WENZENU juzi tulikuwa na uchaguzi wa kugombea ulaji mbalimbali
Kijiweni kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa. Katika uchaguzi wetu,
kulikuwa na mnyukano wa kufa mtu.
Vijana wengi ambao hatukuwa tukiwajua, walijitokeza na kutaka
kuwanyang’anya ulaji wazee wazima. Pamoja na jeuri ya vijana, ulaji wa
mwenyekiti, mke wake na maswahiba wake ulilindwa kwa gharama zozote hadi
kufikia kubadili sera ya kijiwe toka upayukaji kwenda ufisadi.
Ngoma kubwa ilianza kunoga pale wakongwe kama Dk. Mbwa Mwitu aka Eddie
Ewassa na Mchunguliaji aka Endelea Chenga kutakiwa watemwe kama
tulivyomfanyia Ewassa kwenye kashfa ya mkaa tuliyoibatiza Richomond
tuliyoasisi lakini tukamtoa kafara Ewassa Mbwa Mwitu ili kuokoa ulaji
wangu na wake.
Baada ya kumtosa niliamua kuendelea kumlipa marupurupu kama mzee na kiongozi wa Kijiwe aliyestaafu.
Kitu kimoja ambacho unayesoma hapa lazima ufahamu na kuzingatia ni
kwamba wakati tukipitisha ufisadi kama sera mpya ya Kijiwe, tunawaambia
wanakijiwe kuwa bado tutawakomboa na kuwapa maisha bora wote
tukihakikisha wanakula kashata na kunywa kahawa bila kikwazo na kwa afya
yao.
Ukiachia mbali tishio la vijana, kulikuwa na tishio la wake za watu
wasio na majina wala vyeo kutaka kuchukua ulaji wa wake na washikaji
zetu. Ngoma ilikuwa nzito hadi tukaanzisha mkakati wa kuondoa majina
kimya kimya bila kujali lawama.
Hivyo, hata umoja wa wake zetu nao ulikumbwa na misukosuko si kawaida.
Nakumbuka nyumba ndogo yangu yaani Bi Sofi Lion alitishiwa na mke wa
kigogo mwenzangu aitwaye Joni Malikula. Kama siyo busara kutumika, si
ajabu angekufa mtu. Kwa vile tunajua Kijiwe kina wanawake wengi na
tusingependa watumie wingi wao kuchagua mwenyekiti mwanamke, tuliingilia
haraka na kuzuia akina mama kutustukia kuwa tumekuwa tukiwatumia kwa
kuwapa nafasi uchwara za udohoudoho.
Hata Umoja wa Vijana ambao tumeuweka mikononi mwa vitegemezi vyetu
tunauangalia kwa makini sana hasa tukijua kuwa vijana na akina mama ni
wengi kuliko sisi vizee. Hivyo, wakijitambua na kujua janja yetu,
wanaweza kutunyang’anya ulaji wetu kirahisi. Wanaweza kufanya mapinduzi
ndani ya mapinduzi tukaishia kunyang’anywa maulaji yetu.
Pamoja na kufanikiwa kurejesha ulaji wetu, wale wahuni wote waliotaka
kutukosoakosoa kama Deo Filikumjomba, Nimlord Mkononi na wengine
tuliwatupilia mbali.
Hawa jamaa walituudhi sana walipotaka eti waziri mkubwa wa Kijiwe
ajiuzulu baada ya kuongopa na kufanya madudu. Kwa kuwashughulikia kama
tulivyofanya, wengi wenye mawazo mgando kama hayo watakoma kama siyo
kukomaa.
Kosa jingine walilotenda hawa jamaa ni kutaka eti wazee wa Kijiwe
walioghushi nao watupwe nje wakati ni washirika wetu. Akina Mare Nyagu,
Emmy Nchimvi na Willy Lukuvu walinusurika kutokana na sera mpya ya
kulindana na kulinda ufisadi.
Wakati tukiendelea kupongezana kwa kuminyana na kuokoana, wapinzani
wetu waliandika ujumbe ufuatao kwenye mtandao wao ambao anwani yake ni
siri.
Waliandika: “Kama wapinzani wetu wataamua kufanyia kazi hii sera mpya
ya Kijiwe ya ufisadi vilivyo, hawana haja ya kutafuta la kuwaambia
walevi wakaelewa. Upinzani uende vijijini na kutoa tafsiri ya hiki
kinachoendelea ndani ya Kijiwe. Uwaeleze walevi hasa wanywa kahawa kuwa
kile Kijiwe walichoanzisha na Ticha Mchonga kikaleta nafuu kilikufa
zamani.
“Wawaeleze ukweli kuwa kile Kijiwe hakikufa kifo cha kawaida bali
kiliuawa na nafasi yake kuporwa na wenye maulaji na dili, tena
zipatikanazo na kila aina ya jinai na ujambazi kama vile HEPA, Richomond
na mazabe mengine.
“Kwa wenye kupenda ukombozi wa Kijiwe chetu, wanapaswa kushangilia na
kukiombea kiendelee kufanya makosa kinayorudia kila mara ili kidhoofike
na kuondoshwa kama KANU kule Kenya.”
Waliendelea: “Ingawa baadhi ya vigogo waliokuwa wapeleke pigo la
mwisho kwa Kijiwe waliomo ndani wamekuwa wanafiki, woga na wababaishaji,
njia iliyochukuliwa na Kijiwe kwa sasa ina uhakika wa kuimaliza.
“Hata Usalama wa Kijiwe wafanyeje kulinda huu uchafu wa mchana, mwisho
wa Kijiwe kama siyo mwanzo wa mwisho umeishawadia. Ni vizuri kuwa sasa
Kijiwe hakina kiongozi hata mmoja mwenye visheni.”
Walinishambulia mimi na kusema: “Ukimwangalia mwenyekiti wake, kila
mtu anajua anavyopwaya. Makamu wake naye, hana udhu tena baada ya kashfa
za Ngorongororo na kujaza watoto wake kwenye balozi za Kijiwe nje
zimemmaliza kabisa. Zaidi ya hawa amebakia nani?”
Baada ya kusoma utumbo wao tuliamua kwanza tunyamaze na kumaliza
sherehe za kupongezana ili hapo baadaye tuje tuwashughulikie hata kwa
kuwanyotoa roho. Tutaazima vijana wa jamaa yetu Mwemamwema wawamwangosi
ili wakome kufuatilia ulaji wetu. Hatuwezi kuacha amani ya Kijiwe
ivurugwe na watu wanaotaka kutunyang’anya ulaji wakati ulaji wetu
tumepewa na Mungu na walevi wenyewe.
Hata kama walevi wanaliwa, wao inawahusu nini? Tulishasema kama
wanataka ulaji waende baharini wakavumbue vijiwe vingine kwenye visiwa
ambavyo havijakaliwa na mtu wakatawale na kula kule. Hawa hawana adabu
na wana tamaa kama jamaa zetu wa Uangusho wanaodai eti wanataka
watawaliwe kisharia wasijue kaya ina wenyewe na wenyewe ni sisi tusio na
dini wala nini.
Nasema tena. Haamshwi wala kuangushwa mtu. Nenda Arabuni muone watakavyowanyotoa roho watumwa nyie msio na macho wala akili.
Kwa ufupi tulichofanya ni kile wazungu huita ‘ballyhoos done by yahoos and yo-yos.’
Hatukuwa na jinsi bali kuendelea kutowaamsha waliolala, yaani vijana na akina mama.
Baada ya kuhakikisha kuwa wanamalizana wenyewe kwa wenyewe wakigombea
ulaji wa hovyo wa kupewa kwa kutumia jinsia na umri, sasa maulaji yetu
ni salama u salimini. Tunaendelea kupeta na kutesa bila noma kama hatuna
akili nzuri.
Hatufichi ujanja wetu. Tunasema tena kwa kinywa kipana - walevi
wajijue na wataendelea kuliwa na kuliwaga hadi wakome ubishi. Sisi ni
kijiwe chenye maarifa na sanaa kila aina vya kuwalewesha na kuwala
walevi mchana kweupe.
Naona niishie hapa niwahi home kumpa talaka mshirika wa bedroom
kutokana na kunitia hasira kama Wahasira kutokana na vijana wetu
kujiunga na CHAKUDEMA. Nitaua mtu leo!
Chanzo:Tanzania Daima Oktoba 3, 2012.
2 comments:
Stori refu hata unasahau mwanzo ulianza vipi ujinga mtupu
Yeah! Ukiwa na short attention span hii stori inahitaji siku nzima kuielewa. Unahitaji tuition?
Post a Comment