The Chant of Savant

Tuesday 5 January 2016

Kijiwe chajadili mjengo wa Uhindini

          Kijiwe kilisherehekea mwaka mpya 2016 kwa furaha isiyo ya kawaida. Hii ni baada ya magazeti ya umbea kuripoti kuwa mahekalu ya mchunaji Gettie Rwakaterehe –hatimaye –yatapigwa chini kwa vile yalijengwa kinyume cha sheria.
            Kapende anainga na gazeti la Danganyika Daima. Mchuguliaji mpenda magazeti analidaka na kuanza kusoma kwa sauti ya juu. Anasoma, “Mahekalu ya mchunaji Rwakaterehe kupigwa chini.”
Kabla ya kuendelea Mijjinga anadakia, “Kwanini mahekalu ya mchunaji tu ambayo hayajawahi kuua mtu zaidi ya kuua sheria si ule mjengo dada wa mjengo uaji wa ugabacholini?” anamkata jicho Kanji ambaye naye anamkata Mijjinga jicho na kutabasamu.
            Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic, “Kwa spidi ya Daktari na mwanafunzi mwenzangu Joni Kanywaji –kama hatazimwa au kuishia kuwa nguvu ya soda –hata huo mjengo wako utapigwa chini tu. Ni suala la wakati. Nadhani ninachompenda na kumfahamu my friend Joni ni kwamba he is uncompromisable. Huo mjengo wako utavunjwa tu. Ni suala la muda. Na hapa suala si utavunja wa au la bali ni lini utapigwa chini.”
            Mgosi Machungi anaamua kula mic, “Timefuahi sana kuona kuwa hata wasioguswa sasa wanaguswa. Tinataka sasa tipange mikakati ya kumwabia daktai Kanywaji ashughuikie mashamba mengi yaiyopoa na vigogo wa seikali ziizopita. Hamkusikia juzi eti shamba la Dan Jonah liivamiwa? Haya mashamba nayo yanapaswa kuejeshwa kwa umma. Timechoka na wakubwa vibaka na mibaka. Hata Kiwia ya Nkapa nayo azima iejeshwe na ikiwezekana jamaa atupwe upango.”
            Mipawa aliyekuwa akimalizia kichungi cha sigara kali anaamua kula mic, “Hata mimi nimefurahi kuona hata wakubwa wanaguswa pabaya. Nilidhani zoezi la kubomoa lingeishia Uswazi nisijue litakwenda hadi Uzitoni. Nilidhani kuwa ubomoaji ni kwa ajili ya wanyonge wa mabondeni. Kumbe na wazito nao wanaonja joto ya jiwe siyo. Ama kweli hii ni kutenda haki. Naunga mkono wazo la kurejesha mashamba ya umma yaliyoporwa na vigogo wa sirikali zilizopita.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kukamua, “Tupanue wigo. Lazima na mashirika ya umma kama vile UDA yaliyoibiwa na wezi wenye ushirika na wakubwa yarejeshwe kwa umma. Lazima mikataba yote ya uwekezaji ambayo kimsingi ni ya uchukuaji ifanyiwe marekebisho mara moja ili tuache kugeuzwa shamba la chizi na wezi na washitiri wao wa hapa kayani.”
            Msomi anajerea, “Usemayo mheshimiwa Bwege ni kweli tupu. Nangojea kuona akina Symbion na Dowans bila kusahau Escrow, IpTL watakavyonyolewa bila maji. Lazima hapa tuheshimiane. Haiwezekani tukaendelea kuwa maskini wakati majizi machache yanatuchezea na kutanua wakati sisi tukitanuliwa na matatizo yatokanayo na umaskini.”
          Mpemba ambaye leo amechelewa kutia timu kijiweni anaamua naye kula mic, “Yakhe hakuna kitu kilionifurahisha kama kuona sasa zile zama za Nyerere zikirejea kupita kwa Makufuli. Kuna watu walishajiona wao miungu kiasi cha kudhani kuwa hawawezi kuguswa na sharia. Sasa twangojaona jinsi wauza bwimbwi watavoshughulikiwa sawa na mafisi na mafisadi tunaoona wakihaha sasa.”
            Mijjinga anakula mic tena, “Tena ami umenikumbusha. Juzi nilisikia waduwanzi wakisema eti katika ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria lazima sirikali ilinde nyumba za ibada. Kwani kazi ya sirikali ni kulinda nyumba za ibada au sheria? Kama kuna nyumba za ibada zilizojengwa kinyume cha sheria lazima zipigwe chini. Kwani nyumba zinapaswa kufuata sheria lakini siyo sheria kufuata nyumba za ibada.”
            Msomi anarejea, “Usemayo Mijjinga ni kweli. Hapa suala si nyumba za ibada au ada bali kufuata sheria. Nyumba za ibada zilizojengwa na wachunaji kama huyu Rwakatarehe si za ibada bali maduku ya kuwachuuzia na kuwaibia makapuku wetu wajinga.  Wakati mwingine unashindwa kutofautisha kati ya uganga wa kienyeji na uchunaji wa siku hizi. Hamkusikia waganganjaa wanavyowaibiwa wachovu kwa kutumia Quantum Magnetic Analyzer wakati ni utapeli mtupu? Hawa nao wanapaswa kubomolewa biashara zao kwa kuzifunga kwani wanaeneza magonjwa na kuwaibia wachovu. Tangu lini mganga wa kienyeji akatumia vifaa vya kisasa? Ukianza kutumia vifaa vya kisasa unakoma kuwa mganga wa kienyeji na kuwa mganga wa kisasa ambaye anapaswa asomee. Tulidhani wangeendelea kutumia matunguli. Lakini baada ya kugundua kuwa matunguli yameishastukiwa nao wanajifanya madaktari wakati ni matapeli wa kawaida. Hawa nao lazima wapigwe chini.”
            Sofia Lion aka Kanungaemba anakula mic, “Msomi usinikumbushe hawa wana hizaya wasio na huruma. Waliniibia pesa nyingi wakati mwanangu anaumwa nyumonia kiasi cha kutaka kusababisha nimpoteze kwenye ujinga na utapeli wao. Kila nikienda wanampima na hiyo kwantumu yao na kuniambia ana matatizo ya vitamin wakati tatizo ilikuwa nyumonia. Sina hamu nao. Hawa wanapaswa hata kupigwa risasi. Hawana tofauti na majambazi yanayobomoa majumba.”
            Kanji naye anaamua kula mic, “Hii ganga kienyeji naibia jinga jinga tu.” Kabla ya kuendela Sofia anamchomekea, “Kanji unadiriki kuniita mjinga!”
            Kanji anajibu huku akicheka, “Kwani jinga tusi? Jinga ni ile hapa jua kitu fulanifulani kama veve ilipopeleka toto kwa tapeli ya Quantum Magnetic Analyzer. Kwani natumia magnetic analyze veve iko madini? Hiyo ndiyo jinga ongelea mimi dada yangu.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la Rwakatarehe. Acha tumpongeze kwa kubomolewa mahekalu yake! Waligeuza kaya yetu shamba la bibi na wakome.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 6, 2016.

No comments: