Tuesday, 6 March 2012

Mama Maria Nyerere anapofunda wasiofundika!

HIVI karibuni mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere alikaririwa akitoa wosia ufuatao kwa wake wa viongozi. Alisema: “Unapokuwa mke wa kiongozi unapata changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutoa dira kwa wengine...unapaswa kufikiri kwa niaba ya wengine, iwe ni kwenye ujasiriamali, elimu, afya au masuala ya kijamii hasa namna ya kukabili changamoto za kina mama na watoto.”

Haya maneno ni ya maana kwa wenye kutia akilini. Ni mazito yenye kueleza mengi katika uchache wake. Mama Maria anawataka wake wa viongozi wa sasa na hata waliopita watoe dira.

Hawa wana dira gani zaidi ya kuchuma na kujineemesha? Nani mara hii kasahau, mfano, fuko la Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) lililoishia kuwa mrija wa kutengenezea pesa kwa kisingizio cha kuwainua kina mama?

Nani amesahau Anna Mkapa alivyotokea kuwa milionea baada ya mumewe kuingia madarakani huku akitajwa karibu katika kashfa nyingi asijibu? Alishindwa hata kumshauri mumewe kutangaza mali wakati wa kuondoka.

Kwa kumbukumbu, zama za Mwalimu, jinsi Mama Maria ambavyo alifanya kazi kuu za kumtunza na kumshauri Baba wa Taifa, wanashangaa kuona wake za watawala waliofuatia kuwa marais nyuma ya pazia kwa kuanzisha NGOs zenye kutia kila aina ya shaka. Ukiacha mke wa Mzee Ali Hassan Mwinyi ambaye naye alishutumiwa kutumia ofisi ya mumewe kuwapatia mikopo ndugu zake, wake wa waliofuata wamekuwa kama wafanyabiashara wa kawaida ambao sijui kama wana dira hata mawazo ya kuwashauri waume zao.

Kama kuna ushauri mke wa Mkapa aliompa ni kujitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ulioishia kuwa aibu ya mwaka kwa ukoo mzima wa Mkapa.

Nani mara hii kasahau kashfa ya Net Group Solution ambayo ilisemekana kuletwa na waliokuwa karibu na ukoo wa bwana mkubwa hasa bi mkubwa?

Ukija kwa mke wa Rais Jakaya Kikwete, Salma, sijui akama anamshauri vizuri mumewe kuhusiana na anavyopasa kutawala zaidi ya kutumia muda mwingi kwenye NGO yake ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo sawa na EOTF inalalamikiwa sana. Sina ugomvi na NGO hii zaidi ya kuona umma unavyoiangalia kwa jicho baya kutokana na namna inavyoendeshwa.

Swali kuu ni kwanini kuwa na NGO baada ya mume kuingia madarakani? Je, NGO hizi zinaweka wazi taarifa zake za ukaguzi wa mahesabu kila mwaka?

Mama Maria alikuwa na uwezo hata udhu wa kuanzisha NGO na ikawa ya kuwahudumia wanawake hata watoto kweli kuliko hizi za sasa ambazo ni shaka tupu. Lakini hakufanya hivyo kutokana na kuepuka mgongano wa maslahi na kujenga mazingira ya waovu kuweza kuitumia kuchafua uongozi wa mumewe.

Nani hajui kuwa ukichunguza wafadhili wengi wa NGO za wake wa wakubwa si watu wenye nia njema? Hili liko wazi hasa kutokana na ukweli kuwa baada ya waume za wenye NGO kuondoka madarakani, NGO zao hudoda kiasi cha kutovutia tena wafadhili. Je, hapa kinachofadhiliwa ni NGO au zinatumiwa kuwa karibu na jungu kuu kama ilivyo sasa?

Huwa nashangaa kusikia kwa mfano mke wa rais anakwenda kutafuta misaada kwa ajili ya wanawake na watoto wakati huo akishindwa kumshauri, kwa mfano, mumewe kuwashughulikia mafisadi, kupunguza ukubwa wa serikali, safari za nje zisizo na ulazima zaidi ya kuumiza uchumi na mambo mengine kama hayo.

Je, huyu asiyeona haya anaweza kuwa na uchungu na hao anaodai kuwa nao uchungu au kuwatumia kwa faida binafsi? Je, kazi ya wizara ya kina mama na watoto ifanye kazi gani kama kila mke wa rais anayeingia anataka kuwatumikia kina mama na watoto?

Basi tufute wizara, maana wizara ya kina mama na watoto ya First Lady ipo na inapokea misaada.

Kama kwelli hawa wanaochangia wana uchungu na kina mama na watoto kwanini wasichangie hiyo wizara husika ambayo ina waziri, naibu waziri, katibu wa wizara, wataalamu na wafanyakazi lukuki kikatiba? Jamani hapa nani anamdanganya nani na nani anamtumia nani?

Ukiondoa Tanzania, sikumbuki kwa mfano kusikia eti mke wa rais mstaafu wa Kenya Daniel arap Moi au wa sasa Mwai Kibaki kuwa na NGO.

Pamoja na ufisadi wake wa kunuka aliokuwa akifanya, hata Mobutu Sese Seko hakuruhusu mkewe kuwa na NGO.

Turudi kwa Mama Maria na kuwafunda wasiofundika wala kufundwa. Je, aliwaambia aliyowaambia kutokana na kuona hawafanyi hayo au kupwaya? Aliwashauri watoe dira baada ya kugundua kuwa hawana dira?

Je, aliwaambia changamoto kutokana na kugundua kuwa changamoto mojawapo iliyowakabili na kuwashinda ni kujitajirisha kutumia mgongo wa ikulu?

Yote yanawezekana. Je, hawa aliokuwa akiwafunda walikuwa na lolote la maana la kumuonyesha mama gwiji huyu au kujikomba tu?

Anasema: “Unapaswa kufikiri kwa niaba ya wengine, iwe ni kwenye ujasiriamali, elimu, afya au masuala ya kijamii, hasa namna ya kukabili changamoto za kina mama na watoto.”

Je, hawa walengwa wetu wanafikiri kwa niaba ya wengine au familia zao tu? Je, wanakabiliana na changamoto zinazowakabili kina mama na watoto au kuwatumia kuwatupia moja katika kila kumi waisakayo kwa kuwatumia hawa wanyonge na madaraka ya waume zao?

Leo utasikia kwa mfano mke wa rais amejenga shule kwao au mwingine kupeleka miradi kwao au kwa mumewe.

Kwanini asiachane na ubangaizaji akamshauri mumewe akawa na sera safi zenye kuwezesha kujenga hizo shule popote badala ya kwao au kwa kuuweka urais majaribuni kama ilivyo? mie naona ni bora ya Mama Maria ambaye hakuacha nyuma hata shule moja wala utajiri binafsi kuliko kuacha shule mia zitokanazo na kufanyia biashara Ikulu na cheo cha rais.

Sikumbuki kusikia tuhuma zozote dhidi ya Mama Maria, mumewe wala watoto wao. Je, hawa wa sasa hali ikoje?

Kila kona ni tuhuma na bahati mbaya hazikanushwi zaidi ya kutoa vitisho visivyo weza hata kutekelezwa. Hivi tuhuma za mtoto wa Kikwete, kujinufaisha kwa kutumia mgongo wa baba yake ziliishia wapi?

Kimsingi, ingawa mawazo ya Mama Maria ni lulu, ima amewafunda wasiofundika au ameamua kuwapasha kwa hekima. Yote yanawezekana.


Chanzo: Tanzania Daima Machi 6, 2012.

No comments: