Tuesday, 5 November 2013

Kijiwe chaandaa matanga ya CCCM

BAADA ya rahisi Njaa Kaya kutangaza utabiri wake juu ya kifo cha Chama Cha Chagizo la Maulaji (CCCM), Kijiwe kimejiandaa kutangaza na kusherehekea kuondoka kwa kikwazo hiki katika maisha ya wanakijiwe.
Mbwa Mwitu, bingwa wa utani, ndiye wa kwanza kuingia uwanjani akiwa na tanzia yake. Bila wajumbe kutegemea, anachomoa karatasi mfukoni na kuanza kusoma yafuatayo:
“Ndugu Munene Mkubwa Jua Kali, anasikitika kutangaza kifo cha bosi wake marehemu CCCM kilichotokea kule Idodomya tarehe 24 mwezi Oktoba kutokana na kipogo kikali na kuchomwa moto baada ya kuzidi ufisadi na ujambazi. Habari ziwafikie dada yake marehemu Kanu akiwa Nairobbery Nyayo, mdogo wa marehemu MCP akiwa Lilongwe Maravi, mdogo wa Marehemu UNIP akiwa Lusakama, shemeji wa marehemu KAFU akiwa Pemba, NCCR-Maangamizi na TeLP wakiwa Moshi, UDDP akiwa Bariada na UPDPP akiwa Zaramo na ndugu na jamaa wote wanaohusika.”
Hata kabla ya kuendelea, Mgosi Machungi anamnyang’anya mic na kuchonga. “Mbwa Mwitu leo umetiacha hoi. Sikujua kuwa kumbe nawe unayamanya mambo ya sanaa!”
Bi. Sofi aka Kanungaembe alikuwa amefura nusu ya kupasuka. Alisema: “Ulichofanya mwenzetu si kizuri. Utatangazaje msiba wa chombo ambacho kiko imara na hai? Jaribu kuwa na adabu japo kidogo.”
Kabla ya Sofi kuendelea, Mijjinga anamchomekea. “Sofi acha hizo. Kama mkulu mwenyewe ametabiri kitakufa wewe ni nani kusema vinginevyo au ni yale yale ya kuishi kwa matumaini kama wagonjwa wa miwaya?”
Msomi Mkatatamaa hangoji waharibu mada. Anatia guu. “Kimsingi alichosema Mkulu si jipya. Watu tulishaona hili sema kwa vile sisi si maarufu na washitiri wa chama hicho, mawazo yetu yalipuuzwa.”
Mpemba aliyekuwa ndiyo amemaliza kusoma gazeti anakatua mic. “Yakhe mie jamaa kaniacha hoi wallahi. Kumbe naye atabiri kama rafiki yake yule Shehena Yahayaa?”
“Kwani kutabiri kazi? Si utapeli wa kawaida uliojificha nyuma ya kile mtu anachohisi kinaweza kutokea tu.” Anajibu Kapende huku akisogeza simu yake aliyokuwa ameiweka mezani.
Kanji naye hataki aachwe nyuma. “Mimi ona kama hii chezo. Hapana weza ua powerful parti like this. Kama naanguka sisi takwenda vapi jamani?”
“Mtakwenda wapi? Rudini kwenu au muamue kukaa na kujenga kaya badala ya kuiba na kutoroshea kwenu,” anajibu mzee Maneno.
Mipawa ambaye alikuwa kimya akisoma gazeti anaamua kukatua mic. “Beng’we, alichosemaga Mkuru ni ushindi kwetu. Je, hawa wapingaji nao wana uwezo wa kukamata madola bila kuiba?”
Msomi anajibu. “Dk. Mipawa swali na wasiwasi wako ni vya msingi. Kinachohitajika hapa si kuangalia sura za nani watashika nafasi ya marehemu. Kinachotakiwa ni kuweka mfumo thabiti unaoweza kuendesha nchi bila kujali nani yuko madarakani. We need to maintain the momentum seeing to it that we don’t backslide.”
Mzee Maneno anamkumbusha Msomi. “Mzee Kikameruni hicho (Yaani kimombo).” Maana kwa wengine wengi hakipandi. Wanajikubali kuliko kwenda kughushi kama akina Luukuuv na vihiyo wengine wanaojiita wasomi.
“Mimi mambo ya nani atachukua mikoba na kuiba nini hayanihangaishi kwa sasa. Kwanza tuzike na kusahau balaa hili halafu tuanze kuwasaka wabaya wetu walionufaika tokana na utawala wa genge hili hatari,” anadakia Kapende ambaye kijiwe humuita muhafidhina kutokana na kuwa na msimamo mkali kwenye masuala mengi.
“Dua la mwewe hilo. Wenzenu tunajiandaa kuwa na mgombea anayekubalika mheshimiwa Eddie Ewassa nyie mnaongelea mazishi hewa,” anabeza Bi. Sofi.
Mijjinga hamkawizi. “Hata kama umehongwa na kuharibiwa kiasi hicho, unadhani hata mafisadi na majambazi watapewa power tena? Kumbe nawe ni wa hovyo kama Joni wa kujikombokomba kwa fisadi mkuu! Nani anataka HEPA nyingine kwa kuchagua bwana Richimonduli? Mie siku jamaa akigombea nitajinyotoa roho kuliko kuingia mkenge mwingine.”
Msomi anadakia. “Hakuna kilichonichefua, kunifedhehesha at the same time kunichekesha kama mkuru kuanika madudu yao. Sikujua kuwa wenzetu wanahongwa upuuzi kama suti na kadi za simu.”
“Mkuu ulikuwa hujui kuwa kaya yetu inagawiwa kwa wezi kwa udohoudoho na upuuzi mtupu? Hukusikia kuwa hata wale majambazi waliotorosha wanyama wetu walikuwa na pasi za kidiplomasia?” Anazoza Kapende.
Mipawa naye hajivungi. “Mnaongelea suti! Mbona kuna wengine wanahongwa chupi.”
Mgosi anakatua mic. “Sasa tinaanza kuona mantiki ya uhishimiwa wa dezo. Kumbe kuna ulaji hapa!”
Sofi hakubali. “Mnajuaje kuwa wanahongana ngono kama si umbea, kwani huko kwenye mahoteli makubwa nanyi huwa mnakwenda au ni hisia tu?”
“Wewe kalia hisia na imani mfu. Utaliwa hadi ukome,” anabeza Mijjinga.
Kanji naye leo kaamua kuzoza. “Hii mambo ya chupi iko baya sema hadhani jamani.”
Mpemba hakubaliani na ushauri wa Kanji. Anakatua mic. “Kama wao wanofanya hawaoni aibu kwanini sie tufiche ati? Huu wakati wa uwazi na ukweli ati.”
Mbwa Mwitu aliyekuwa akisikiliza huku akisoma gazeti anaamua kukatua mic. “Nimesikia michango yenu nyote na majonzi na king’ang’anizi cha Bi. Sofi na Kanji. Ukweli ni kwamba CCCM ishakufa. Kilichobaki ni kuandaa maziko, tena ya kibudu.”
Kanji anamkata jicho la chuki Mbwa Mwitu huku akinong’ona jambo na Bi. Sofi na kuzoza. “Kila mtu takufa dugu yangu. Kama CCCM kufa nawe siku moja kufa. Nini bwana.”
“Kwanza si kweli kuwa mimi ni ndugu yako. Usinidanganye na dugu yako ya mdomoni wakati moyoni unanibagua. Ni kweli nitakufa. Lakini nitakufa kifo cha heshima. Hivyo siogopi kusema ninachoamini, tena kilichotabiriwa na mshitiri wako eti kwa vile Kanji na Bi. Sofi watachukia. Halo halo! Mwenye uchungu akajinyonge!”
Mgosi Machungi anakiacha kijiwe hoi. Anasema: “Wanaosema titakufa hawana maana. Tife maa ngapi iwapo tiishauzwa, kunyonywa na kuuawa kwa miongo mingi?”
Kanji haridhiki. Anazoza. “Gosi dugu yangu omba mimi samaha. Mimi iko mtu ya maana sana sana sana. Veve hapana jua tu.”
Mgosi hakubali. “Kama wewe ni wa maana ni kwa Bi. Sofi na magabacholi wenzako na hao wanaowatumia kutuibia na kuficha kwenu.”
Kanji kuona somo halieleweki anasimama na kuondoka huku akiwa amechukia. Nyuma Mgosi na Mijjinga wanamzomea. “Nenda mwana kwenda ukale dengu Bombay.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si tukashuhudia trafiki akitaka kushikishwa. Basi tulitoka mbio kwenda kumtia adabu.
Chanzo: Tanzania Daima Nov., 6, 2013.

No comments: