Tuesday, 26 May 2009

Kifo cha rais Roh Moo-hyun na somo la ufisadiTAIFA la Korea ya Kusini lilighubikwa na vilio, ghadhabu, lawama na mishangaa. Ni kutokana na kujiua kwa rais wao wa zamani Roh Moo-Hyun (62) baada ya kushindwa kuvumilia tuhuma na aibu ya ufisadi anaodaiwa kuufanya alipokuwa madarakani.

Ingawa kujiua kunaweza kuchukuliwa kama ukatili, Roh alikuwa mwanaume na nusu. Aliripotiwa kuwa alijitupa kwenye bonde karibu na milima ya nyumbani kwake. Na kifo chake kilisababishwa na majeraha makubwa kichwani.

Roh anakuwa rais wa kwanza katika muongo huu kujiua. Kujiua ni kubaya. Lakini marehemu rais Roh amehakikishia dunia; alikuwa na moyo mkubwa. Angewezaje kuishi kwa aibu na ngoa ya uchafu kama fisi? Hakika hili ni suto kwa mbweha,mbwa na fisi wetu waliojazana katika bara la Afrika wakiiba na kudhulumu mchana kutwa huku umma ukiteketea. Amejisuta na kujihukumu baada ya kukiri kuwa alichofanya si sawa.

Mwezi uliopita , Roh aliomba msamaha kutokana madai kuwa familia yake ilipokea rushwa ya dola milioni sita. Kiasi hiki kikilinganishwa na wizi unaofanyika Afrika ni sawa na punje tu. Ajabu pamoja na ujambazi huu, hakuna anayekiri wala kuomba msamaha hata kujinyonga kama Roh!

Dola milioni sita ni punje ni pesa kidogo kwa wezi wetu ambazo zinaweza kutapanywa na wake au watoto zao kwa siku moja bila kujutia wala kuona aibu! Nani amesahau jinsi rais wa zamani wa Zambia , Fredrick Chiluba alivyotumia dola milioni moja kwenye duka moja nchini Uswizi kwa siku kununua upuuzi ilhali wazambia wakifa kwa magonjwa yanayotibika?

Kwa roho, kutenda ufisadi ni kuwatwisha mzigo watu wasio na hatia. Ni kosa lisilosameheka wala kuhitaji msaada zaidi ya kujinyonga hata kunyongwa ikibidi. Kama angekuwa barakara kama wetu basi angeweza kukana au kutafuta ulinzi wa wakubwa hata kutumikia kifungo. Kwake heshima yake ilikuwa bora kuliko pesa na ukwasi. Kwake kifo kilikuwa bora kuliko maisha ya kukana na aibu. Bahati mbaya nguruwe na mbweha wetu hawana moyo wa namna hii.

Sipati picha jinsi Roh alivyokuwa akiugulia na kuteseka rohoni. Je angekuwa rais wa Tanzania wizi wa EPA, Richmond , TICTS, ANBEN, Deep Green Finance na mwingine ungemsukuma ajiue kifo cha namna gani?

Hata hivyo Roh hakufa kimya kimya. Aliacha ujumbe. Aliandika: “Siwezi kuhimili mateso ya maisha ambayo huko tuendako yangekuwa mzigo kwa wengine. Siwezi kufanya chochote. Kwa sababu nimedhoofu. Siwezi kusoma vitabu wala kuandika. Misisikitike. Je maisha na kifo si sehemu ya maishaa? Msimlaumu yeyote. Ni majaliwa. Tafadhali nichemeni. Na tafadhali wekeni mnara mdogo karibu na nyumbani. Nilifikiri juu ya hili kwa muda mrefu.”

Wakati wezi wa kiafrika huwaza wanawake na madili, Roh aliwazia vitabu na kuandika. Aligundua kuwa kuishi bila kuandika na kusoma ni bure. Wetu huwa hawaandiki wala kusema isipokuwa kuwazia mali na kusema uongo. Nyoyo na bongo zao zimetawaliwa na dhuluma na mali matanuzi na upuuzi mwingine. Na hii ndiyo maana hatuna vitabu vilivyoandikwa na watawala wa kizazi hiki kwa sasa. Hawana cha kuandika wala kutueleza zaidi ya uongo na ufisadi. Ni wavivu wa kufikiri kwa kijimbe alichojipiga Ben Mkapa zama zake kabla ya mambo kubadilika.

Roh aliona makosa yake. Hakutaka kuruka kimanga wala kutafuta sababu ya kuficha sura yake zaidi ya kujihukumu kifo. Wala hakupenda kuwalaumu wengine kama wetu walivyo. Wala hakufikiria kujificha kwenye kinga za kwenye katiba za uongo. Kwa Roh, ufisadi unapotendwa na wakubwa tena walioaminiwa madaraka, adhabu yake ni kifo. Ingawa tunalaani kujiua, kifo cha Roh ni somo na mfano na aina ya pekee ya kutubu ambavyo tunapaswa kujifunza kama tutataka kufikia ukamilifu wa maisha yenye kicho.

"Shutuma kuhusiana na wanafamilia yake zilivujishwa kwa vyombo vya habari kila uchao.” Rais wa zamani Kim Dae Jung aliyemrithi marehemu alikaririwa akisema. Hili ni onyo kuwa pamoja na kuwa madarakani, bado watu wanajua mambo yako na wanaweza kumwaga mtama.

Aliongeza. “Yawezekana hakuweza kuhimili shinikizo na ghafiliko zaidi. Natoa pole kwa familia yake.”

Habari za kifo cha Roh zilipotangazwa, nilikumbuka. Je wezi wetu wa Kiwira walizichukuliaje. Nadhani. Huenda kwa upumbavu na ufisi wao walimcheka kwa kujiua kwa vijisenti kiduchu hivi!

Rafiki yangu alinisimulia hadithi ya mawaziri wawili wa maendeleo toka Ahaha na nchi ya Malaya . Nchi hizi mbili zilipewa pesa na benki ya dunia kwa ajili ya maendeleo. Baada ya kitambo walikutana.

Maongezi yalikuwa: “Umepata wapi pesa ya kujenga hekalu hili waziri? Waziri wa Malaya alimuuliza waziri wa Ahaha.

Waziri alijibu: “Hukumbuki pesa tuliyopewa na benki ya dunia?

Mwenzie aliingilia: “Ina maana hukujenga barabara na badala yake ukajenga hekalu lako! Mimi nilijenga bara bara nyingi sana na naishi kwenye kijibanda kidogo tu.”

Waziri wa Ahaha alijisemea moyoni: “Jamaa fala kweli!”

Kwa ufupi ni kwamba mpumbavu wa Ahaha alimcheka shujaa wa Malaya asijue alikuwa akijicheka!

Tukirejea kwa Roh, aliyeacha urathi unaong’ara, nina kila sababu kumkumbuka shujaa huyu hata kama amekufa kwenye mazingira mabaya.

Nenda salama shujaa Roh kwa kuacha urathi wa mfano. Umekufa kwa ajili ya ukweli kama alivyosema Plato. “Tunastahili kuufia ukweli.”
Chanzo: Gazeti la KULIKONI Mei 26, 2009.

No comments: