Wednesday, 1 February 2012

Mpayukaji aenda kutanua Davos

NAJUA wasomaji wengi wanaona kama stori hii ni kamba za kawaida wasijue ni ukweli mtupu. Kwanza mimi si msanii wala mjingamjinga kujipinga au kufanya vitu vinavyoweza kunitokea puani.

Kwa taarifa yenu ni kwamba nimeanzisha NGO ya ulaji ambayo iliniwezesha kupata wafadhili kwenda kuhudhuria mkutano wa kiuchumi na ulaji matanuzi na mambo mengine kule Davos Uswisi. Chunga sana ni Uswisi si Uswazi wala Sweden kama baadhi ya magazeti yalivyoandika hivi karibuni. Hivi hata neno dogo Swiss nalo linawashinda waandishi wa siku hizi?

Wanaobisha kuwa sikuwa Davos ngoja niwape vipande. Mkutano wetu wa ulaji wa waliwaji ulifunguliwa na dada yangu na mwanafunzi mwenzangu Dk. Angela Merkel, ambaye alinipongeza sana na kusema kuwa huwa ananikumbuka nilivyokuwa kipanga darasani. Tulipiga picha pamoja na kubadilisha business card na kila mtu akaenda zake. Niliandamana na marafiki zangu kama kumi na watano hivi, akiwamo mfotoaji wangu binafsi, Mwidini Michozi
Hayo tuyaache.

Baada ya wafadhili kunipa yapata dola kama 250,000 kwa ajili ya matanuzi yangu na watu wangu, tulijitoma kwenye pipa la Katari na kutua zetu kule kwenye kiwinta na kula mikuku na mitotoz. Jina la kampuni iliyonifadhili naweka kapuni kuogopa Matonya wetu wakubwa na wadogo kwenda kule kubomu na kututilia kichumvi. Si unawajua tena Waswahili walivyo na mitima nyongo.

Katika msafara huu ingawa nasema nilikwenda na watu 15 totoz zangu zilikwenda kivyake ili wanoko wasinishtukie na kumpa taarifa bi mkubwa ingawa hawezi kufanya kitu ikichukuliwa kuwa naye ananichuna kwa kutumia mamlaka yangu kijiweni. Kwani yeye hana washikaji wake wanaonilia vyangu? Anadhani sijui?

Hakuna kitu kilichonifurahisha kama kwenda kwenye ma fauna na kwa wataalamu wanaoitwa chiropracticians au madaktari wa kuchua mwili. Najua wale washenzi wakisikia neno kuchua wanaanza kufikiri upuuzi. Hapa namaanisha kukandwakandwa na kunyooshwa kila kiungo. Kitu kimoja sitawaambia ni kwamba wale wadada wanaofanya udaktari huu lazima wawe bila ngu… we koma! Wakati jamaa zangu madaktari wamegoma, niliamua kwenda kule kula upepo na kujitibia kwa kukandwakandwa. Kitu kingine, kule Davos hakuna dini wala ushehe. Unakata kilaji kama huna akili nzuri. Hayo tuyaache.

Kule Davos nimejifunza mikakati mipya ya kukuza uchumi wa kijiwe hasa kuhakikisha kuwa kila tone la kahawa inayochemshwa linaingizwa kwenye kitabu cha mapato.

Mbali na la usimamizi wa mapato, mengine niliyojifunza Davos ni kama ifuatavyo:

Mosi, kuondoa au hata kupunguza ofa za hovyo hovyo kwa wale ninaowalipa fadhili kutokana na kunisaidia kuukwaa ukuu. Hapa akina Silvia Rweyependekeza nadhani wananipata.

Pili, kufanya kampeni kuhamasisha watu kunywa kahawa na siyo gongo na upuuzi mwingine.

Tatu, kupunguza au kufuta ushikaji na kujuana kwenye kijiwe ambapo watu wamekuwa wakija na kunywa kahawa bila kulipa hata kukopa pesa za kijiwe kwa vile eti wananijua mimi au ni ndugu au marafiki zangu. Huu ni ukupe lazima ufe mara moja.

Nne, kumnyang’anya gabacholi Kanji mraji wa makaa kutokana na kuutumia kuibia kijiwe kwa kuanzisha ujambazi wa mkaa almaarufu Richmonduli, Downs, APITIELO na mwingine.

Tano, kuchemsha kahawa kwa umeme badala ya mkaa. Maana naona mkaa licha ya kuchafua mazingira umechafua hata maadili kutokana na kashfa tajwa hapo juu.

Sita, kupambana na mgawo wa umeme ili kuwepo na nishati ya kuchemshia kahawa. Hapa najua lisirikali litanichukia kwa vile nataka kuingilia ulaji wao kwa maslahi ya wana kijiwe changu. Hata hivyo nitajaribu. Maana mie simuogopi mtu awe Njaa Shibe au Kapinda mie namvaa tu.

Saba, kupandisha bei ya kahawa na kuhakikisha wanywaji wanalipwa kwa dola. Hii ni kutokana na madafu kuporomoka kila uchao kama mabua.

Hatua ya nane ni kuhakikisha nampiga stop bi mkubwa kuacha kuchota fweza za kashata. Kinachokera sana ni kwamba anachukua na mashoga zake nao wanakuja kuhomola nikimuuliza naye aniuliza kwani watu wangu si walaji? Kitu kingine kinachonitia shaka ni ile ya bi mkubwa kutaka kutumia vita yangu ya kuhakikisha kuna uadilifu kuwa chanzo cha kuvuruga u-house wetu.

Hapa kusema ukweli amenishika pabaya. Hata hivyo napanga kumpa laivu kuwa kama anaona u-house wetu unashikiliwa na kumruhusu kuwa fisadi basi nitaoa mwingine ambaye atakubaliana nami. Mbona mchonga aliishi hadi kufa na mama Mary? Najua wanawake wote si kama Anna Tamaa au Shari Salima wa Njaa Kaya.

Anyway hilo nitalishughulikia nikipata time baada ya kutafakari mikakati yangu ya Davos.

Ukiachia mbali hiyo mikakati hapo juu na matanuzi mengine, kule Davos kulikuwa na party ya kupiga picha na wakubwa wa dunia hii. Nakumbuka. Hakuna kilichonifurahisha kama kupiga simu na Devil Kameruni, Go- down Brauni, Yakobo Zumaa wa Sauzi ambaye kwa totoz anaonekana kunitoa jasho. Kuna kipindi niliambiwa nikapige picha na wakuu wa kaya kama Hafkanisheitani na Pakasheitwan nikakataa kwa kujua walivyo matapeli na magaidi. Kama wingi wa picha ungekuwa fweza basi kijiwe kingekuwa tajiri kuliko kaya zote ulimwenguni.

Najua mijitu mingine isiyo na adabu inaposoma ujumbe huu inasema moyoni kuwa ni kamba. Kama mnadhani ni kamba nenda kawaulize wote waliohudhuria ulaji huu wakwambie kama hawakuniona tena nikijinoma mipicha ya madingi wa ulaji wa mataifa mbalimbali.

Unajua? Acha niishie hapa niende kutekeleza mipango kemkemu kutoka Davos. Basi nanyi waulize wakubwa zenu waliounguza kodi zenu kwenda kule wawaeleze walifanya nini na wamekuja na nini cha mno kama mimi. Kama watawadanganya njoo kwangu niwape siri zao. Maana kamera yangu ilikuwa ikimulika kila mchovu aliyekuwa Davos akijinoma.

Nauli yangu na watu wangu kwenda kule Uswisi ilitolewa na Baraka Obamiza. Ila hii ni top secret ya confidential tell nobody except yourself. You know what?

Chanzo: Tanzania Daima Februari 1, 2012.

No comments: