The Chant of Savant

Saturday 23 November 2013

Mlevi amuomboleza Dk. Mvungi



Kwa majonzi na moyo uliopondeka, mlevi leo kwa namna ya pekee anaomboleza kifo cha gwiji wa sheria Dk. Sengondo Mvungi aliyenyotolewa roho na walioitwa majambawazi.

Je! kweli aliuawa na majambazi au maadui zake wa kisiasa? Napata shaka hasa pale ndata wanaposema eti wamekamata bastola yake lakini si kompyuta mpakato au laptop kwa kimakonde. Je! kunani? Kwanini wapate bastola lakini washindwe kupata mpakato wake?

Sambamba na kuomboleza kifo cha Mvungi, naomboleza kifo cha kaya. Maana kaya si salama tena hasa wakati huu ambapo wanaopaswa kupambana na ujambazi wanaupamba. Imefikia mahali hata nikipata kanywaji na kuvuta mibangi yangu sijihisi raha kutokana na woga wa majambazi.

Sambamba na haya, naomboleza kifo cha njuluku zangu zinazoibwa kila siku na kutengeza mabilionea kwenye kaya ombaomba na kapuku ya kutupwa.

Kesho sitashangaa kusikia hata wauza dini wenye roho mtakachafu wanayemuita mtakatifu kuwa kwenye orodha ya mabilionea wetu wa kutia shaka ingawa si wote.

Hapa mzee Mengi na Bakhressa inabidi mnielewe. Sina ugomvi na ukwasi wenu. Waliobaki niwie radhi, sina imani nanyi. Nina sababu. Huwezi kuwa mtuhumiwa wa EPA, Richmonduli na Kagoda ukawa bilionea wa kweli zaidi ya kibaka na jambazi anayeitwa bilionea kwa makosa.

Huwezi kuwa mbunge anayelinda maslahi ya biashara uchwara za baba yako inayoitwa yako ukawa bilionea wa kweli. Hivi ubilionea mnaujua au mnausikia tu?

Huwezi kuwa bilionea kutokana na kukwepa kodi, kutorosha pesa yetu, kuwauzia walevi bidhaa mbovu na upuuzi mwingine. Kwangu wewe ni kibaka au niseme mbaka mkubwa tu hata kama kuna wanaokudanganya na kukuita mheshimiwa.

Wewe ni mheshimiwa anayepaswa kunyea debe Segerea na Ukonga. Bahati yenu mnao wezi wenzenu wanaowadekeza na kuwakingia kifua. Siku nikichaguliwa kuwa munene, nitawanyonga kama kuku kama si kuwapiga mpini kama mbwa mwizi. Nina hasira kutokana na jinsi ujambazi wenu ulivyomuua rafiki yangu Dk. Mvungi.

Turejee kwa Dk. Mvungi. Hakika alikuwa mlevi wa midahalo na muumini wa dini tofauti nami ambaye dini yangu ni kanywaji na tubangi na kubwabwaja.

Tulikutana kwa mara ya mwisho pale South Law Chembers aliyoianzisha na Dk. Harrison Mwakyembe mwaka 2002 pale Mnazi Mmoja mtaa wa Lumumba zilipokuwa ofisi zao.

Tulibishana sana juu ya uhalali na ukweli wa dini. Katika mabishano yetu alionyesha utaalamu wa kujenga hoja na kuhimili maswali yangu chokonozi na ya kilevi na kibangibangi.

Dk. Mvungi alikuwa mwalimu sawa na mlevi tofauti ni kwamba yeye hakuanzia ualimu kama mimi. Alifundisha chuo, nikafundisha sekondari ingawa kama majadiliano ninayofanya yataenda vizuri, niko mbioni kufundisha chuo lau niitwe lecturer au profesa. Hayo tumuachie mwenyewe bwana mkubwa aliyeko juu.

Dk. Mvungi alibobea katika sheria sawa nami niliyebobea katika ulevi na usuluhishi wa migogoro. Cha kujivunia ni kwamba alikuwa msomi wa kweli na siyo wale wa kughushi tuliowazoea kayani.

Historia yake inasema kuwa alianzia uandishi wa habari bila kuusomea wakati mimi nilianza uandishi kabla ya kuusomea na baadaye kuusomea.

Alipata shahada yake ya mwisho nje kama mimi ingawa hakufanya kazi majuu kama mlevi mwenyewe.

Nakumbuka, Dk. Mvungi alikuwa mwalimu wakati nikisomea sharia pale chuo kikuu cha Manzese ingawa hakunifundisha. Alikuwa mtu mchangamfu na mwenye kuchanganyikana na watu bila kujali makando kando ya vyeo na usomi kama viherehere, wanywanywa na malimbukeni wanaodhani kuwa kusoma ni kujitenga na watu wakati ni kuwatumikia na si kuwatumia kama ilivyo kwa wengi kwa sasa.

Alikuwa mpare ambaye hakuujua ubahiri. Alikuwa mtu wa watu tofauti na wengi wa hadhi yake waliojiona wametoka anga za juu.

Kitu kingine cha kukumbukwa ni kwamba alipenda haki sawa nami ambaye niko tayari kuifia kama alivyofanya.

Ukipenda na kutenda haki, ujue you are on the line those thinking you’re in their way will nary let you live longer. Again, is there any person who won’t return the number? Shame on Mvungi’s killers whoever they are! Looooh!

Naona mibangi na gongo vimechanganyikana na kupandana kiasi cha kunilazimisha kuongea kimombo na kisambaa, oh tate nane tate nane.

Thijui ninyamaze niache kuthema haya ninayothema au? Vudee mpo? Hi five basi!

Nalaani waliomuua, wawe majambazi au wanasiasa.
Katika kuomboleza kifo cha rafiki na msomi mwenzangu Dk. Mvungi, acha niushukie ujambawazi mbuzi. Ujambazi umekuwa tatizo linalolelewa na kuengwa engwa na wenye pawa kwenye kaya. Nasema ukweli hata kama ni kilevi.

Nilijisikia vibaya kiasi cha kutaka kugeuka gaidi nilipoona wale waliotuaminisha kuwa wanaweza kupambana na ujambazi wakati wakiupamba nao kwenda kuwahani wafiwa na kupewa nafasi za juu wakati kazi yao ndiyo matokeo ya kifo cha marehemu.

Wako wapi waliotwambia wana orodha za majambazi wakaishia kula na kulala nao? Niliumia kusikia kuwa majambazi wa Kagoda walitangazwa mabilionea kayani wakati wa msiba wa Dk. Mvungi.

Kutokana na hujuma aliyofanyiwa Dk Mvungi, mlevi napanga kuhamia uhindini Kariakoo na Posta ili kuishi mahali salama. Nikipanga kuhamia Oyesterbay na kwingineko kwa wenye nazo sitaweza wakati sina fweza ya ufisadi wala bwimbwi?

Acha nihamie kule tubanane huko hata kama sina sifa ya kuishi kwenye nyumba za dezo za Asajile Mwaijumba. Nitalazimisha hivyo hivyo hata kama sina magendo na dili za kuficha. Heri kuwa mtasha mweusi wa Kariyakoo au Postale kuliko kuwa marehemu nikiwa bado wamo. Kama wakubwa wameamua kututosa unategemea nifanye nini?
Kwa vile nina majonzi ya kuondokewa na mlevi mwenzangu, acha niende kupata kanywaji huenda nitaganga hasira na mavune yangu. Rest In Eternal Peace (RIEP) Sengondo Mvungi my friend. 

Chanzo: Nipashe Jumamosi Nov., 23, 2013.

No comments: