The Chant of Savant

Wednesday 1 February 2012

Jakaya anajifunza nini davos kila mwaka?


Kwa mtu anayejua uchumi wetu unavyoharisha huku toboatoba ya mafisadi ikizidi kuuzamisha, anashangaa uwezo wa rais Jakaya Kikwete kujifunza. Tunasema hivi kutokana na mazoea yake ya kwenda Davos Uswisi kuhudhuria mkutano wa kiuchumi wa dunia wenye lengo la kutoa mikakati na mbinu za kuimarisha uchumi duniani. Tunasema hivi kutokana na kutoona tofauti kiuchumi.

Kila unapofanyika mkutano wa uchumi duniani kule Davos Kikwete na walaji wenzake huwa hawakosi. Inaonekana hii tabia aliirithi toka kwa mtangulizi wake Benjamin Mkapa aliyesifika kwa kupenda kusafiri na kuhutubia mikutano ya kimataifa kuliko hata ya ndani kama alivyowahi kutuhumiwa na akaamua kujibu kwa ubabe. Hii siyo hoja leo. Hoja ni kutafakari nini anachotufanyia na kutuletea Kikwete kwa kwenda Davos kila mkutano huu unapofanyika. Sisi si wa kwanza kuuliza. Gazeti hili lilihoji na ikulu ya Kikwete ikatoa majibu ya kitoto kubwa likiwa ni kutafuta udhaifu wa kitaaluma zaidi ya hoja husika.

Swali muhimu na kubwa linalotusumbua ni: Je Kikwete hujifunza nini iwapo uchumi wetu ndiyo wa hovyo kuliko zote katika eneo la afrika mashariki? Hebu itazame sarafu yetu. Utazame mfumko wa bei na kupanda gharama za maisha. Kwa wanaokumbuka, wakati Mkapa akiondoka mfumko wa bei ulikua ni asilimia tano. Leo tunaambiwa ni 20%. Sarafu yetu inabadilishwa kwa takribani shilingi 1,500 kwa dola moja wakati mkapa akiondoka ilikuwa ikikaribia kufikia dola moja kwa shilingi 800. Je hapa tatizo ni nini? Je ni muarobaini gani Kikwete anaendea Davos? Je inakuwaje mtu aende kuogelea kisimani asitoke na tone hata moja la maji? Je tatizo hapa ni kisima au mhusika? Haya ndiyo maswali yanayopaswa kujibiwa na hao wanaomjibia rais kwa kutoa majibu ya kitoto. Wakati mwingine huwa tunashangaa watu kama hawa wanalipwa kwa lipi iwapo hawawezi hata kusoma hoja na kuzitolea majibu yanayoingia akilini! Je ni ile hali ya kupatikana kwa wahusika kwa mbinu chafu kiasi cha kuwa genge la kulipana fadhila?

Kitu kingine kinachomuweka Kikwete msalabani ni ile hali ya kuwa nchi yetu inaongoza barani kwa kuombaomba kiasi cha kuwa nyuma ya Afghanistan na Iraki kutokana na nchi hizi kusumbuliwa na vita. Swali jingine muhimu ni: Anajifunza nini iwapo tunaongoza katika bara la afrika kupewa misaada ambayo mwisho wake ni kufujwa?

Sitaki nionekane namkejeli Kikwete. Acha niulize :Je kikwete huenda kujifunza uwekezaji wa kijambazi wa mtangulizi wake ambaye naye alikuwa shabiki wa Davos? Kwa uchumi wetu, hii Davos siyo divorce jamani? Je kama uchumi wetu haufanani na Davos, ina maana Kikwete na wenzake anaoandamana nao wanakwenda kule kutanua kwa kufuja kodi zetu? Nakumbuka jamaa mmoja toka Sudan ya Kusini aliyerejea nchini mwake baada ya kupata uhuru. Msimuliaji wa kisa hiki ambaye ni rafiki yangu toka huko anasema kuwa siku ya siku kijana aliyekuwa amekaa Marekani kwa zaidi ya miaka kumi aliporejea kwao katika mji mkuu Juba, aliitwa na wazee. Wazee hawa walikuwa kumbe wamemuandalia bonge la ofisi na cha mno kulikuwa na kompyuta. Kwa vile nchi hii ni change na ina kiu ya maendeleo, wazee hawa walidhani kijana wao kwa kukaa nchi iliyoendelea naye alikuwa amepata angalau ujuzi hata uzoefu unaofanana nayo. Hivyo walimpeleka ofisini na kumpa kumkabidhi ofisi yake.

Jamaa alifurahi sana. Lakini kabla ya wazee kuondoka walitaka kijana awaonyesha atakavyotumia ile kompyuta. Bila kujua kuwa katika wazee wale kulikuwapo mmojawapo mtaalamu wa kompyuta, jamaa aliwasha kompyuta na kuanza kubabaisha huku na kule. Mara yule mzee mtaalamu alimwambia kuwa angetaka afungue programu ya Power Point ambayo si ngumu. Kijana alianza kutoa toa macho. Kufupisha kisa hiki, wale wazee waliamua kumpa kipigo cha mwizi.

Somo la kisa hiki ni kwamba lazima mtu afanane na mazingira anayoishi au aliyokwenda kujifunza sawa na rais wetu kuja na mikakati inayofanana na mkutano wa Davos badala ya kuja na picha alizopiga na viongozi mbali mbali mashuhuri duniani. Watanzania hawahitaji kuona sura za viongozi mashuhuri bali kuona mabadiliko katika uchumi na maisha yao. Hili kwao ni muhimu kuliko hizo picha na stori za mara tuliomba hili au tulijadili hili. We need actions not words and photo gallery from Davos.

Ni jambo la hatari kwa mfano rais kutumia shilingi zaidi ya 300,000,000 kwenda kufanya vitu ambavyo hata haviingii akilini. Tunasema hivi si kwa sababu ya uchochezi au chuki. Tuna sababu. Hivi kulikuwa na mantiki gani kwa mfano kwa rais kwenda zake Davos huku makamu wake akijichimbia mikoani (Lindi na Tanga) akifanya ziara za kupanda miti wakati madaktari wakiwa wamegoma? Je kupanda miti na kuhudhuria mkutano wa Davos ni muhimu kuliko afya za watanzania? Je ni watanzania wangapi walipoteza maisha wakati wa mgomo wakati viongozi wao wakiwa wanatanua nje ya nchi na mikoani? Mbona rais kwa mfano Mwai Kibaki wa Kenya hakwenda kule na badala yake alimtuma waziri mkuu Raila Odinga kutokana na kutaka kusikia wakenya walikuwa wanatafakari vipi hukumu ya Mahakam a kimataifa? Kwani kila mkutano lazima uhudhuriwe na rais au ni ile hali ya kupenda kusafiri na kukimbia matatizo ya msingi nyumbani? Tunamshauri rais Kikwete kubadili tabia na mapenzi yake ya kujali mambo ya nje kuliko ya ndani. Yeye si waziri wa mambo ya nchi za nje tena bali rais. Je kwa kukimbia matatizo ya msingi ya nyumbani, rais Kikwete amekuja na kipi cha mno kwa uchumi wetu uliko chumba cha wagonjwa mahututi (ICU)?
Chanzo: Tanzania Daima Februari 1, 2012.

3 comments:

dcny-ntilema said...

Ipo tofauti ya viongozi na watawala,ukiona kiongozi hajali maslahi ya wengi huyo ni mtawala anayekimbizana na maisha madarakani.

dcny-ntilema said...

Ipo tofauti ya viongozi na watawala,ukiona kiongozi hajali maslahi ya wengi huyo ni mtawala anayekimbizana na maisha madarakani.

Anonymous said...

click to view chanel purses with confident