Wengi Wanaojua madudu ya rais mstaafu
Benjamin Mkapa walishangaa mantiki ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpa jukumu la
kurejesha jimbo la Arumeru Mashariki baada ya kufariki kwa aliyekuwa mbunge
wake. Kwa wanaojua jinsi Mkapa alivyomwangusha kipenzi chao Baba wa taifa
mwalimu Julius Nyerere, walishangaa busara hii ya kumteua mtuhumiwa wa kufanya
biashara ikulu, kuridhia ubinafsishaji wenye kila shaka, kujitwalia mali ya
wananchi yaani mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira alioutwaa akiwa rais
akishirikiana na waziri mwandamizi, familia zao na hata wakwe wa Mkapa. Hata
hivyo habari zilizotufikia ni kwamba Mkapa amegwaya kwenda Arumeru Mashariki.
Hili halituzuii kuuliza maswali ambayo angepambana nayo kule.
Wenye kumbukumbu na busara walishangaa
kuteuliwa kushika usukani katika kampeni kwa mtu aliyewadhurumu wananchi benki
yao ya biashara (NBC) iliyokuwa ikiingiza faida kuliko ilivyoelezewa. walishagaa
mtu kama huyu aliyejenga msingi wa ufisadi na wizi wa wazi wazi unaoendelea kama
kuingia mkataba wa hatari wa IPTL kupewa jukumu kubwa kama hili. Je huu si
ushahidi kuwa CCM imeishiwa na kuparaganyika? Basi kwa niaba ya
Mkapa iulizeni CCM itampelekea ujumbe wake. Je kule kutangaza mali zake wakati
wa kuondoka madarakani kuliishia wapi? Muulize ni kwanini alibariki wizi wa pesa
za umma chini ya ujambazi wa EPA ambapo mabilioni ya shilingi za wananchi
yaliibiwa kugharimia uchaguzi wa aliyemfuatia ambaye naye, kama Mkapa, huwa
hataki kujibu tuhuma. Endeleeni kumuuliza. Ni kwanini aliruhusu mkewe kujipatia
utajiri wa haraka na haramu kupitia biashara ya NGO. Muulizeni ule uchumi wa
kisasa alioahidi kwanini uligeuka uchumi wa kisasi na kifisadi. Muulizeni
alikopata jeuri ya kujiuzia nyumba ya serikali na kuwapa marafiki zake nyumba
nyingine. Muulize hata hayo mabilioni ya kujengea hekalu Mkuzi Lushoto yalitoka
wapi?
Mngeweza kuendelea kumuuliza Mkapa
hata CCM ni kwanini aliamua kukikabidhi chama cha wanyonge kwa mafisadi huku
akiwaacha wakiwa yatima. Muulizeni ni kwanini ameendelea kunyamazia tuhuma zote
zinazomkabili yeye, familia yake na marafiki zake? Je ataendelea kuishi kwa
hisani ya Kikwete hadi lini? Kitu ambacho kiko wazi ni kwamba Mkapa hawezi
kupata jibu lenye kuingilia akilini hata la swali moja. Sana sana akifika
Arumeru Mashariki ataenda kupiga siasa za kukandiana na kujilisha pepo kuwa
wapinzani hawana kitu wakati asiye na kitu ni yeye na chama chake ambacho
kimeonyesha kuishiwa kulhali.
Kipindi hiki wananchi wa Arumeru
Mashariki msikubali majungu naporojo za kwenye majukwaa bali muwape mtihani hao
wanaotaka kuwawakilisha kuhakikisha wanaeleza na kuwahikikishia kuwa
hawatakwenda kuwakilisha matumbo yao na koo zao hasa wale wanaoendekeza siasa za
kurithishana kama ufalme.
Maswali mengine ya kumuuliza Mkapa ni
kwanini chama chake na serikali yake wameamua kwa makusudi kutumia raslimali za
umma kwa manufaa yao binafsi? Watu wa Arumeru Mashariki wanajua jinsi mbunga za
wanyama zilizowazunguka zinavyonufaisha wageni na wenye madaraka wachache huku
wanancni wakizidi kutopea kwenye umaskini wa kutengenezwa na waroho wachache
wanaokaa ikulu kufanya biashara ya kujitwalia mali za umma. Hawa ni wezi wa
kawaida hata kama wana madaraka. Hawa ni watu wa kuzomewa siyo kusikilizwa wala
kushangiliwa. Kufanya hivyo ni kujidhalilisha hasa wananchi watakaotapeliwa na
wezi wanaowajua fika. Je wananchi wa Arumeru Mashariki watajiruhusu kutumika
kama daraja na ngazi ya watu waongo wachache kupandia kwenda kwenye neema
itokanayo na kuwahujumu hao hao watakaopiga kura?
Kituko cha pili ni ubunge unaoanza
kuwa wa kurithishana ambapo anayepeperusha bendera ya CCM ni mtoto wa aliyekuwa
mbunge. Je tunaaza taratibu kujenga msingi wa siasa za kihindi? Hata hivyo,
tujiulize, nani msafi kwa sasa anayeweza kuheshimika kwa wananchi ndani ya CCM
baada ya wote kuchafuka au kuchafuana? Rejea kambi moja ya CCM hiyo hiyo
iliyomtangaza mteule wa CCM Arumeru Mashariki kuwa si mtanzania. Leo uraia wake
umepatikanaje haraka hivi?
Kama wananchi wa Arumeru Mashariki
wanataka ukombozi na hawako tayari kutumiwa na wezi wenye madaraka basi
wamuulize Mkapa swali moja kuu na la maana: ilikuwaje akajitwalia mali ya umma
wakati alikuwa akituahidi kujenga uchumi imara ulioishia kuwa
legelege?
Chanzo: Dira ya Mtanzania Machi, 2012
No comments:
Post a Comment