Tuesday, 12 January 2016

Kijiwe chataka rais atumbue na mabusha


            Rais Joni Kanywaji Makufuli amejipa cheo cha mtumbua majipu. Wengi wamemkubali ingawa wapo wanaomlaani hasa wale wakazi a mabondeni. Wanalaumu kwanini watoe kura waishie kubomolewa mijengo yao.
            Leo mheshimiwa Bwege ndiye analianzisha. Baada ya kutua gazeti la Danganyika Daima mezani, analianzisha, “Mmeisoma hii ya mchunaji Rwakatarehe kughushi uhalali wa hekalu lake kuendelea kukaa kwenye eneo alilojenga kinyume cha sheria?”
            Mijjinga anamchomekea hata kabla ya kuendelea, “Hili hekalu litapigwa chini tu. Huyu mchunaji na mwanasheria wake uchwara wametumia mbinu za kitoto. Waliozoea kuchezea utawala wa Njaa Kaya waliokuwa wameuweka mifukono. Kwa hii ngoma iliyopo ikulu wamekwama.”
            Kabla ya kuendelea Msomi Mkatatamaa anakula mic, “Kwa hili nakubaliana nawe mheshimiwa Bwege. Kwanza walichofanya ni jinai ya kughushi. Hata kabla ya kujadili mantiki na kwanini walifanya hivyo, Rwakatarehe na wanasheria wake walipaswa kuwa ndani ili uchunguzi zaidi kufanyika. Inashangaza kwa kaya yenye utawala wa sheria –kwa mtu mwenye akili timamu kufanya vitu kama hivi. Ajabu eti gendaeka mwenyewe alipewa PhD ya heshima. Kwa heshima ipi wakati ni tapeli wa kawaida?”
  “Msomi unashangaa huyu mchunaji kufanya aliyofanya na kupewa digrii ya heshima ya juu! Mbona wapo wengi kama yeye wanajiita madaktari wakati hata sekondari hakumaliza?, anajibu Mipawa huku akikamua kahawa yake.
            Kapende aliyekuwa ndiyo anaweka kisimu chake vizuri mezani anakula mic, “Mie nadhani huku kutumbua majipu anakofanya rahis hakujaniridhisha. Bila kutumbua mabusha kama yale ya Escrow, UdA, BoT na mengine mengi sitakubaliana naye. Lazima rais ayatumbue majipu na mabusha sambamba.”
            Mgosi anaamua kuchomekea, “Hapa Kapende umenena. Tinataka kuona mabusha yote yaiyoingia mikataba feki nayo yakitumbuiwa. Tinataka kuona vinaa wa hujuma wakisakwa na kutumbuiwa. Huwezi kutumbua majipu na mapunye ukaacha mabusha kama yae yaiyosababisha mgao wa umeme kwa kuazamisha kuuza majeneeta yao. Lazima rahis aambiwe kuwa atumbue na mabusha.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe naye anaamua kukamua, “Nakubaliana nawe Mgosi. Kutumbua majipu na mapunye tu na kuacha mabusha ni kufuga ugonjwa. Lazima rais atumbue. Pia nasi tutumbuane bila kuoneana aibu.”
            “Mimi nitakutumbua wewe da Sofi kama mchezo wenyewe ndiyo huu,” Mbwamwitu anamchomekea da Sofia.
            Msomi anarejea, “Kweli mnaomtaka rais atumbue mabusha mna pwenti hapa. Hamkuona juzi baadhi ya mabusha yakienda ikuu eti kumpongeza na kutaka ayape kazi kana kwamba hajastaafu? Hivi jamaa aliyejitwalia mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwila siyo busha? Je jamaa yetu wa Loliyondo, Kagoda na EPA siyo mabusha? Kama Dokta Kanywaji amepania kweli kusafisha kaya na kuondoa ugonjwa, lazima atumbue haya mabusha makubwa makubwa.”
            Kabla ya kuendelea, Kanji anakula mic, “Mimi chuki busha kuliko jipu. Nini jipu mtu naweza ficha? Kila mtu ona busha kubakuba napita mbele ya nyumbani yake. Kama rais haiko ona busha mimi tapelekea yeye orodha.”
            Mijjinga anapoka mic, “Orodha ya nini Kanji wakati Dokta Kanywaji anayajua mabusha yote kwa vile amefanya kazi nayo? Tangu Njaa Kaya alipoatamia ile orodha ya wauza bwimbwi mafisadi na majambazi, siamini tena katika kuwapa wakubwa orodha. Wao wana vyombo vya usalama vinavyolipwa mabilioni ya njuluku. Wavitumie hivyo hivyo kuyabaini na kuyatumbua majipu na mabusha.”
            Mzee Maneno anatia guu, “Hapa Mijjinga umenikuna. Bila kutumbua mabusha tutakuwa tunapaka rangi upepo. Hakuna mabusha yanayonisumbua kama yale yaliyojaa Banki kuu. Hivi rahis ajui kuwa ile banki imejaa watoto wa mabusha? Je rahis hajui kuwa hata haya majipu anayonasa TRA, Bandari na kwingineko yameajiriwa kutokana na kudhaminiwa au kupelekwa na mabusha? Je tuna wafanyabiashara wangapi tena wanaoitwa mashuhuri ambao ni wakwepa kodi kwa vile wamekiteka chama twawala kwa kukichangia njuluku wanayoibia kaya yetu?”
            Kabla ya mzee Maneno kuendelea Mpemba anakula mic, “Yakhe unosema hakika kweli tupu. Tuna wafanyibiashara wengi matapeli wanaoibia kaya kwa kujifanya wanatoa huduma za maendeleo. Hivi kweli hii migodi ya dhahabu inayoiba mabilioni na kujenga vijishule na vijizahanati viwili vitatu si mabusha? Je haya makampuni ya promosheni za kila uchao hasa yale ya simu si mabusha? Twataka yote yatumbuliwe kwani yajulikana ati.”
            Mipawa anarejea, “Hata Chama cha Maulaji (CcM) nacho ni busha. Kwani ndicho kilichoruhusu wezi wakifadhili kana kwamba haina uwezo wa kutafuta vyanzo vyake vya fedha chenyewe. Kwani Dokta Kanywaji hajui kuwa wafadhili wengi wa CcM ni wauza bwimbwi, wakwepa kodi, walanguzi, wafanya magendo, mafisadi na hata majambazi! Kama hajui aje hapa kijiweni tumtajie majina wazi wazi bila kificho kwani tunakula na kulala nao.”
            Wakati kijiwe kinanoga si likapita shumbwengu la mchunaji Rwakatarehe. Acha tulitoa mkuku. Bahati yake tungempata tungemfanyia kitu mbaya ili liwe somo kwa wengine.
Chanzo: Tanzania Daima January 13, 2016.

No comments: