Wednesday, 29 February 2012

Kupunguza ujumbe au kuchunguza ziara za Kikwete?

TAHARIRI ya gazeti hili ya tarehe 22 Februari si ya kupuuza. Suala ililolenga na kuliongelea ni muhimu sana kwa mustakabali wa uchumi wa Tanzania na watu wake. Kwa ufupi ni kwamba tahariri tajwa ilibeba kichwa cha “Msafara wa Rais nje upunguzwe.”

Mhariri alimuonea aibu Rais Jakaya Kikwete kwa kutaka msafara wake upunguzwe. Kimsingi, msafara wa rais Kikwete si wa kupunguzwa bali kuchunguzwa na kuwekewa masharti. Kama rais hana nidhamu ya matumizi wa chini yake wataipata wapi? Maana, pesa anayofuja na marafiki zake huko nje si zake bali za mlipa kodi maskini wa nchi hii. Hapa ndipo mzizi wa umaskini wa nchi yetu. Lazima waliomwajiri (walipa kodi) wajue aina ya watu anaoandamana nao na kwanini? Kwa nchi yetu ilivyooza, tusipozuia mchezo huu wa matumizi ya hovyo yasiyoangalia hali halisi ya kiuchumi, tutashtukia tukiwa tunalipia misafara sawa na ile ya akina Mobutu Seseseko iliyojazana marafiki, waramba viatu na wanafamilia ya mwizi huyu wa zamani wa DRC.

Niliwahi kuhoji ni kwanini msafara wa rais siku hizi umekuwa hata siri. ni juzi tu nilijua kuwa aliandamana na watu 40. Mara nyingi idadi ya anaoandamana nao inakuwa siri. Mbona wakati wa mwalimu Julius Nyerere licha ya kufanya ziara chache, ujumbe aliokuwa akiandamana nao ulikuwa ukitangazwa? Rais Kikwete amelalamikiwa mara nyingi ila ameziba masikio. Amefikia kuitwa majina ya ajabu ajabu kama mtalii, Vasco da Gama na mengine mengi kutokana na mapenzi yake ya kusafiri nje hata wakati akihitajika kutoa maelezo na uongozi nchini. Nani mara hii kasahau alivyokwenda kwenye mkutano wa uchumi wa Davos nchini Uswizi wakati wa mgomo wa madaktari uliosababisha vifo vya watu wengi?

Kwanini rais hataki kujua na kukubali kuwa ziara zake nje ni chanzo kimojawapo cha umaskini wa taifa letu na mfadhaiko wa uchumi? Je, ni kwanini rais anajali sana safari za nje badala ya watanzania wenye dhiki nyingi za kutengenezwa na utawala mbovu uliokumbatia ufisadi na matanuzi? Je, rais anafanya hivi kwa faida ya nani? Kwa wanaokumbuka shutuma zilizompata waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye alipotumia zaidi ya shilingi 500,000,000 kwenye ziara yake ya Marekani, wajaribu kufikiri. Je rais anatumia kiasi gani kwa ziara moja ughaibuni iwapo waziri mkuu zama zile wakati mfumko wa bei na gharama za maisha vilikuwa chini anatumia kiasi gani kwa sasa? Kwa mujibu wa taarifa za siri za kiuchunguzi, kufikia tarehe 9/9/2011 rais aliposafiri kwenda Kenya kwa ziara ya kikazi, alikamilisha ya 316 tangu aingie madarakani mwaka 2005! Hii maana yake ni kwamba tangu Rais Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, amekwisha kusafiri nje zaidi ya mara 300. Hii ukigawanya kwa miaka sita ambayo amekuwa madarakani ni kwamba kila mwaka amekuwa akisafiri mara 50 sawa na karibia mara mbili kwa mwezi au tuseme kila baada ya siku 20. Je, rais kama huyu anayekaa nje ya ofisi na nchi zaidi ya ofisini anafanya kazi lini?

Mbona marais kama Ian Khama wa Botswana nchi yenye uchumi mzuri Afrika hawasafiri kila siku? Mbona hapa jirani yetu Rais Mwai Kibaki hatumsikii akiruka kila uchao? Kuna nini kwenye biashara hii ya ziara za ughaibuni? Kwanini Kikwete hataki kuona na kuukubali ukweli? Je, hajui kuwa baada ya kuondoka madarakani hiki chaweza kuwa kikwazo kwake? Inashangaza kuona taifa lenye bajeti tegemezi kwa wafadhili kwa kiasi cha 40% kuwa na rais anayesafiri sana kuliko hata wafadhili wake. Ukifuatilia ziara za rais Barack Obama nje au waziri mkuu wa Uingereza na Canada nje, utakuta hazifikii hata hamsini, kwa mfano tangu Obama aingie madarakani, ni kwa utajiri upi Kikwete anatanua hivi? Kufikia tarehe 19/11/ 2009 Rais Obama alikuwa amefanya ziara 24 nje ya nchi tangu aingie madarakani na hili lilipigiwa kelele na Wamarekani. Kwa miaka minne maana yake ni kwamba kila mwaka amefanya ziara nane kwa mwaka wakati Kikwete akifanya mara zaidi ya kumi na mbili ya ziara za Obama! Ziara za Obama si siri; zina hadi Wikipedia yake ili anayetaka kujua aweze kujionea. Huu ndiyo uchumi na uwazi na ukweli na si matanuzi na maangamizi ya fedha za umma.

Kufikia tarehe 23/10/2010 rais mwingine anayeitwa mtalii na watu wake Zuma alikuwa ameishafanya ziara 40 chini ya miaka miwili tangu kuingia madarakani. Hata hivyo, baada ya kupigiwa kelele na wananchi wake, Zuma amepunguza ziara zake nje tofauti na Kikwete anayeendelea kuongeza ziara zake. Kwa wanaojua tabia ya Kikwete hawatashangaa kutokujifunza kwake. Hatabadilika. Maana hata alipoingia madarakani aliahidi kupunguza ukubwa wa serikali hasa baraza la mawaziri. Alifanya nini baadaye? Licha ya kuunda baraza kubwa la mawaziri kuliko la mtangulizi wake, aliongeza idadi ya wilaya na mikoa wakati uchumi ukiendelea kuporomoka kutokana na usimamizi mbaya na ufisadi.

Anachofanya Kikwete sawa na mwenzake wa Uganda ni kutumia pesa nyingi kuliko hata wizara nyeti. Mwaka 2011 kulikuwa na kituko ambapo Ikulu ya Uganda iliomba jumla ya sh za Uganda 5,055,000,000 kwa ajili ya safari za rais kwa miezi saba tu huku Wizara ya Maji na Mazingira ikitengewa sh bilioni 2.44 kwa mwaka 2010 na bilioni 3.228 mwaka 2011 kwa ajili mishahara ya miaka miwili. Wakati Ikulu ikitaka bilioni hizo 5.055 kwa ajili ya matanuzi ya Museveni nje, Ikulu hiyo hiyo iliomba pia Ushs bilioni 3.497 kwa ajili ya matengenezo ya magari ya rais huku mafuta pekee yakigharimu Ushs 120, 000,000! Wachunguzi wa mambo wanasemea kuwa Museveni alitumia jumla ya Ushs bilioni 13.386 ambazo ni zaidi ya mara nne ya bajeti ya Maji na Mazingira. Je, kwa watawala waroho na wabinafsi kama hawa Afrika inaweza kusogea mbele? Je, hawa si chanzo kikuu cha umaskini wa watu wetu? Je, rais kama Museveni au Kikwete wanatumia pesa kiasi gani katika utawala wao wote? Trillions of shillings of course. Kuna haja ya kuchunguza bajeti inayotengwa kwa ajili ya matumizi ya Kikwete. Chanzo: Tanzania Daima Februari 29, 2012.

No comments: