JUZI nilihudhuria mkutano wa kampeni uliokuwa ukihutubiwa na bi mkubwa wa mkubwa. Jina leo silitaji atakayejitokeza kujihisi, atajiju. Japo wengi wamekuwa wakimshutumu kufanya kampeni kifamilia, mie sina ugomvi na hilo kama wataacha kutumia njuluku za Kijiwe chetu.
Hata wakitaka na mbwa na paka wao wawapigie kampeni ruksa. Ilmradi wasiguse njuluku zetu. Kwa vile nami ni mgombea na rais mtarajiwa, naamua kuwananga kwa kuninanga kuwa sina sera bali photocopy na wao ni orijino tena handsome orijino.
Hata mie ni handsome. Sema sina tabia ya kujisifia ujinga. Hayo tuyaache.
Kwenye kampeni za rais mama, nilishangaa kusikia upuuzi badala ya sera. Badala ya mtu awahamasishe walevi kwa kuwaambia atakachowafanyia, cha ziada zaidi ya kile alichokwisha wafanyia, anahanikiza upuuzi mwingine. Ni kero na machukizo hasa upuuzi huu unapotoka kwenye kinywa cha mtu anayeitwa mheshimiwa.
Basi bwana, mama mkubwa alitua kwa ndege yake kijijini kwetu na wasaidizi, walinzi yakiwamo hata yale majini wake, huku akilakiwa na viherehere wa mikoa na ngoma za kitamaduni.
Ukiona anavyotembea, kupungua mikono na kuongea, utaamini naye ni rais. Hapa bado hujaangalia utitiri wa mishangingi na mishankupe anayoandamana nayo.
Anahutubia kama rais na kulala hata Ikulu kama rais. Je, huyu si rais nyuma ya pazia? Mie nasema mapema. Si Bi mkubwa wangu wala kitegemezi changu watakaribia hata kiti changu achia mbali kutumia madaraka yangu kuwaibia walevi kijiweni. Hivyo lazima wote mnipe nifanye kweli na si kuambiwa mfanye kweli kitanda kwa kitanda. Kitanda kwa kitanda ni kueneza ukimwi na nyumba kwa nyumba ni kueneza ujambazi.
Nasikia wanasema zile ndege anazotumia Bi mkubwa, zinalipiwa na lisirikali hili kapa. Kama siyo ujambazi mbuzi, wanamlipia kama nani? Hata mkubwa hapaswi kulipiwa usawa huu. Maana ashamaliza ngwe yake. Nashangaa kumuona hata akiwapa ulaji waramba viatu wake usawa huu ambapo yeye si rahisi bali mgombezi!
Basi mama, bila chembe ya aibu, tuseme. Kutokana na kiherehere chake si alianza kumwaga matusi akidhani ni sera. Alipayuka. “Kuanzia sasa nawataka wanachama wetu wafanye kampeni nyumba kwa nyumba na kitanda kwa kitanda. Wafanye hivi bila kukoma.”
Umma wa mashabiki wake majuha ulimshangilia sana. Kwenye mti jirani, kunguru walimzomea na kuwashangaa walevi wanavyolishwa matusi na uchafu.
Kabla ya kuendelea sisi hatuna mbavu. “Wafanye bila kuchoka! Kitanda na kampeni wapi na wapi kama si kutaka kumalizana kwa ukimwi kutokana na kuhongana ngono?” Nilimsikia mkota mmoja akizoza.
Naye Mkota wa pili ambaye anaonekana anaunga mkono chakudema aliiingilia haraka. “Dokta alishasema hawa watu hawana sera zaidi ya uhuni. Lakini wadanganyika walio wengi hawataki kumwamini. Sasa mmesikia na kuona wenyewe,” alimalizia.
Siku hiyo niliandamana na Msomi Mkatatamaa. Yeye alichomekea hapo hapo. “Siku zote nimesema kuwa hawa watu licha ya kuwa na mawazo mgando, wamefilisika vichwani hamtaki kuniamini.
Hili jimama laonekana kulewa madaraka na kudhani hayana mwisho.” Alinigeukia na kuendelea. “Ngoja mzee Mpayukaji ashinde kiti tuwafungilie mbali hawa gendaeka.” Nami kwa kumwagiwa ujiko nilikenua kama Chekacheka utadhani nami ni kibopa wa kaya hii.
Tukiwa na kikao chetu ndani ya kikao, mama mkubwa aliendelea. “Nawahimiza kina mama msilale hadi kieleweke. Msichague wapinzani wana ahadi za uongo kama zetu.” Kabla ya kuendelea nilisikia mhuni mmoja aliyejichora rangi za chama cha mafisadi akisema. “ Toboa mama toboa lazima wafanye kweli na kieleweke.”
Mke wa mkubwa kusikia kasifiwa ujinga anapanua domo lake na kuongeza. “Hamjasikia kuwa mwanamke lazima awe ndoo kichwani na vidumu mikononi? Bila hiyo, hakuna raha.” Alimalizia mpuuzi huyu kujivua nguo. Kumbe anadhani wote wazaramizi? Kusum audhubillahi minaa shaitwan rajiim.
Mwingine alidakia: “Mnatukanwa na kutumiwa ajabu mnashangilia. Kweli nyinyi danganyika. Mama anaongopa huku. Baba kule. Mwana naye kadhalika wakitafuta uongozi nanyi mlivyo majuha mnazidi kuwashangilia badala ya kuwashushia mkong’oto kama aliokoswa koswa kiherehere wao kule kwa kina Kamwene.”
Tokana na uhuni aliokuwa akifanya ma mkubwa, nilipandwa hasira hadi umombo ukanitoka. Nilimgeukia Msomi na mgosi Machungi na kuzoza: “First off, I'm totally against impotent and incompetent politicos you see in power campaigning on public funds and resources.”
Msomi naye kuwaonyesha kuwa ni msomi na siyo wale vilaza wa kughushi alijibu. “Mzee you're dead right. These goons must be booted out the sooner.”. Mgosi Machungi yeye alisema: We wee make sure that the are not coming back mgosi. Kwai?” Baada ya kuona wachovu walio kuwa karibu nasi kuanza kunong'ona kuwa tunajifanya watasha tuliachana na ung'eng'e na kuondoka tukijadili hili na lile.
Mpake leo sijaelewa ni kwanini Chama Cha Mafisi kimeamua kufanya uhuni kikidhani ni sera na isiwe dharau kwa wanaoambiwa matusi haya!
Yaani mafiga matatu kama wale ndugu zangu wanaotumia matatu yaani kutoa chifu original (figa la kwanza) kutoa uchifu kwa chifu feki (figa la pili yaani daddy au mkuu) na kumalizia kugawa ‘uchifu’ kwa mtoto wa chifu feki (figa la tatu).
Tusipoangalia kuna siku kutakuwa na figa la nne yaani na mama kupewa uchifu maana wote ni walevi wa sifa na kutapeliana. Wanawatapeli walevi na walevi wanawatapeli wezi kwa kuwapa uchifu.
Siku Bi mkubwa wa mkubwa akitangazwa na akina Twa mbombo twa bakangale kuwa chifu nitacheka hadi ninyauke kama siyo kupagawa. Lakini hata hivyo hawana kosa. Kama mama amepata urahisi kutokana na mumewe kuwa rahisi atashindwa nini kupata uchifu?
Mwanzoni nilidhani mpuuzi ni bi mkubwa, kumbe na baba naye hovyo tu! Maana kila anapokwenda kuongopa kwa jina la kampeni utamsikia akihanikiza: “Tumefanya, tutafanya na tutaendelea kufanya zaidi.” Ukiuliza mmefanya nini zaidi ya ufisadi na ujambazi, utaambiwa wewe photocopy.
Heri photocopy isemayo ukweli kuliko orijino katika ufisadi. Yote hii ndugu zanguni ni uhuni, usanii, ubabaishaji na ukosefu wa sera. Ni aibu hata ukosefu wa busara. Nashauri mnichague mimi kwa vile nina sera madhubuti na adabu ya hali ya juu.
Mie nina sera si uhuni. Na isitoshe mie situmii midege ya mafisadi ambao baada ya kuniwezesha watataka wawanunue nyinyi na raslimali zenu. Nichagueni niwafunge mafisadi na kuwanyonga bila huruma. Sitegemei yule shehe mhuni ambaye natabiri atafia India hivi karibuni.
Kabla sijasahau, yule shehe wa Migomigo nasikia anatumiwa kutangaza mbinu za kutaka kuninyotoa roho. Ninyotoeni roho damu imwagike.
Du kunguru kaninyea. Wewe kunguru mwanga na mhuni kama shehe ubwabwa na bi mkubwa wa mkubwa. Khalas kweisine.
Chanzo: Tanzania Daima Septemba 6, 2010.
2 comments:
....Sophia Simba aliposema kuwa wanawake wa ccm wawanyime unyumba waume wao wanaoshabikia upinzani ulidhani masikhara?
Ndo aina ya viongozi tulokuwa nao na pengine tutakaokuwa nao ambao fikara zao zote ni kuanzia 'chini ya kitovu'!
Bwa Ng'wanambiti usemayo ni kweli watu wetu tunaowaita viongozi kwa makosa hawafikirii zaidi ya chini ya kitovu. Hebu angalia jinsi mgosi Makambale wa Machungi alivyorushiwa kimondo na Dokta SILAHA kuwa alitumliwa kwa kubaka alivyokula pini kana kwamba si yeye aliyepewa vipande vyake.
Post a Comment