo. Ngoja niachane na mambo ya kuimba niingie kwenye mada ya rero. Tulimalizanaje na mzee Maneno? Hayakuhusu. Acha umbea.

Baada ya kurejea na hangovers za Davos, nilijikuta nikishauriana na mshirika wa Bedroom kuongeza posho za makalio za wanywa kahawa. Msianze kuhoji kama mimi ni fisadi au fisadi mtoto. Jamani mimi si Rizikione wala sina uhusiano na ulaji wao. Najua matahoji huyu jamaa kapata wapi pesa ya kutoa hata posho ya makalio kwa wanywa kahawa. Msijihangaishe. Mshiko niliopewa kwenda Davos ulitafunwa wote kule. Ninachoiita posho hapa si kingine bali kahawa ya dezo kwa wanywaji kahawa hasa wale wanaowakilisha walevi.

Nikiwa nimetoka zangu kuosha macho kule Davos nilikopiga picha na wazito kama sina akili nzuri, sikujua kuwa kumbe nilikuwa nimerejea Uswekeni kwenye matatizo ya kujitakia na kutakiwa. Sikujua kuwa kumbe Davos ilikuwa ni kisingizio cha muda. Sikujua kumbe matatizo niliyokuwa nimekimbia yalikuwa yamezaliana na kuongezeka kiasi cha kunitia majaribuni. Huwezi kuamini. Niliposhuka toka kwenye pipa na kuwasili nyumbani, nilikuta malalamiko hasa kutokana na wambea waliosoma habari zangu kwenda Davos. Nilijilaumu kwa nini sikuwaonya kuwa baada ya kusoma hawakupaswa kuwaambia watu!

Kwanza, nilikuta mshirika wangu wa bedroom amenuna baada ya kuambiwa kuwa nilikwenda kule kujivinjari na totoz na si kujifunza jinsi ya kuwa na nidhamu ya matumizi kama nilivyoeleza kwenye taarifa yangu ya wiki jana.

Kwa vile mie ni bonge la mjanja, hili halikugeuka tatizo. Kwani nilikuwa nimemfanyia shopping ya viwalo ya kuua mtu. Michuchumio na mi-gold nilivyotoka navyo Paris nilikopitia toka Davos vilimlainisha kiasi cha kusahau madai yake. Kilichonikera ni wanoko wa kijiweni kutojali kuwa nilikuwa nimetoka kutumia. Hivyo nilipaswa kupewa muda wa kupumzika.

Kumbuka, nilipoondoka kwenda zangu Davos, niliacha mgomo wa wanywa kahawa waliotaka waongezewe nyongeza ya posho ya makalio yaani vikombe na kashata ili kuendelea kuchangia kijiwe. Kadhalika niliacha minung’uniko ya waonja kahawa na mabwana usafi kijiweni.

Ajabu kina mgosi Machungi niliokwenda nao kutanua Davos wao hawaulizwi kitu isipokuwa mimi kwa vile ni mkuu wa kijiwe. Nasikia hata wapishi wa kahawa nao wana mpango wa kugoma wakidai kuongezewa ujira wao. Watashindwaje kudai iwapo sisi wanywaji tusiofanya chochote tunaongezeana posho na marupurupu ya makalio na makoo hata kuuchapa kijiweni?

Sikujua kuwa kumbe kukurupuka ni ugonjwa na tabia mbaya sana. Baada ya mshirika wangu wa Bedroom kunishauri kuwa lilikuwa jambo jema kuwaongezea motisha na posho wanywa kahawa, niliona ni jambo bora sana. Niliamua kuandika kimemo na kumpa mzee Machungi atangaze tena bila kupindishapindisha kama yule jamaa wa kupinda anayecheza makidamakida na yule Ana Makimba. Jamaa bila ajizi likatangaza kuwa mzee mheshimiwa Dk Mpayukaji ameongeza posho na ulaji wa wanywa kahawa! Lololo! Kama nilikuwa nimeingiza kidole kwenye kichuguu! Walevi walivyohanikiza kunipinga na kunilaani na wengine kuniita kilaza sina mfano.

Nilipoona maji yamezidi unga nikaamua kumruka mgosi Machungi kwa kusema kuwa nilimshauri yeye na mshirika wa bedroom watumie busara kuona kama kulikuwa na haja ya kuongeza ulaji wa wanywa kahawa ambao kijiweni hupenda kuuita posho ya makalio kama ya wale waheshimiwa wanaoongoza kuuchapa usingizi kwenye njengo.

Brother Wahasira upo? Ila jamaa zako wa Chakudema wanachapa kazi nzuri wakati wewe ukiutononoa na kupewa posho ya makalio, usingizi, kupayuka, koo hata kuongopa. Kwanza niseme. Genge lenu limeniponza. Kwani walevi waliposoma kwenye magazeti kuwa nanyi mmeongezewa mshiko wa makalio na mkuu wenu nao si wakaanza kudai mshiko au posho ya makalio ingawa wao wanalipwa kahawa na kashata!

Nasikia hata mkuu wenu amejifunza kuchomoa toka kwangu. Tofauti ya kijiwe nanyi ni kwamba nyinyi mna fweza nyingi ila hamna akili nzuri ya kuitumia zaidi ya ufisi na ubinafsi wenu wa hovyo.

Hiyo pesa mnayotanulia na kuingiza kwenye mifuko binafsi ingeletwa kijiweni tungeweza kuachana na kunywa kahawa na kunywa mvinyo tena ule wa champagne ambao wachovu wengi wameujua kupitia kwenye harusi basi. Hata hivyo mimi niliubwia sana nilipokuwa Davos ndiyo maana nikarudi na hangovers kama mia na ushei hivi. Hayo tuyaache mtamalizana wenyewe na mazabe yenu.


Chanzo: Tanzania Daima Februari 8, 2012.

No comments: