Tuesday, 19 January 2016

Kijiwe chamtahadharisha Dk Kanywaji na Makapi


            Baada ya kushuhudia baadhi ya waadhirika waliokuwa na majivuno na kiburi enzi zao wakienda kwa rahis Dokta Kanywaji Makufuli kuhiji, kupiga soga, kupoza hasira na wengine kusaka kibarua, Kijiwe kimeamua kutoa tahadhari kwake.
            Mgosi Machungi kama kawa yake anaamua kulianzisha kwa maaamiko. 
Anakula mic, “Wagosi muiona akina Njaa Kaya, Ben Makapi aka Big Ben wakienda ikuu kutaka kumuhaibia ais wetu kiboko ya wavivu, wezi na mafisadi huku wakitaka eti awape kazi wamhaibie? Sijui wenzangu mliitakaitafakai hii vipi. Hebu tip you anaisis.”
            Kapende anakamua mic, “Unaongelea hawa gendaeka waliovuruga wakavuliwa nguo na nguvu ya ajabu ya Dokta Kanywaji kiasi cha kutaka kujifanya wanamkubali na kumheshimu ili wawe karibu naye wapenyeze fitina zao asiendelee kuwazidi ujiko siyo? Kama unaongelea hawa wala usiwe na wasi wasi. Dk Kanywaji amekaa nao na anawafahamu sana na fitina zao ukiachia mbali wivu wa kike na uvivu wa kufikiri.”
            “Hebu tuwe serious jamani. Hivi Ben na uzee na uzito ule anaweza kufanya kazi gani ya maana kama siyo kutafuta ulaji? Je anayo rekodi ya kufanya kazi nzuri au anataka kumharibia mwenzake baada ya kuona anaanza kufichua madhambi yao?” anazoza Mijjinga huku akiweka tai yake vizuri.
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutua, “Mimi sishangai. Unadhani Mungu akitaka kumuumbua au kumuadhibu mjivuni anafanya nini zaidi ya kumpa ujasiri wa kujivua nguo? Huyu Big Ben Tunituni Makapi ana lipi jipya wakati ndiye alitubinafsisha na kutunyakulia Kiwila yetu? Kimsingi wanachofanya hawa gendaeka ni kuendelea kujivua nguo na kutaka kupunguza aibu inayowapata baada ya Dk mwenzangu kuwaonyesha namna ya kutumia kichwa badala ya makalio.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kukatua mic, “Ama kweli wahenga walinena kuwa nyani haoni ninihini lake! Sikutegemea mijitu hasa hii miwili Tunituni Big Ben na Njaa Kaya kama wangekwenda kujivua nguo zaidi. Kwanza, si heshima kwa jitu kama Njaa Kaya ambalo ndani ya miezi miwili lililokaa nje ya ulaji limeishajipeleka kukuu mara mbili kana kwamba kuna kitu lilisahau.”
            Mzee Maneno anakula mic, “Kumbe nyie hamjui! Taarifa alizonipa mtoto wa dadangu anayefanya kazi Uhasama wa Taifa ni kwamba kuna mafisadi ambao ni washirika wa jamaa wamemsonga na kutaka aende kurekebisha mambo vinginevyo wanasema kama watabanwa mbavu na Dk Kanywaji watamwaga mtama kwenye kuku wengi ili na munene aliyeshirikana nao aumbuke ikiwezekana kushughulikiwa.” Kutokana na unyeti wa inshu yenyewe, wanakijiwe wanaangaliana kama kushuku kama kuna ukweli au la kwenye habari hii.
            Mipawa anakwanyua mic, “Mimi sishangai kusikia haya. Jamaa alivyoruhusu gendaeka na mafisadi wenzake wainajisi kaya, lolote lawezekana. Pia mjue lisemwalo lipo. Kama halipo basi laja. Hata nami nimesukuti kutaka kujua mantiki ya safari za mara kwa mara za jamaa ikuu kama hakuna namna.  Jamaa kwa alivyokuwa hamnazo, huenda kuna mazabe alitenda ambayo asipofunika kombe mwanaharamu akapita anaweza kujikuta lupango siku si nyingi.
            Mchunguliaji ambaye mara nyingine huwa hachangii anaamua kutia daruga. Anapoka mic, “Mna habari hawa jamaa waliopita wote kuanzia yule babu wa rukusa hakuna aliye salama hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo waliosimika mizizi ya ufisadi unaoisumbua kaya. Hivyo, kila mmoja kivyake vyake lazima aende kwa Dokta lau kujikomba ikiwa ni mkakati wa ima kumtisha au kumfurahisha ili asiendelee kuwaua nguo hawa wajalaana watatu.”
            Kanji anakula mic, “Mimi taka tokea kama ile natokea Israel. Iko jua nini natokea Isreal? Ile waziri kuu zamani nafungwa gereza kwa kula rushwa.  Kama hapa yetu nayo nafungwa mimi iko raha sana na nakuna mimi.
            Mbwamwitu mpenda utani hamkawizi. Anampoka Kanji mic na kumchomekea, “Kanji tafadhari acha tusi veve. Eti Napata raha nakunwa na Israel ile napenda tembea usiku! Nakuna nini na wapi Kanji hebu fafanua dogo dugu yangu.”
            Kanji hajivungi. Anakula mic, “Mimi iko serious veve naleta tani. Kumbe haikosikiliza BBC English! Acha chezo na tani dugu yangu. Ile Ehud Ormet nafungwa yeye nakula rushwa zamani sana.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anabusu mic, “Kanji kaka yangu nakuelewa. Ila utofautishe Danganyika na Israel. Huenda anaweza kufungwa gendaeka hasa ikizingatiwa kuwa kaka Kanywaji anaonyesha si mtu wa mchezo.”
            Kapende anarejea, “Da Sofi nakuunga mkono hasa baada ya kuzaliwa mara ya pili na kuachana ushabiki na mapenzi kibubusa. Jamaa anaweza kuandika historia kuwa kiongozi wa kwanza wa kiafrika kufanya mambo kwa haki. Hakuna kilichoniacha hoi kama Big Ben kuomba kazi wakati alichofanya ni kutuuza kwa wachukuaji waliokuwa wakimkatia chake. Huyu Njaa Kaya alivyo sijui hata kama alikatiwa zaidi ya kuliwa mkenge tu.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si tukapokea simu toka kwa Dk Kanywaji akitaka twende ikulu kumshauri!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 19, 2016.

No comments: