Thursday, 7 May 2009

Mfumo wetu ni wa kifisadi na kinyonyajiSAFU hii huwa haiachi kujiuliza. Inawezekanaje rais wa nchi kuwa mwenyekiti wa chama tawala lakini mkuu wa mkoa akashindwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho hicho tawala?

Kwa nini na wakuu wa wilaya wasiwe ni hao hao wenyeviti wa wilaya badala ya wanajeshi wastaafu na wengine ambao rais hutujazia maofisini wakifilisi hazina yetu itokanavyo na kodi na kuomba omba?

Bado kuna makatibu wa CCM wa wilaya na mikoa ambayo ukiuliza mishahara yao itokako hutapata jibu la maana zaidi ya longo longo tu.

Kwa nini mawaziri wasitokane na ajira huru badala ya mafungamano ya kisiasa kama ilivyo sasa ambapo hali hii inasababisha kujuana na kulindana ukiachia mbali uzembe kazini?

Mawaziri wetu karibu wote ni makada wa chama ambao hutumia pesa ya serikali kufanya kazi za chama ambazo ni kuhujumu vyama vingine huku wakikibeba chama chao.

Hii ni kinyume na utawala bora na wa sheria. Ni mgongano mkubwa kimadaraka ukiachia mbali kumtwisha mzigo mwananchi maskini.

Hiki ni chanzo kizuri cha ufisadi na umaskini nchini. Kwa nini kwa mfano, rais aweze kuvaa kofia mbili ilhali wengine hawawezi?

Ukiangalia hata utitiri wa wilaya na wizara na viti maalumu tulivyo navyo unagundua jinsi gani mfumo wetu ni wa kinyonyaji na kifisadi ukiachia mbali kuwa wa kikale na kikoloni.

Watawala wanawanyonya wananchi maskini licha ya kulipwa marupurupu mengine kwa kazi zisizokuwapo au kama zipo hazina umuhimu kwa wananchi. wamepewa hata mamlaka ya kumegeana na kutengenezeana wilaya na majimbo ya uchaguzi!

Je, mfumo wetu unakubalika kwa wanyonywaji au wanyonyaji tu? Kwa nini, kwa mfano, rais asilipe kodi ya pango lakini daktari, mwalimu, karani, rubani na wengine wafanye hivyo?

Nani analitumikia taifa kuliko mwingine? Kwa nini aandamane na mkewe kila aendapo lakini watumishi wengine wa umma wasifanye hivyo?

Kwa nini mbunge awe na mshahara na marupurupu mengi na makubwa kuliko daktari, mwalimu, na watumishi wengine wa umma na pia asilipie kodi kitita hiki?

Ukipata majibu sahihi kwa maswali haya, utajua ni kwa nini nchi yetu itaendelea kuwa maskini na kichaka cha mafisadi kila namna.

Kwa nini polisi na askari wengine wasafiri bure huku wanafunzi wasio na ajira wala posho ya nauli walipe? Nchi zilizoendelea, hujali sana watoto na wazee (senior citizens).

Kwetu, kutokana na mfumo na utawala wa kinyonyaji tunawajali askari kuliko hata vichanga na wajawazito! Aibu. Na huu ni ufisadi.

Kwa nini iwe suala la hiari kwa rais wabunge na mawaziri kutangaza mali zao ilhali wakiwataka wafanyakazi wa chini yao wawajibike hasa kulipa kodi wakati wao hatujui kama wanalipa kodi au la?

Kwa nini tupate pesa tena kwa mabilioni ya kununulia mashangingi ya wabunge, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya bila kusahau wakuu wa wizara ilhali hatuna pesa ya kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu?

Kwa nini tuwe na mashangingi mengi ilhali hatuna barabara za kutosha wala madawa hospitalini na vifaa vya kutosha mashuleni? Kwa nini tufikie mahali hata tuishiwe akiba ya chakula ilhali tuna watawala wanaoishi kikwasi kama wafalme wa Nchi za Kiarabu?

Kwa nini wabunge watutungie sheria za viwango vya mishahara lakini sisi tusiwapangie mishahara na marupurupu yao? Haya ni maswali wanafalsafa waanzilishi kama Plato, Socrates, Democritus, Heraclites na wengine walijiuliza na kuwauliza watawala.

Haya ndiyo maswali yaliyosababisha magwiji wa falsafa kuchukiwa hata kuuawa. Hata hivyo hawakuacha kuuliza wala kumgwaya mtu zaidi ya nafsi zao.

Je, ni nani leo yuko radhi kufa kwa ajili ya kuuliza maswali haya adhimu ya ukombozi iwapo wachache kama Dk Slaa waliojaribu wanaitwa wezi wa nyaraka za serikali? Lazima tusemezane na kusemana.

Tumerithi mfumo mchafu wa kikoloni ambapo tuna msururu wa utawala unaotunyonya na kuzidi kutudidimiza. Ukiangalia ngazi ya taifa ni balaa tupu. Nenda kwenye ngazi za mikoa na wilaya nako kadhalika ni balaa.

Kuna maafisa wengi wasio na kazi isipokuwa kulipwa posho na mishahara bila sababu. Mfano leo utakuta kuna maafisa wa kilimo kuanzia mikoa hadi kata. Hawa wanafanya kazi gani iwapo kilimo tuliishakizika na kupapatikia uwekezaji, uombaomba na umachinga?

Rais wetu anafanana sana na gavana wa kikoloni. Anakula bila kulipa. Anaishi kama Malkia wa Uingereza akiwa juu ya sheria. Anateua na kufukuza atakaye bila kutoa maelezo. Namna hii hatuwezi kusema tumejikomboa bali kujikomoa.

Hata ukiangalia kwenye ofisi zetu ambazo zimegeuka vijiwe vya kupanga jinsi ya kuliibia taifa utakuta kuna wafanyakazi wengi wasio na sababu ya kuwapo.

Tunaendesha nchi kama daladala. Maana kwenye daladala unamwajiri dereva naye anaajiri kondakta ambaye naye humwajiri mpiga debe ambaye naye huwaajiri wapiga debe wa kituoni.

Mfumo huu mchafu umetambaa kwenye mishipa yote ya taifa. Hata kwenye mabaa kuna wapiga debe. Nenda kwenye kila kitu kuna wapiga debe. Hiki ndicho chanzo cha ufisadi kimfumo.

Hamkusikia wapiga debe wa rada waliokamua taifa mabilioni ya shilingi wakiliuzia rada feki. Kwenye dege bovu la rais kadhalika bila kugusia uwekezaji wa kijambazi unaotuhangaisha. Mbona tunageuka taifa la wapiga debe!

Kuna haja ya kuuasi na kuutokomeza mfumo huu mfu na kifisadi kama tunataka kusonga mbele. Njia moja wapo ni kuuliza kwa nini? Baada ya hapo ni kutenda kwa njia ya kupigania mabadiliko ya katiba ili tuwa na katiba itokanayo na wananchi.

Vinginevyo tutaendelea kutawaliwa na mafisadi na mabwana zao. Sitaacha kuuliza kwa nini; na kwa nini; na kwa nini; na kwa nini!
Chanzo: Tanzania Daima Mei 6, 2009.

No comments: