Sunday, 10 November 2013

Mlevi azimia wachina kuuza ndimu na vitunguu!

 
Kwa vile huku ughaibuni huwezi kutajirika wala kuukata kupitia wizi au ujanja na jinai nyingine, lazima nirudi home. Huku kila mtu anachopata au kutumia lazima aeleze umepata vipi. Kuna sheria ya kutaja mali inayowahusu wote bila kujali wadhifa wala nini. Huku kuwajibika maana yake ni kuwajibiki si kuwajibisha wengine wakati wewe huwajibiki. Huku hakuna unafiki, siasa wala ushenzi wa better than thou yaani mie bora kuliko wengine kama huko.
 Viongozi wanataja mali zao kila siku. Si kama huko ambako wanene huwahimiza walevi kutaja mali zao wakati wao wakificha zao. Si kama huko ambako wanene wanakula kodi za walevi wakati wao hawalipi kodi hata kama wanapokea mishahara ya mamilioni ya njuluku. Huku ujambazi, kama vile kukwepa kodi, kuuza bwimbwi au kuiibia umma haulipi zaidi ya kumuozesha mwizi lupango hata awe mkubwa na mhishimiwa vipi. Huku uongozi na uhishimiwa ni utumishi kwa umma na si kuuma umma kama ilivyo huko.
Baada ya wachina wauza vitungu na ndimu kukamatwa na vipande lukuki vya meno ya tembo, mlevi nimeanza kusukuti kurejea Bongolalaland al maaruf kama shamba la chizi ili kuzichanga njuluku. Ninapanga mambo makubwa.
Kwanza, sikujua kuwa Bongo inaagiza vitunguu swaumu kutoka uchina wakati huko Lushoto na mikoani vinaoza kwa kukosa soko.  Nilizoea kuwaona wachina wakijitoa kimasomaso na kuimba taarabu ya kimasomaso na kusoma magazeti ya Kiswahili. Sikujua kuwa hali inatisha kiasi hiki. Kumbe tuna India nyingine nchini!
Je wanene wetu watajenga majumba mengine ya msajili kuwaweka watu hawa wasiopenda kuchanganyikana ili kulinda biashara zao haramu au tutegemee African-China towns soon? Kumbe waliosema kuwa operesheni kimbunga ipo kwa ajili ya wachovu hawakukosea. Inakuwaje hawa wauza vitunguu na ndimu wajikite kwenye kaya yetu hadi kuweza kupata fursa ya kukusanya shehena kubwa kama hii bila kula na wakubwa? Je kwanini kago hii bab kubwa imekamatwa baada ya kuwepo kwa tishio la kumng’aoa waziri mhusika? Je ni ajali tu ya kimatukio au msuko wa matukio?
Haya ya wachina na kufanya umachinga au wahindi kukalia Msajili wa Majumba peke yao nawaachia wao walioyaruhusu bila kujua madhara yake. Ila siku moja watajuta baada ya kujikuta wakimtoa jini kwenye chupa wasijue jinsi ya kumrejesha.
Kutokana na uhalifu kulipa kwenye kaya hii iliyogeuzwa shamba la chizi, mlevi nina mpango kamambe wa kurejea ili nitengeze ukwasi nami niitwe mtu. Nitaingia na mipango ifuatayo:
Mosi, nitauza pembe za ndovu na faru bila kujali kuwa vizazi vijavyo vitaadhirika. Kama wazito wanahusika na biashara hii kama ilivyodaiwa hivi karibuni kuwa na wahishimiwa wamo, mie njjali ni nani?
Pili, nitauza unga hasa ikizingatiwa kuwa wauza unga wanaogopwa kama ukoma kayani kwetu. Rejea mkuu alivyogwaya kuwataja huku waziri wake Dokta Harry Mwakiwembe akijitia kimbelembele asijue anacheza na mtandao wa akina na nani na bab kubwa kiasi gani. Si ameishia kujichafua na kujishaua shaua baadaye akanywea. Nitaanzisha kiwanda cha kutengeneza madawa kama yule jambazi aitwaye Ramazani Madabidabida anayedaiwa kuuza mhidarati lakini haguswi kwa vile ni kada wa chama nonihino. Je tunao Madabidadabiba wangapi kayani wakijificha nyuma ya chama twawala?
Tatu, nitakwepa kodi kama wenye nazo wanavyofanya. Kama nitaagiza mikangafu ya magari toka Dubai, nitahakikisha napata msamaha wa kodi.
Nne, nitaunda genge la ujambazi ili kuvunja mabohari hasa ya sirikali na wenye nazo. Nikishazinyaka nahakikisha nafadhiri chama twawala ili kilinde madili yangu kama ilivyotokea kwa wale waliowahi kutuhumiwa kuwa majambazi wakubwa lakini wakubwa wenzao hasa wale wa kisiasa wakawakingia kifua upepo mbaya ukapita na walevi wakasahau na kuendelea kufanyiwa ujambazi,
Tano, nitaanzisha kundi la kufanya uharamia baharini ili kuingiza njuluku zaidi. Baada ya kuona wasomali wanavyopakuwa njuluku na kuangusha majumba ya bei mbaya kwenye ukanda wote wa Afrika Masharti sorry mashariki, nami lazima nitie timu majini nivue madola badala ya samaki. Inapendeza au siyo?
Sita, nitaficha pesa Uswizi na Ukamerunini aka Uingereza. Ili kufanya hivyo barabara, lazima nianzishe kampuni la kiwekezaji na kichukuaji na kuchanga pesa kama sina akili nzuri. Napendekeza kuanzisha kampuni ya simu. Hii ni baada ya kugundua kuwa biashara ya simu inalipa kuliko bangi. Unaleta mitambo chakavu na kufunga halafu unawalangua viwango vya kupiga simu walevi. Ikizidi ikipungua unaweka mitambo yenye uwezo wa kumkata mtu pesa hata kwa kubeep na kumwambia kuwa salio halitoshi kwa vile unamwibia kama ilivyo sasa ambapo simu za kaya yetu ni hovyo kuliko hata zile za enzi za Adam na Eva.
Saba, nitagombea udiwani ili kukamua pesa za mamlaka za miji. Hii ni baada ya kusoma repoti ya mkaguzi mkuu wa wizi wa pesa za serikali ambaye kila mwaka huripoti wizi wa matrilioni ya njuluku na hakuna anayekamatwa. Jamaa naambiwa wanakula mshiko mkubwa tu kiasi cha hata wahishimiwa kutaka wawakatie kitu kidogo na kikubwa kama ilivyotokea kwa yule jamaa yangu wa Pahi aitwaye Goodwell.
Nane, baadaye nitagombea ubunge ili kuzidi kuzichanga. Nikiwa na cheo cha mheshimiwa nitaweza kuingia kwenye makampuni ya kiwekezaji na kuyataka yanikatie kitu kidogo na kikubwa ili tusitunge sheria ya kuyakamua kodi. Pia hapa nitapata posho za usingizi, umbea, makalio, do nothing, uchakachuaji na hata uchangu.
           Tisa, kwa vile najua CcM itakufa, nitagombea urahisi ili niweze kupata mabilioni ya njuluku na kuyaweka kibindoni bila kutozwa kodi ukiachia mbali kusafiri kuliko Vasco da Gama yule jambazi wa kireno anayeenziwa utadhani alifanya la maana.
Kwa vile sijapata kanywaji na bangi, acha niwaageni niende kupata!
Salamu za pekee kwa wachina na washitiri wao watakaowaaachia huru kwenye mazingira ya utatanishi kama wale majambazi wa kipakstani. Watu wa mahakama ya kuachia wahalifu mpo?  Estaa Bulaya kawachoma je mwasemaje?
Chanzo: Nipashe Jumamosi Novemba, 10, 2013.

No comments: