Friday, 8 January 2016

Mlevi aja na Quantum Corruption Detection Theory


                  Baada ya matapeli wanaocheza na uhai wa walevi kuja na kinachoitwa Quantum Magnetic Analyzer ili kuwaaminisha kuwa nao ni wataalamu tena wanaokwenda na sayansi na teknolojia, Mlevi nimeingiza kitu inaitwa Quantum Corruption Detection Theory (QCDT) itakayomsaidia rais Dk Kanywaji Magufuli kupambana na mafisi na mafisadi.  Hii dhana ni ubunifu wa kisomi wa mlevi wala haitoki China wala Korea hata Ugabacholini. Chini ya dhana hii ni rahisi wadanganyika kuona tofauti yangu na matapeli wenye roho mbaya na uchoyo wa fisi unaosababisha vifo na umaskini kwa walevi, mlevi analenga kuwakomboa walevi wenzake kutoka kwenya makucha na uroho wa mashetani watu hawa. QCDT tofauti na Quantum Magnetic Analyzer, haitoi jibu ndani ya muda mfupi wala hairuhusu matapeli kuitumia kwa vile inataka mhusika awe amebukua si nchezo.
            Tofauti nyingine ni kwamba Mlevi haji na kifaa chochote bali wazo au nadharia ambayo –kama itafanyiwa kazi vizuri –italeta mapinduzi ya hali ya juu ukiachia mbali kutoa haki kwa walioikosa kwa miongo mingi hasa baada ya kuachia ngazi mzee Mchonga. Hivyo, nadharia hii ya kimapinduzi hailengi kumtapeli wala kumnyonya yeyote bali kumkomboa kila mlevi hata wale waroho na mafisi wanaowaibia kwa sasa wasijue wanajiibia hata wao wenyewewe. Sasa baada ya serikali mpya ya Dk Kanywaji kuja juu na kutaka kurejesha kaya kwenye mstari, lazima tumpe tafu ili kuharakisha maendeleo ya kaya na walevi wetu.
            Chini ya dhana ya QCDT si lazima uibe ndipo uwe tajiri na si lazima ukwepe kodi ndiyo upate utajiri. Lazima ufanye kazi kwa juhudi na maarifa ndipo upate ufanisi. Hapa kazi tu na asiyefanya kazi asile. Dhana ya QDCT inasema wazi kuwa kama umma utafanya kazi kwa kujituma na kutenda haki kwa kila mtu kaya nzima itaendelea kwani hakuna atakayekuwa anamnyonya mwenzake na hivyo utajiri utatiririka toka lisirikalini hadi kwa walevi. Hapa lazima pande zote zitimize wajibu wake. Walevi wachape kazi na kulipa kodi na kufanya manunuzi na lisirikali likusanye kodi na kuwekeza kwa walevi. Chini ya dhana ndogo ya QCDT iitwayo Yin Yang interconnectivity (YYI) wawili hawa yaani lisirikali na walevi hutugemeana na kufanya kazi kwa kushirikiana kuheshimiana na kulindana ilmradi wote watendeane haki kwa mujibu wa makubaliano ambayo huwekwa kwenye kitabu kinachoitwa Katiba.
            Chini ya dhana ya kisomi ya QCDT serikali inapaswa kutumia mbinu chokonozi na fumuzi ya kuwapa fomu wale wote inaowashuku kuwa nyuma ya ufisadi ili wajieleze na kuorodhesha utajiri wao na namna walivyoupata bila kusahau kuonyesha wamefanya hivyo kwa muda gani na kwa shughuli gani halali na haramu. Hapa lazima serikali iwasisitize kusema ukweli. Ili kubaini upungufu, unapokuwa na watuhumiwa kama hawa, unawaita sehemu na kuwahoji bila kuwa na nyaraka halafu unawaruhusu waandike maelezo kwa mikono yao wakitumia ushahidi wowote ili baadaye upambanishwe na yale waliyosema kwenye mahojiano ya awali. Hii ni njia ya kisayansi ya kumfanya muongo abainike kutokana na kutoa maelezo yanayogongana.
            Baada ya hapo dhana ya QCDT inapendekeza kuwachunguza watuhumiwa baada ya kuwahoji na kupokea maelezo yao ya maandishi na ya mahojiano.  Baada ya hapo unakwenda kwenye  taasisi  na makampuni ya simu na mawasiliano na kupata taarifa za simu zao ili kuangalia kama kuna walichoficha bila kusahau kuwahoji, watu wa karibu nao,  majirani zao hasa maadui zao.
            Ili kuopata taarifa sahihi zoezi la kuwahoji lazima lifanyike si mara moja wala mbili kwenye issue hiyo hiyo moja.  Kitaalamu ni kwamba lazima watafanya makosa na kujikanganya. Pia katika mahojiano na fomu za kujieleza hakikisha watuhumiwa wanaorodhesha matumizi yao miaka mitano.
            Wengine unaweza hata kuangalia saizi ya vitambi vyao, mitaa wanayoishi, kampani zao hata safari zao.  Wengine unaweza kuchunguza ngoma wanazochukua ujue zinatokea mikoa gani na zinawakwangua kiasi gani kuzitunza au kuzihudumia. Ukikuta mduwanzi anazo na ana ngoma toka karibu na ile milima ya akina Shimbo… we koma! Ujue kuna kitu hapo si bure hasa mdingi mwenyewe anapokuwa ana manzi kali ikilinganishwa na shepu yake. Hayo tuyaache japo meseji sent.
Chanzo: Nipashe, Januari 8, 2016.

No comments: