Monday, 5 March 2012

Tanzania itakuwa shamba la bibi hadi lini?

Hivi karibuni gazeti moja la kila siku wiki liliripoti kuwa kigogo mmoja wa dini mkoa mmoja kanda ya ziwa angefikishwa mahakamani kwa kosa la kuhujumu uchumi.

Kosa lake ni kwamba alikuwa akitumia dini yake kupata misamaha ya kodi ilhali alichokuwa akifanya hasa kwenye kununua saruji ni kuwasaidi wafanya biashara kukwepa kodi ya mamilioni kila mwezi. je huyu kweli ana dini au ni kafiri wa kawaida? Je ni wangapi wanatumia taasisi zao za kidini zilizochipuka kama uyoga kujitajirisha? Je hiki ndicho chanzo cha utajiri wa ghafla wa viongozi wengi wa madhehebu ya dini?

Nimekuwa nikilalamikia uholela na urahisi wa kusajili madhehebu ya kidini bila kusikilizwa. Nadhani Kwa tukio hili angalau tunaoshuku biashara hii ima ya misamaha hata unga ukiachia mbali kuiba sadaka na kutapeli wananchi tutaanza kusikilizwa kwa makini kama hakuna mkono wa serikali kwenye ushirika huu mtakakitu.

Pia kuna uwezekano kuna maafisa wa serikali wanaojua mchezo huu. Lakini kwa vile wananufaika nao hawataki hata kuishauri serikali kuweka vigezo vigumu kusajili madhehebu ya kidini ambayo siku hizi yamegeuka kama maduka ya kawaida.

Nchi yetu ina utaratibu wa hovyo kwenye mambo mengi kuliko nchi zote za Afrika Mashariki. Shilingi yetu iko chini kuliko sarafu zote kwenye eneo hili. Tunazidiwa na hata na Burundi na DRC pamoja na kukumbwa na misukosuko miaka nenda rudi! Angalia tulivyo na maduka mengi ya madawa tena mengi yakiuza madawa feki na yaliyo expire utadhani nchi yetu ni ya wagonjwa wa akili?

Tazama maduka ya mikorogo yalivyotapakaa huku tukiendelea kuhatarisha afya za watu wetu hasa akina mama. Tazama tulivyowekeza kweney glosari kuliko hata shule. Niliwahi kuliongelea hili kwa kulinganisha na Uganda ambako kuna shule nyingi wakati sisi tuna glosari na guest house za chap chap nyingi. Hili ni tatizo hata tunapodanganywa tuugane na nchi nyingine za Afrika mashariki ambazo hazina raslimali nyingi kama zetu na ardhi. Tatizo jingine ni kwamba hatuna hata mipango mizuri. Bado tunafanya unafiki wa kutangaza matangazo ya kuchochea ngono kwa kisingizio cha kupambana na ukimwi.

Turejee kwenye kuhujumu uchumi kwa kutumia majoho ya dini. Kwanini serikali haitaki kujiuliza ni kwanini madhehebu ya dini yameongezeka huku wanaojipachia uchungaji, ushehe, uaskofu, utume-bado upapa-ni wengi na hawafanyi kazi yoyote zaidi ya kuhuburi lakini bado ni matajiri wa kutupwa? Wasitudanganye kuwa pesa inapatikana toka kwa waumini maskini wanaolalamika kila siku. Lazima kuna njia nyingine nyuma ya pazia na huu ndio motisha wa kila mtu kupenda kufungua makanisa na misikiti. Imefikia mahali hata wageni wanakuja kufungua makanisa Tanzania kwa vile hakuna sheria ya kuwazuia wala kuwachunguza.

Mbona Yesu alipiga marufuku watu kukalia kupiga kelele badala ya kufanya kazi maana binadamu hawezi kuishi kwa neno pekee? Kwa kutilia mkazo mtume Paulo alisema asiyefanya kazi na asile. Ajabu hawa wetu wanakula hata kuwa matajiri bila kulazimishwa na sheria kutoa maelezo walivyopata utajiri wao! Mbona Sayyidina Omar bin Affan aliwazuia waislamu kupoteza muda mwingi kwenye ibada bila kufanya kazi miaka zaidi ya 1,000?

Tunao wezi wengi wanaowaibia watu wetu na kuwahadaa. Kwanini mhasibu au mfanya kazi wa serikali anapoiba ofisini kwake linakuwa kosa la jinai lakini kiongozi wa dini akiliibia kanisa au dhehebu lake haliwi kosa la jinai? Mwizi ni mwizi hata awe askofu au shehe au rais. Kinachokera ni pale serikali inapozidi kuwapumbaza watanzania kuwa ni nchi ya amani wakati ni nchi ya kuibiana. Hivi haya maelfu ya wetu wanaotapeliwa na majizi haya na kutumia nafasi zao kukwepa kodi yanaashiria amani?

Tusipofumbuka macho tutajikuta tuna makampuni yanayoonyesha kunawiri kuliko mengine si kwa sababu ya umahiri katika kufanya biashara bali umahiri katika kukwepa kodi. Kwanini taifa letu hasa viongozi wetu ni wagumu kujifunza? Wawekezaji wengi wamekuja wameiba na kuondoka huku tukizidi kukaribisha wengine kuja kuiba. Wako wapi wahindi waliokuwa ‘wamewekeza’ kwenye shirika la reli? Wako wapi majambazi wa Dowans walioendelea kutuzidi akili kwa kubadilisha majina ya biashara zao? Nenda kwenye mahoteli yetu mashuhuri. Kila baada ya miaka mitano yanabadilishwa majina ili kupewa muda mwingine wa kutuumiza. Angalia makampuni ya simu yanavyobadilisha majina mara leo so tell kesho mot el tel tel tel tel mpaka lini? kwanini msiseme ni stealtel?

Bado makampuni hayo hayo ya simu yanayolangua watu wetu ukiachia mbali kuwalisha huduma mbovu kuliko nchi nyingine za kiafrika. Imefikia mahali watu walioko nje kupiga simu kupitia nchi jirani kuepuka kulanguliwa. Hebu tutoe mfano mdogo. Ukipiga simu toka Kanada kuja Tanzania kwa Tanzania unachajiwa senti 25 za dola ya Kanada wakati Kenya wanakutoza senti 5. Hii maana yake ni kwamba kupiga simu Tanzania ni aghali mara tano kuliko Kenya. Je ni kwanini hali inakuwa hivi kana kwamba hakuna serikali? Hata ukipitishia Uganda hata Burundi bado ni nafuu kuliko kupiga moja kwa moja Tanzania. Hapa bado hujapambana na upuuzi kuwa namba unayopiga haipo mara huna salio la kutosha na ushenzi mwingine mwingi? Je huu ndiyo uwekezaji au uchukuaji? shame on you all!

Nikijumlisha yote hayo hapa juu huwa mara nyingi nafikia hitimisho kuwa nchi yetu imo mikononi mwa ima mataahira au watu wasiojua wanachofanya na kama wanajua basi watu wasiopenda nchi yetu. Imo mikononi mwa watu hatari ambao huko tuendako watasababisha vurugu na balaa kwa taifa. Maana hakuna kisicho kuwa na mwisho. Watu wetu hawawezi kuendelea kugeuzwa mbuzi wa shughuli au bidhaa kwa ajili ya wezi wachache kujitajirisha

Chanzo:Dira Machi, 2012

No comments: