How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 21 May 2009

Busanda ilipogeuka sanda ya makada



BWANA we, Busanda ni kuzomea kwa kwenda mbele. Pati ya zomea zomea ilianza na Pio Mchekwa, Jo Malisera (si maneno na bila shaka) na walifuatia vimbelembele wengine. Hakuna kitu kilinifurahisha kama yule mama niliyezoea kumhusudu Annae Kilanga kuzomewa na kilanga chake sambamba na yule waziri tapeli kibaraka wa Tunituni Ben Makapi, Bill Ngereja na Joji Mkwichika.

Mambo yalizidi kunoga pale alipoingia Apeche Alolo ajiitaye Bwana Mapesa. Huyu aliufyata kama jibwa lililokwapua mafuta. Hakujua watu wanamjua. Tangu ulipofichuliwa utapeli wake na hekalu lake kuwekwa rehani ameishiwa hadi sera!

Mie nilipiga kambi maeneo ya Butundwe, Chikobe, Chigunga, Kabuguzo, Chankorogo,, Chibingo, Katoro, Nyamigota, na Nyakagomba na kwingineko.

Nikiri. Nilitenda kosa kubwa kuhusudu kimama fisadi. Huwezi kuolewa na fisadi usiwe fisadi. Huwezi kuwa mwanachama wa chama fisadi usiwe fisadi. Kweli walisema Nonihino ni Chama Cha Mafisadi. Nimeamini.

Ngoma ilinoga pale wale Mbwa mwitu akina Tambo Hizo na Salimu M7ha waliojipendekeza kwenda kueneza umbea wasijue umma unawajua walivyo vyangudoa wa kisiasa ambao mlo wao hutegemea fitina na salata. Mara nilisikia, “tunawajuaga nyie ku….nina zenu.” Matusi yalitembea kweli. Mengine siwezi kuyaandika hapa .

Mijitu mingine hovyo kabisa. Yaani inadhani wadanganyika na walevi bado wanaishi kwenye miaka ya ujima ambapo iliwajaza kila uongo? Miaka mitano sasa inaisha. Hakuna cha maana kilichofanyika zaidi ya kuongeza jitihada za kuvunja mabenki na mashirika yetu. Mnadhani hawajui? Badala ya kuwaneemesha watu mmewaneemesha mapapa mnaowatumia kudhulumu nafsi za waja wa Mungu! Aiwee! Oneni japo aibu na mkubali hamna sera wala lolote bali wizi mtupu. Wizi wizi wizi mtupu!

Wambieni miaka yote hii mmefanya nini na siyo kutoa ahadi uchwara zisizoingia hata kwenye akili ya kuku wala mbuzi. Hawa ni watu si samaki ambaye huwekewa kijinyama kwenye ndoana akapoteza maisha yake. Wala hawa si panya kama nyinyi mhongwao upuuzi kuuza roho na miili ya ndugu zenu.

Mwongo uliopita mlijipitisha pitisha mkawaahidi safari ya Kanani. Badala yake mmewakabidhi kwenya midomo ya mapapa! Wanajua sana . Na sasa eleweni. Wameamua kusema ‘sasa basi yatosha’. Imetosha jamani.

Huwa siachi kucheka nikifikiri kichapo mtakachopata mwakani kwenye kipute chenyewe. Halo halo mtajijeijei! Mtambe mna dola nyie?

Mijitu inajulikana ilivyonufaika na ujambazi wa EPA eti inakwenda Busanda kudanganya italeta maendeleo na maisha bora kwa wote. Inajulikana ilivyo mijizi ya kutupwa ukiachia mbali uongo. Eti inakuja na rongo rongo za ‘tuchague muhula huu tutabadilika’. Komeni na mkomae. Mna bahati mmezomewa hamkupondwa mimawe. Ila kaa mkijua mwakani tutatoana roho.

Watu wa Busanda si majnuni kama mnavyokosea kuwadhania. Wanajua mliiba nyumba zao. Wanajua mliiba Kiwira yao . Wanajua mlikopa mabilioni na hamlipi. Wanajua mlivyo mibaka wa kunuka. Wamechoka na siasa za upanya na ufisi. Wanataka maendeleo na heshima na siyo kugeuzwa zana za mapapa kuneemekea.

Pia eleweni. Wanajua mlivyo na mishahada ya kughushi. Ajabu eti walimpeleka na Chitaahira kuimarisha kampeni wasijue wana Busanda wanamjua alivyo kihiyo wa kutupwa. Hata mngempeleka Njaa Kaya asingefua dafu. Watu wememchoka hakuna mfano. Jitu linaishia kuzurura likitumia pesa yao wao wakisote eti walipende. Thubutu yako! Wanjua fika msivyowapenda ingawa mnajitia kuwapenda. Wanajua mnawaongopea na msemayo hayatoki moyoni bali kwenye matumbo yenu yasiyoshiba kama shimo la choo.Wanawajua nyinyi ni karata tatu. Utapeli utapeli utapeli mtupu! Wanajua mmewauza kwa mafisadi tena papa. Bahati mbaya, kwa uroho na upofu wenu, nanyi mmejiuza tena kwa bei ya kutupa na aibu ya ten percent.

Baada ya Tarime kuilima chini CCM, nani angedhani Busanda ingegeuka sana ya makada na urongowao? Hayawi hayawi! Sasa yamekuwa! Watu wemeishazomewa hakuna mfano. Wanaficha aibu zao kwenye vitisho na rongo rongo za magazetini. Ukweli unabakia pale pale umesimama kidume-wameumbuka na wamekwisha.

Hii inanikumbusha wakati wa ujuhani ambapo jamaa walikuwa hawaguswi. Sasa si kutoguswa tu bali hata mawe hutembea na sauti za kuzomea husikika wazi wazi bila kuchelea kitu. Kweli kila kitu na zama zake.

Harakati za zomea zomea zitaifanya KISHIPA au MSHIPA (Kikwekwe+Shaini+ Pindua) au (Mirisho+Shaini+Pindua) kujua mbivu na mbovu. Watu wameamka na wamechetuka hakuna mfano wala msalie Mtume.

Wamestukia usanii ngonjera na nyimbo zenu. Kazi kwa Kishipa. Mijitu hii kweli laanifu. Jitu linasimama mchana kweupe bila hata chembe ya aibu eti linakana kuwa ujambazi wa EPA hakufanyika! Baya zaidi, tena likenua linawageuza watu majuha lisijue wanajua kuwa lenyewe ndilo juha la majuha na marhuni wa marhuni. Wizi wa EPA ulifanyika na walioutenda ni wakubwa piga ua.

Huwezi kuwatia madole watu wa Busanda ambao miaka nenda miaka rudi wamekuwa wakishuhudia midege ya kukodisha ikitua na kuondoka na madini yao . Kama vile haitoshi, wamekuwa wakishuhudia mabehewa kwa makumi yakiiba dhahabu yao kwa kisingizio cha kupima mchanga nje.

Hakuna mtu alinifurahisha kutokana na alivyokuwa akiubuka na kujivua nguo kama kibaraka wa Tunitunim Ngereja alipojitia kurap wimbo wa jamaa wa “ndiyo mzee”.

Watu wameishachoka na ngonjera na nyimbo zenu. Wanataka sera. Wamechoka na sera za kulindana na kujuana na kulipana fadhila jasho lao. Wamechoka kugeuzwa shamba la bibi na mapimbi.

Busara ya leo; kiburi alikwezwa akapanda kwenye mgongo wa farasi. Alijisahau akafanya kiburi chake na farasi akamshusha kwa mateke akaishia kumlaumu farasi wakati kiburi ndiye chanzo cha yote haya!

Yaliyojiri Busanda ni mwanzo tu wa yatakayojiri mwakani kaya nzima. Waliozoea vya kunyonga kweli vya kuchinja wataweza? Leteni taarifa ya utekelezaji wenu badala ya rongo rongo. Watu wamekomaa. Hawataki utani wala utoto. Hawataki wala kuvumilia urongo na fitina. Hapa akina Tambo Hizo walie na ofisi za kufinyangiwa na Joe Makamba.

Kila la heri kwa mashujaa wa Busanda. Tuendelee kuzomea hadi kieleweke.
Chanzo; Tanzania Daima Mei 20, 2009.

No comments: