Wednesday, 28 March 2012

Nkapa na Wahasira mmefilisika

JUZI nilicheka hadi nikalia niliposikia kampeni za kipuuzi kule Arushameru.
Mwanzoni vyama shindani hasa Chakudema na kile cha Magamba viliposema vitafanya kampeni na kampani za kistaarabu nilidhani itakuwa hivyo.

Hivyo niliacha safari yangu ya kwenda Nairoberry kumjulia hali nyumba ndogo yangu –Muthoni. Sorry sikuwa nakwenda kwa nyumba yangu ndogo bali kumsalimia rafiki yangu Ndirangu wa Ndamu wa Jamba Nene ya Ita kule Ithekahuno. Hayo tuyaache. Ila usimwambie bi mkubwa kuwa nilisema nilikuwa nakwenda kuona nyumba ndogo kule Nyeri.

Mie siyo kama Stivi ambaye nasikia kwa nyumba ndogo si mchezo.
Lakini ajabu ni kwamba yeye ndiye wa kwanza kuwashupalia wenzake kuwa wana nyumba ndogo wakati ukweli ni yeye.

Je, hii inatokana na jamaa kutoka usingizini na kujifanya Mpayukaji asijue kupayuka kuna wenyewe? Twende kwenye siasa za kipuuzi.
Kama mnakumbuka kijiwe cha kama wiki tatu hivi zilizopita, nilionya chama cha Magamba kutomruhusu Denjaman Nkapa kwenda Arushameru.

Kwanza nilihofia angepayuka hata kulipuka na kuvuruga kila kitu ikichukuliwa kuwa tangu afanyie umachinga ikuu na kujitwalia machimbo ya Nkaa wa Mawe alijishushia heshima na kuonekana kama waganga njaa wa kawaida.

Pili, anakabiliwa na kashfa ya kuanzisha na kubariki ujambazi wa HEPA ukiachia mbali mwingine kama vile ENBIISII, Chandarua Solution Group –tafsiri neno la kwanza kwa kimombo utajua nimaanishacho.

Tatu, ana kaugonjwa wa kupayuka payuka hasa anapozidiwa kiasi cha kujisahau na kubwabwaja hovyo.
Hivi kwa mfano, kwa msomi mwenzangu na mbishi kama Beni mambo ya Vise kwamba si mtoto wa Nchonga yangekisaidia vipi chama chake?

Kama Mzee alidhani Vice ni mtoto wa nje ya ndoa yeye hana?
Namheshimu sana Mzee wetu lakini anapovamia kazi yangu ya kupayuka sitamheshimu tena.
Kama aliona kupayuka ni raha si angewasiliana nami nikampa mbinu za kupayuka bila kuchemsha.
Najua Nkapa huwa ananisoma sana. Kwanza ni mwandishi mwenzangu ingawa baada ya kuula alianza kututukana waandishi kuwa hatujasoma wakati tumekula vitabu kuliko hata yeye.
Hivi kama angeulizwa alivyouza nyumba za walalanjaa angejibu nini? Natamani nyumba zile nizibomolee mbali kama zile za Gerezani ambazo ziliuzwa kihalali na lisirikali halafu likajipiga mtama na kuzitaka kwa bei ya kijambazi.

Kwangu mimi, Nkapa kama Wahasira walichemsha. Eti linadai litapigana kwa nguvu zake zote kurejesha ardhi ya Wameru iliyoporwa nalo! Ajabu, lingekuwa na aibu hata mmoja si lingeacha kujimilikisha nkaa wa mawe ukiachia mbali kunyakua ardhi huko huko Arushameru na Ushoto kwa kina mgosi Machungi.

Tangu lini mbwa akarejesha nyama?
Nilishangaa kuona jitu zima kama Stivi Wahasira likisema eti Daktari Silaha aliiba pesa wakati wa ujio wa papa sijui dagaa sijui nyangumi.
Mbona lenyewe linalala kila siku likipokea mshahara kwa kusinzia? Je, huu si wizi tosha wa njuluku za Wabongolalanlanders?

Eti ni kweli nawe unapolala huuota urahisi? Ama kweli siku hizi urahisi hauna tena maana hadi unawaniwa na wasinziaji.
Siku Wahasira akiteuliwa nitajinyotoa roho ili nisitawaliwe tena na kilaza mwingine.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 28, 2012.

No comments: