Wednesday, 22 February 2012

Mlevi aanzisha kampuni ya simu

KAMPUNI hii inaitwa TapelitelCOM. TAPELITEL au kwa urefu Tanzania Affordable and Preferable and Economical long-distance and Internal Telephone ni kampuni mpya iliyoanzishwa na mjasiriamali mie.

Ujasiriamali wangu ni tofauti na wa wale walioamua kujitwalia mali za umma wao wake zao watoto wao hata wakwe zao. Nadhani bado mnawakumbuka ingawa hamkuwapa discipline kwa ujambazi na udokozi huu.

Kwa vile mie si kibaka wala fisadi, nimeamua kuanzisha kampuni halali na ya kisasa isiyo ya kisasi kama ya wale.

Mie siyo kama wale walipopewa ulaji waliamua kugawana hata raslimali za umma. Nenda kwenye miraba ya uwindaji huko maporini utajua nimaanishachoa. karibu kila mahali ni ulaji ulaji ulaji mtupu. Na hii ndiyo maana mafisadi na mafisi hawashughulikiwi kwa vile huwezi kujua nani ni nani. Usijekuta unayetegemea amkamate mwizi ndiye mwizi mwenyewe. hayo tuyaache.

Nilitaka kuita kampuni yangu ya simu WALEtel au World Airphone Longdistance and Abracadabra Telephones baada ya kugundua kuwa kumbe uwekezaji kwenye makampuni ya simu una ulaji usio wa kutoa jasho, Mlevi nimesukuti kuanzisha kampuni ya simu. Ingawa sawa na makampuni ya simu ya ulaji yaliyojazana Danganyika, kampuni ya mlevi imebeba neno tel na com kwa shingo upande.

Maana uzoefu umeonyesha kuwa makampuni yenye majina ya tel mwishoni ni tel kweli kweli. Unajua maana ya tel? Tell Everybody Lies kwa Kiswahili mwambie kila mmoja hasa mteja uongo. Hamjasikia ukipiga simu unaambiwa mara: namba unayopiga haipo, huna salio la kutosha hata kama unapiga kwa dola, mara utasikia: jaribu tena mwaka ujao, namba yako imerongwa, namba unayopiga ni ya mzito na anaogopa kupokea, mara unayempigia yuko chooni na upuuzi mwingine mwingi. Wajua maana ya Com? com imewekwa kuficha ukweli wa neno lenyewe yaani Con or tapeli.

Tapelitel haitakusumbua na nyimbo za dini wala rafu ili kukuibia maana hazitolewi bure. Maana unaburudishwa ili kupumbazwa uibiwe. Pia mchezo wa simu kupokewa na secretary ndani ya gari la bosi unaambiwa bosi katoka nje kamuachia secretary usukani na simu hakuna.

Mambo ya bosi yuko mkutano wakati yuko pembeni mwa secretary ni noma sana. Pia kampuni ya Tapelitel haitaruhusu ukupe wa watu kubeep beep au kupiga haraka na kusema naomba unipigie. Maana uzoefu umeonyesha kuwa wanaobeep au kupiga na kuongea kama machizi kuwa uwapigie huwa na shida zao wanazotaka kukwambia lakini kwa kutumia pesa yako.

Wao wanajiona wajanja huku wakikuona wewe juha. Siku moja mlevi amewahi kupigiwa simu na jamaa akaomba ampigie. Alipompigia alishangaa kusikia kupe huyu akisema alitaka kumbomu fedha! Yaani unibomu halafu kufanikisha kunibomu eti mie ni kupigie? I am not mad and stupid that way. Sorry saana.

Kwa wale wanaishi nje wanajua adhabu wanayopewa kwa kukatwa pesa nyingi kwa kuunganishiwa simu bila kuongea. Yaani inakuwa pale kugundua kuwa mtu anakatwa pesa simply because kusikiliza upuuzi na uongo uliorekodiwa kwenye memory ya kompyuta. Jamaa washenzi kweli. Wanaunganisha simu ukianza kuongea wanakata na kuishia na pesa yako. Utasikia kuwa huna salio mara simu imeugua na upuuzi mwingine.

Kampuni ya TAPELITEL inawaahidi huduma mulua na za kisasa na si za kisasi kama hizi za sasa. Tutahakikisha wenye makampuni yote ya kijambazi na kisanii yanayowaambia upuuzi kila mnapopiga simu yatafunga madudu yake na kurejea huko ushenzini yalikotoka.

Kwa vile taifa linataka mkombozi katika mawasiliano, Tapelitel mkombozi aliyesubiliwa miaka mingi inawaahidi huduma siyo hujuma bora kama ilivyo. Kwanza tutatoza kiwango kidogo cha kuunganisha simu kwa walioko nje. Hawana haja tena ya kupiga simu zao kupitia kaya jirani.

Kwa walio ndani ya kaya, mambo ya kuwa na mitandao elfu katika simu moja sahau. Tutawapa huduma bora karibu na bure. Ila kwa wale wanaotumia simu kusema uongo na kutongozatongoza hovyo wanafunzi, wake na waume za watu wajue ima watapandishiwa gharama au simu zao kukatika hovyo hovyo kama hizi za sasa.

Kadhalika Tapelitel haitawasumbua na matangazo ya kijinga au kampeni za kifisadi kwa kuhongwa pesa na wanasiasa kuwatumia ujumbe wa kipuuzi. Sisi tutahakikisha mnaongea mnavyotaka wakati mnaotaka na kwa mnaowataka mradi msivunje kanuni tulizotoa hapo juu.

Pia Tapelitel haitashiriki kwenye kamari ya jishindie hiki wala kile. Sisi badala ya kuwapa zawadi zitokanazo na kuwaibia tutawapa huduma mnayostahili. Tutalipa kodi ipasavyo na wala hatutabadili jina hovyo hovyo ili kukwepa kodi.

Kitu kingine tutakachofanya tofauti na makampuni mengine ya kijambazi ni kuhakikisha tunaajiri wazawa kwenye kila idara ya kampuni. Tuna shida gani kuajiri wakimbizi wa kiuchumi wakati kaya ina maelfu ya watu wanaomaliza vyuo vikuu ndani na nje?

Kwanini kuajiri watu wa kuja kuiba na kulia kwao huku wakiwaacha walevi wakiadhirika kwa umaskini? Kitu kingine, Tapelitelcom haitaruhusu wakubwa wenye uroho, wake zao au watoto na wapambe zao kuja kununua shea kwenye kampuni hii adhimu.

Kwa ufupi ni kwamba kampuni hii mpya inaahidi kuwakomboa walevi kutoka kwenye makucha ya wezi wanaoitwa wawekaji wakati ni wachukuaji. Tunaahidi mapinduzi ya hali ya juu kuhakikisha kuwa kaya yetu inakuwa mojawapo ya kaya zenye huduma bora za simu. kitu ambacho tunapaswa kuwaambia mapema ni kwamba, sisi hatuna mshikamano na wanasiasa.

Hatuhitaji msaada wa wanasiasa kwa vile hatuna mpango wa kuhujumu uchumi wa kaya kama wao kwa kuwahonga wenye mamlaka ili waendelee kututia umaskini. Kimsingi, Tapelitelcom ni simu ya kila mtu.

Ni simu ya jamii na mali ya jamii. Tuungeni mkono tutokomeze huu ujambazi wa mchana unaofanywa na watu wenye mtindio wa ubongo kwa kukubali kutumiwa kuwahujumu watu wao.

Ngrrrrrrr! ngrrrrrr! Nani huyu kanideep? Ngoja nimtwangie. Pwi,pwi,pwi, ngrrrr ngrrr. “Simu unayopiga ina mafua.” Kwaheri.


Chanzo: Tanzania Daima Februari 22,2012.

No comments: