Thursday, 21 May 2009

Kuna kila sababu upinzani kuchukua Busanda

SIKU njema huonekana asubuhi. Na mwanzo wa ngoma lele. Kwa mchunguzi makini anayeangalia yaliyokwishajir kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo jimbo la Busanda mkoani Mwanza, atakubaliana nami:CCM ina kila sababu ya kulipoteza kama ilivyotokea Tarime ukiachia mbali mizengwe ya Mbeya.

Tumesikia zomea zomea za vigogo wa CCM, Makamu mwenyekiti Pius Msekwa na Makamu mwenyekiti wa zamani John Malecela-Kibajaj, mkewe Anne Kilango na waziri William Ngeleja. Hata wanafunzi wameingia! Rejea kupigwa bakora sita sita kwa wanafunzi wa shule ya Butundwe!

Hii inafanana na kisa cha Mfalme mzee mpumbavu na kijana maskini jasiri. Ingawa upinzani wetu una upungufu wa kutoungana kutokana na ama tamaa au kurubuniwa na CCM, dalili ni kwamba CCM inaanza kupoteza ushawishi wake.

CCM imekuwa ikitumia kampeni chafu na za kizamani za fitina kuwa wapinzani hawana cha kuonyesha kana kwamba wamewahi kutawala na kushindwa kama CCM!

CCM imekuwa ikitumia mtaji wa zama za Julius Nyerere bila kujua kuwa umma umeishabaini uoza na uovu wake na jinsi ilivyoufuja na kumwaibia Nyerere aliyekufa akiwasikitikia wananchi wake.

Je, sasa, CCM ina nini cha kujivunia au kuwaonyesha wananchi? EPA, ANBEN, Tanpower, Meremeta, Richmond , Dowan, IPTL na matumizi mabaya ya fedha za umma?

CCM imekuwa ikitumia mauaji ya kimbari ya Rwanda na machafuko ya kikabila ya Burundi bila kujua haina tofauti na nchi hizi! Hivi karibuni jina la Tanzania limechafuka tokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, vikongwe, polisi kwa watu wasio na hatia-rejea mauaji ya hivi karibuni huko Musoma na wizi wa fedha za umma bila kusahau ufisadi unaokingiwa kifua na CCM. Rejea karipio la mawaziri wawili wa CCM kwa Reginald Mengi alipowataja mafisadi papa.

Kimsingi, CCM imechakaa na kuchanganyikiwa kiasi cha kupoteza mvuto na mwelekeo. Haina cha maana kuwaonyesha watanzania. Imekuwa ikiwachukulia watanzania kama mataahira vipofu na wapumbavu wasioweza kuona uovu wake. Sasa mambo yamebadilika. Umma umeanza kujitambua. Umeanza kuzomea,kuponda mawe hata kusema enough is enough-imetosha.

Watanzania hasa wale wa vijijini wanajua kuwa makada wa CCM na watawala wake waliiba pesa yao toka kwenye Fuko la Madeni ya nje-EPA. Wanajua kuwa CCM chini ya Benjamin Mkapa iliiba nyumba zao na kuingia mikataba mibovu ya uwekezaji hasa kwenye sekta za madini, nishati na utalii. Watanzania wanajua kuwa viongozi wa CCM wamewakumbatia matajiri kiasi cha kukibinafsisha hata chama kilichoanzishwa na wanyonge kujikomboa. Wanajua CCM ni mzigo mzito kwao. Wanajua kila kitu.

Kutokana na uhuru wa vyombo vya habari ambao umepatikana baada ya mapambano makali na utawala wa CCM, wananchi wanapata taarifa zote muhumi. Wanajua kinachoendelea Dar es salaam na Dodoma.

Wanajua kuwa kama si takrima, CCM isingeshinda kwa kishindo mwaka 2005. Wanajua jinsi walivyotapeliwa kwa kuahidiwa maisha bora kwa kila mtanzania chini ya usanii ulioitwa Safari ya Kanani ambayo imegeuka safari ya kuzimu. Wanajua vyote hivi.

Kinachoonyesha wazi jinsi CCM ilivyoishiwa na itakavyopoteza Busanda ni ile hali ya Busanda kuwa kwenye eneo athirika la mikataba mibovu ya uwekezaji. Waulize wananchi wa Busanda kama wanafaidika na dhahabu yao.

Waulize mantiki ya kupitia Nairobi Kenya wakitokea Tanzania kwenda Tanzania . Waulize kama wabunge wao wanawatendea haki. Hivi karibuni baada ya CCM kuzidiwa eti iliwaita wabunge wa mkoa wa Mwanza kuja kuongeza nguvu wasijue hawana lolote la kuwambiwa wananchi. Hivi mbunge kama Samuel Chitalilo aliyesamehewa makosa ya kughushi na kuudanganya umma anaweza kuongeza nguvu gani? Hivi mbunge kama Anthony Dialo aliyetuhumiwa kumhujumu aliyepaswa kuwa mgombea halali wa CCM anweza kuongeza nguvu gani? Hivi mbunge kama William Ngeleja anayeendelea kuficha madhambi ya Mkapa kwa kushindwa kumtaja kuwa ndiye mmiliki haramu wa machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira kama alivyoliahidi Bunge na wananchi mara nne asifanye hivyo anaweza kuongeza nguvu gani zaidi ya kuwa kichekesho?

Sasa umefika wakati wa wananchi wa mashambani kuwaonyesha watawala kuwa wao si wapumbavu wala punda wa kubebeshwa kila upuuzi. Kufanya hivyo ni kuinyima kura CCM.

Ingawa CCM imekuwa ikipayuka na kuongopa kuwa imeleta amani Tanzania , kuna haja ya kuiuliza kama kweli kuna amani ya kweli Tanzania ambapo tofauti ya kipato kati ya watawala na wageni wao matajiri inazidi kuwa sawa na mbingu na ardhi.

Hivi kweli wananchi watatenda dhambi isiyo sameheka wairejeshe CCM amabayo imeshindwa kusimamia raslimali zao na kutumia vibaya pesa kidogo ipatikanayo kwa taabu. Rejea ripoti ya hivi karibuni ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambapo matrilioni ya shilingi yameliwa chini ya uangalizi wa CCM?

Watu wa Busanda, iulize CCM walipo akina Richmond , Kagoda na majambazi wengine walioshirikiana na hao hao wanaowaaminisha kuwa wameleta amani na maendeleo wakati ukweli wameleta maafa na kurudi nyuma.

Waulize yalipo maisha bora kwa kila mtanzania iwapo watu wa kanda ya Ziwa wanaishi Tanganyika ya kabla ya uhuru. Waulize hao wabunge wao ni kwanini wanajilipa mishahara mikubwa huku umma wa walimu, madaktari, wafagia barabara na wengine wakilipwa mishahara ya matusi ukiachia mbali wakulima kulanguliwa na kukopwa mazao yao.

Waulize maana ya maisha bora kwa wote. Waonyeshe kuwa mnajua kuwa wote kwao ni wao si wote watanzania.

Kuitia adabu CCM kwa ulaghai, ufisadi na uzembe wake, watu wa Busanda hakikisha hamuipi kura ili ile kama mlivyobainisha kwa kuanza kuwazomea. Msiishie kuzomea. Hakikisha mnazomea hadi kwenye sanduku la kura ili siku ya kutangaza matokeo mzomee zaidi.

Tuhitimishe kwa kuwatakia kila la heri wapiga kura na wananchi wa Busanda ambao kwa hali ilivyo, kama wenzenu wa Tarime, mmepata nafasi ya kuwa waanzilishi wa ukombozi halisi wa mtanzania toka kwenye chama nyemelezi na nyang’au kinachowachukulia kama hamna akili.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 20, 2009.

No comments: