How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 27 May 2009

Mpayukaji atinga White House kwa mlango wa nyuma

MSOMAJI,

Naomba usome taarifa hii kwa sauti ya chini. Kwanza , sitaki kunguru na wabaya wangu wanizomee na kuniona limbukeni, mshamba na mzururaji.

Kwa taarifa yako Mzee Mzima nilitinga kwenye White House ya Barack Obama. Si utani. Jumba kubwa na kazuri! Kwa yale maua niliyoona, kama ingekuwa Bongolala, vibaka wangetembelea kila siku!

Huwezi kuamini. Nilitamani Bro Obama aniruhusu lau nilale kwenye Oval Office. Maana hilo zuria ni kama peponi!

Mtake mstike, amini msiamini nilitinga kwenye jumba jeupe japo kwa kupitia japo mlango wa nyuma na usiku. Hapakuwa na haja kutangaza kwa sababu Obama alikuwa anasumbuliwa na mafua. Hivyo, tulikutana kwa muda mfupi sana . Aliniomba msamaha sana kuwa angetaka tuongee kwa siku mbili. Kwa kujua uzito wa urahisi nilimkubalia nikaendelea kuzurura kwenye mitaa mingine ya majuu.

Pia naomba usome halafu uchane. Bi. Mkubwa akijua nilivyojinoma, kwanza, atachukia. Na pili siku nyingine nikitaka kwenda kule ataniganda bure na kuzidisha kichunvi tokana na uzuri na ulimpyoto wa vimwana vya White House.

Najua wengi wataniita mzushi kwa kutoniona kwenye runinga ya Teddy Turner ya CNN au FOX, ABC AFP, BBC, na runinga nyingine kubwa. Amini usiamini wakati napiga soga na Obama, runinga nyingi hazikuweza kurusha habari hewani kutokana na kuwa na tishio la shambulizi la kigaidi.

Pamoja na kufaidi maraha White House, nilifaidi uhondo wa mibarabara mipana kama uwanja wa mpira. Nimeamini Marekani ni wezi. Wamewezaje kujenga mibarabara mikubwa hivi bila kuiba? We fikiri daraja la San Francisco ni pana kuliko state house yangu! Hawa jamaa wanakufuru! Pia nilikula kwenye hoteli ya Beverly Hills Hilton, Los Angeles baada ya kuvinjari Hollywood na kuchonga na akina Eddie Murphy.

Unajua ilikuwaje? Niligundua kumbe Obama hana adabu! Nilimbomu misaada akanitolea nje na kunizodoa eti kwanza nikamate jamaa zangu mnaowaita mafisi ahadi!

Jamaa kanaonekana hakana raha tokana na kuongoza taifa kubwa. Ukikaangalia vizuri, kameanza kukonda na kuzeeka tokana na madai yasiyokwisha ya Wamarekani. Kumbe kuongoza ni hatari siyo kama kutawala ambako ni kula salama!

Nilimpa ushauri afanye kama sie Kijiweni. Twala hatuongozi. Kukwepa kuitwa watuwala watu, twaitwa watawala. Upo? Fanya iwe siri. Tusiwastue walevi wakaharibika na kuanza kudai mambo mengi kiasi cha kutukondesha na kutuzeesha.

Huwezi kuamini! Nilionana na Michelle. Mama anajua kupika na kuandaa chai sina mfano! Aliniandalia chai na pizza na turkey. Kwa wasiojua turkey, huyu ni bata bukini anayeandaliwa kwa wageni maarufu na maalumu kama mimi.

Sikuvutiwa na Michelle. Pamoja na kuwa mke wa mwenye nchi kubwa, hajisikii wala hali nchi kama kwetu .Hana hata mkufu wa dhahabu kama Bi. Mkubwa wangu wa bosi wa Maulaji ya Wake wa Wakubwa (MAWAWA)!

Nilimdodosa ni kwanini hana NGO ya kutafutia pesa ya kutanua baada ya mumwe kustaafu. Mama kweli fyatu! Unajua alinijibuje? Eti hana haja ya kuwa na NGO. Maana Wamarekani ni vichaa wanaweza kumfunga yeye na mumewe baada ya kuachia ngazi! Kumbe Wamarekani fyatu na hawana akili siyo!

Ila kamama kamesoma! Ajabu hakajifichi nyuma ya Barack kuishi! Kanapayuka utadhani kana ukoo na Mpayukaji! Kalisema NGO ni ufisadi. Kenyewe kana mission na vision wala hakategemei kudandia mgongoni mwa Barack. Inaonekana kana mpango kama ule wa Hill Bill Clinton. Kanataka kagombee urahisi baada ya mzee kumaliza ngwe zake.

Tuachane na Michelle. Acha niwamegee nilivyofanya matanuzi ya kufa mtu.

Nilianzia San Francisco . Niliweka kambi yangu kwenye mitaa ya Anza baada ya kukosa vyumba Masonic street . Nilikwenda kushanga shangaa daraja na mambo mengine kabla ya kutimka zangu Washington.

isamehe. Siwezi kueleza matanuzi yote. Wenye wivu wanaweza jinyonga. Hivyo kiduchu hiki kinatosha. Habari mbaya, safari hii sikuandamana na Bi. Mkubwa. Alikuwa Mkuranga akiandaa kura za kula mwakani. Hayo tuyaache.

Pia niliamua kutia timu kwa Obama kuepuka upuuzi wa kuzomewa kuwa nami nimo kwenye ulaji wanaoita ufisadi wa njuluku za Kijiwe. Na hii ndiyo maana hamkuniona Busanda kwenye kampeni za kampani ya kuzomea zomea. Sikupenda kuzomewa kama Joni na Pius. Huwa nina hasira naweza kuwavunja watu mbavu kama Makomandoo uchwara wa Nambari one.

Ingawa walevi wananiona kama limbukeni mshamba na mtaradadi, hawajui kiranja wa kwanza wa walevi kukutana na Obama ni big deal. Nimeweka historia. Naye alifurahi sana na kunipongeza kwa kuwa mlevi wa kwanza kukutana naye.

Pamoja na kwamba alikataa kunikatia misaada, alisema: anawaomba walevi wanichague mwakani. Na amesema wakichagua, atamwaga misaada kama hana akili nzuri ili nasi tuweze kujenga bara bara ya pale Kijiweni iwe kama zile nilizoona San Francisco , Washington na New York . Pia aliisifa ndege yangu ya Air Force Zero. Alisema ni ndege ya hadhi hata kama wale wasiojua mambo ya ulaji wanaikandia na kusema ina mafua. Hata kama ina mafua bado ni ndege na mtake mistake itazidi kuwaumiza nyoyo zenu.

Safari yangu Marekani imezaa matunda sana . Baada ya kunichagua mwakani, kwanza, nitaanza safari ya kuwapeleka walevi wote Kanani (Marekani). Pili, walevi wote wataruhusiwa kutumia dolari badala ya madafu. Nitaanzisha viwanda vya kupika pizza kwa kumkaribisha MacDonald afungue maduka yake kila kijiji.

Tuliongelea nishati endelevu au renewable energy. Kuanzia mwakani, serikali ya Kijiwe itakuwa haitumii mikangafu. Tutaanza kuagiza Dodge, GMC, Chevy na madudu mengine ili tufanane na Wamarekani.

Kitu kingine ingawa hatukukijadili, Bi Mkubwa itabidi atafutiwe shahada hata kama ya kununua ya sheria ili awe kama Michelle. Isitoshe itasaidia kuwatisha watakaoendelea kustukia ulaji wake yaani NGO. Pia nikimaliza muda wangu, nitamshauri agombee urahisi ili aweze kuendeleza mema yote nitakayofanya.

Yote katika yote, zile ahadi nilizotoa kwa walevi bado ziko pale pale. Nitaanza kuzitekeleza mwakani baada ya kuchaguliwa tena.

Hakika safari yangu Marekani ilifana. Pia nilipata nafasi tena ya kutumbuizwa na BoyzII Men.

Here we go, to the end of the road, you belong to me I belong to you ni ulaaaaaajiiiiii.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 27, 2009.

No comments: