Baada ya kutoka zangu London juzi
nilipitia Nairobi kuongea mawili matatu na wanakijiwe cha River Road na Ngala.
Sikukwa na mpango wa kusimama kidogo Nairobi. Ila nikiwa zangu London Mureithi
ambaye ni mwenyekiti wa Kijiwe kile alinitwangia simu akiomba nipitie Nairobi
lau nitoe ushauri.
Nilifaidi sana uzuri wa mji wa London.
Barabara zote zina lami, taa, zinapigwa deki usiambiwe. Nilipofika Heathrow
airport, sorry, International Airport nilitaka kuzimia nilipolinganisha na jiji
letu la uchafu na ufisadi liitwalo Chafusalama.
Sikuona mgambo wa site mamantilie wala
wazee wa mabao kwenye barabara za London. Kitu kimoja kilinistua sana-London
kaya inachomwa hadharani na hakuna anayejali! Nilipomuuliza mvuta kaya mmoja
akacheka na kusema kuwa kaya haina tatizo kwa taifa bali kwa mtu binafsi. Hivyo,
nami niligundua kuwa kumbe hapa kwetu heri turuhusu watu wajichomee kaya kuliko
kuruhusu ufisadi. Maana ufisadi unaumiza wengi. hata uchafu wa miji yetu ni
hatari kwa kila ajae na aishie kwenye miji yetu. Ni ushahidi wa uchafu wetu wa
kitabia.
Najua nikirejea kijiweni kwangu wengi
nitakaowasilimulia usafiw a London watanisuta na kuhoji kama naona hivvyo kwa
wenzangu nashindwa nini kutekeleza kwangu? Najua wengi wataniona kama juha na
mtalii asiyejifunza. Hata hivyo tuache utani. Tuna tatizo tena si dogo. Yaani
tunashindwa kujifunza hata mambo ya msingi kama usafi, mipangilio ya miji na
mambo madogo kama haya? Au nayo tunataka waje wafadhili watusaidie kama
walivyofanya kutuchimbia vyoo tukaishia kuvichafua?
Tukirejea kwenye kijiwe cha River Road
Nairoberry ni kwamba siku hizi kule umeibuka mchezo wa akina mama kuwashikisha
adabu waume zao. Ukichelewa kurudi unapatiwa. Wajua kupatiwa maana yake nini?
Kuadhibiwa. Ukishindwa kufanya shughuli za ndani hasa za night unapatiwa.
Ukitoroka kwa nyumba kwenda kula kwa hoteli, ukirudi unapatiana adhabu kama
kawaida. Ukinywa sana kanywaji na kushinda kumudu idara zote, unapatiana adabu.
Huwezi kuamini kuwa juzi nilikuwa
kwenye mahakama ya Kilimani kushuhudia mama mmoja akikabiliwa na kosa la kumpiga
mumewe hadi akazimia. Toka na vipigo vya hapa na pale vya mara kwa mara, walume
wa nchi ya Nyayo wameamua kuanzisha chama cha kulinda haki za walume. Kunogesha
stori ni kwamba kipindi nilichokuwa kule, walume wote walikuwa wamekubaliana
kugoma kula chakula nyumbani ili akina mama wapunguze morali wa Kikyuki.
Hakuna kitu kiliniua kama maongezi
haya kijiweni. Mara anakuja Wagacohi na kuamkua, “Kohani
atya?”
Njoroge na Wamauseto wanaitikia,
“Kutiri na kaolu.”
Wagacohi anaendelea, “Mnajuanga kuwa
Ithe wa Kinywa amepigwa na bibi yake hadi akepelekwa hosi?” Hosi maana yake ni
hospitali.
Anaendelea, “Nyina wa Kamuyu
ameniambia kuwa alipokwenda kunywa akaselewa kurudi akapatiana adhabu kali
sana.”
Gathuma anadandia, “Haki mimi bibi
yangu akipatiana adhabu na mimi nitaua yeye.” kabla ya kuendelea, Gitau
anachomekea, “Kama umeoanga Central hasa Nyeri jua unapigwanga tu. Vinginevyo
uwe umeoa kibeti cha Kikamba.” Wamuseto hana mbavu. anasema, “Haki, kwetu Matuu,
Mbooni na Woote bibi hapingangi bwana. Sisi wakamba bibi akipinga bwana
atalaaniwa aote devu. Kibeti ya Kikamba siyo Kama hii ya Kikuyu.” Anakunywa
kahawa yake na kutafuna mirungi kidogo na kuendelea, “Wajua siku moja mimi naona
bibi kule Ithekahuno akitwanga bwana hadi bwana anakufa kwa muda?”
Anamalizia, “Ukiona bibi anatwanga
wewe understad wewe ni nugu-nyani.”
Mzee Gate anachomekea, “Wacha mabo
yako wewe. Bibi akiamua twanga wewe anatwanga tu. Hukuona Luse alivyopiga watu
ya habari pale Nation na hakuna ameshitaki yeye? Hata Kebaki mwenyewe hasemangi
Luse akileta matata.”
“Kama munene kama Kebaki anapindwa
nani wewe ulete nyoko nyoko kwa bibi ya kisasa asitwange wewe?” Mara mzee Gate
ananigeukia. “Kama unataka bibi asipige wewe nenda kanunue bibi TZ. Huko
nasikianga wanasema tafadhali wacha kuselewa na kurudi usiku badala ya kupatiana
adhabu.”
Wamuseto anamuunga mkono mzee Gate,
“Nasikianga watz ni wapoa sana. Tena ni wabeautiful.”Mie sina
mbavu.
Tukiwa tunaendelea kupata kahawa na
kutafuna miraa si alikurupuka rafiki yangu Ndirangu. Anakuja akipiga kelele,
“Woi woooi, nakwa nie yaani nakufa mie.” punde si punde mkewe Wanjiku anatokea
akiwa ameshika gongo akitaka ammalizie Ndirangu.
wanjiku anahanikiza, “Rehe besha zakwa
ngiri igiri na ihenya, yaani leta pesa yangu elfu mbili haraka.”
msishangae kusikia elfu inaitwa ngiri. Anaendelea, “Ithe wa Katuru, nuuga
rehe besha zakwa naihenya.”
Ndirangu kuona walume wenzie tupo
akajitutumua na kusema, “Dhie wega naiwe. Mutumia mworu uyu-yaani nenda salama,
mwanamke mbaya huyu.”
“Ati, kama unatusi mimi kwa vile iko
mbele ya watu, ukija kwa nyumba napatiana adhabu kali saidi ya Hii. Hii mabo ya
kuleta mudomo kwa bibi hapa jua italeta taabu mingi kwa wewe.” Alijibu Wanjiku
kwa ukali huku akigeuza kurudi zake nyumbani tayari kumngojea mumewe ili akija
ampatie discipline.
Akiwa anaondoka alisema, “Kwa vile
hutaki kuleta besha yangu, ile nyama ya roho na mukimo amepika hukulangi leo
(anamaanisha nayana ya moyo na ugali). Kama unaweza shukua ngwashee uchomege
ukule hapo kwa kahawa.” (Ngwashee ni viazi).
Muiruri anamgeukia Ndirangu na kusema,
“Jamba, mabo ya nyuba uwe unamaliza kwa nyuba siyo kuja hapa na kuleta matata.”
Anatafuna miraa na kuendelea, “Wewe hapana kamata bibi sawa sawa hadi napata
mudomo kukuja hapa na kuropoka bere ya wanaume.”
Izo kumba za moyo sizikwa
Nakoma mabvuto akulobeta mama ine
moyo
Moyo wanga ni mabvuto ine
moyo
Sunga wa busee
Ndinu oletwa ambuye
Oletwa ndinu
Usanga zose ndinu
Moyo moyooo
Naona bi mkubwa kaja acha nitimke
kabla hajanitia discipline.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 14, 2012.
1 comment:
Uninanikumbusha enzi zangu nilivyokua nakua pale Ilala Magorofani nilikuwa na jirani zangu Wakikuyu. Mke alikuwa anamdunda mme wake kila siku mpaka anatoka mbio.
Post a Comment