Tuesday, 19 May 2009

Karibu tena Bongolala mh.Chavda


Nakaribisha habari njema kuwa shujaa VG Chavda, hatimaye, amerejea Bongolala hasa kwenye jiji la Bandari Salama baada ya kufukuzwa kimakosa. Na hii ndiyo sababu iliyonisukumu kumwandikia waraka huu wa kumkaribisha pamoja na wenzake.

Awali kabisa mheshimiwa unahakikishiwa usalama na mafanikio. Kuna dili nyingi zinangoja watu shapu kama wewe. Kwa ubongo wako wenye thamani ya mamilioni, hutakereka wala kukaa bila dili hasa kwenye ukwasi huu na pepo ya mabwege.

Karibu tena kwenye nchi ya wapenda amani na watu ambapo mashujaa watawala wanajua jinsi ya kutumia madaraka yao kwenye dili. Kwa mtu mwenye rangi nyingi kama wewe, nchi hii inalipa. Kwani unamwendea bwege, sorry shujaa mmoja na kumpa urongo sorry tena, mipango yako. Mambo yanajipa. Wajua? Kiumbe kama huyu hawezi kukwepa chambo na uroho na upofu wote huu. Ana kasha la moyo na ubongo mtupu sorry akili nyingi.

Kwa mufilis kiakili namna hii, sorry tajiri, watawala walafu, oh samahani wasio walafu na vipofu, hufanya mambo kuwa rahisi hata ukitaka kuwachukua wake zao. Wako tayari kuwanadi watu wao hata kwa mbwa, fisi hata mbwa mwitu bila kujua kuwa huko tuendako watawararua hata wao.

Vinyamkera wetu wa kiuchumi walikutumia kabla ya kustaafu. Na sasa tazama wewe ni shujaa aliyewaepusha na aibu uliye tayari kutumia na hawa wapya. Kwanini usirudi na kutanua na kutengeneza dili nyingine?

Hivyo kaka, si vibaya kukukaribisha tena kuja kujiunga na wenzio wasioguswa na mashaufu wa Kagoda, Meremeta, Mwananchi Gold, Deep Green Finance, Richmond na wengine wengi kama wewe.

Hivyo kaka, kwa unyenyekevu, karibu kwenye nchi ya mataahira, sorry mashujaa.

Kitu kingine, wala usitie shaka wala kuwa na wasi wasi. Hakuna kinyamkera wa kukugusa. We si mwanasiasa wala mpinzani. Tutakuhakikishia ulinzi milele. Sisi ni wapenda watu hasa wangeni.

Nichukue fursa hii kuwaonya wapenda ghasia. Atakayemgusa Chavda ambaye kimsingi ni mgeni wetu maalumu, tutamshukia kama simba jike au mfalme Joji Mkuchi alikiwapatiliza maadui zake. Kwa ufupi tutamuonyesha kilichowazuia ndege kukojoa na ng’ombe kutaga mayai.

Hapa Bwana Reginald Mengi tuelewane. Ukimuita Chavda papa tutakupakazia u nyangumi.

Kaka Chavda, amini maneno yangu. Washairi wetu, waandishi, viongozi, majaji, wana sheria na wapigania haki wote watasimama nyumba yako na kukutetea.

Kwa vile wengi kama wewe wanapaaza sauti zao bungeni, basi ningekushauri kwa unyenyekevu ugombee ubunge ili utuwakilishe na kutufundisha jinsi ya kutengeneza pesa hasa kipindi hiki cha ukapa. Unaweza kurejea India na kuleta wengine wengi kama wewe ili kufufua uchumi wetu. Amini kaka. Vitabu vyote vya historia ya kipande hiki vitakuandika kwa wino wa dhahabu na kwa kicho kikubwa.

Nafahamu. Wewe ni jasiri. Kama uchumi wetu unaweza kuneemesha vicheche, mafisi, kupe hata vinyama vya mwitu vya usiku, utashindwa kukufaa wewe? Kama wabongo watafunua vinywa vyao, tutawashukia kwa ukali na ukatili unaopaswa.

Wakosoaji vichaa wanasema: hapa ni rahisi kwa kila mseng… ashakum! Anaweza kuukata na kuwa mtu maarufu kirahisi hasa akilala kitanda kimoja na majambazi wenye madaraka. Jua fika. Hata watuite vichaa na mafisadi, atakayekugusa, tutakufa na shingo yake. Ndiyo. Ukitaka kumjua mwenye mbwa, mtupie mawe. Tutakulinda milele. Narudia kwa msisitizo.

Ingaw vipofu wanakuona kama mtu mbaya, wanakosea sana . Kutoka kwenye omba omba mwenye akili wanayekuita tapeli mwenye ubongo wa thamani kwa kutengeneza pesa kiharifu, hakika wezi wetu wa ngazi za juu watakuhitaji sana .

Hebu niibie siri. Je ni wewe uliyewafundisha jamaa zetu dili kama zile za ununuzi wa rada feki na dege la kulanguliwa la rais? Nauliza hili kwa sababu bila ubongo kama wako sakliligo hili lisingewezekana. Je na vipi ile michoro ya EPA, NSSF na Richmond nayo ni vitu vyako?

Pia niambie uliwezaje kuponyoka kuitwa fisadi papa na Mengi? Je unaweza kueleza ulivyokuwa muhimu kwa utawala wa awamu ya pili hasa kwa rafiki yako waziri mkuu JSM?

Je we ndiyo ulimfunza fisadi papa mmoja mlalamishi rafiki wa waziri mkuu wa zamani ENL aliyetimuliwa kwa uchafu wa Richmond ?

Kwa muhtasari, unakaribishwa kwa mikono miwili kwenye pepo ya mabwege sorry nchi ya mashujaa. Tutakulinda hadi tone na senti yetu vya mwisho. Tafadhali, karibu mheshimiwa V.G Chavda.

Tafadhali mpigieni makofi ndugu msomaji.
Chanzo: Gazeti la Kulikoni Mei 19, 2009.

No comments: