“Kwa nguvu zangu zote wakati nina
uhai, nitatetea haki za wananchi wa Tanzania pamoja na kumilki ardhi na kuitumia
kwa maendeleo yao,” Hiyo ni nukuu ya aliyosema rais mstaafu
Benjamin Mkapa alipokwenda kumnadi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye
uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki.
Kwanza, kwa wengi, hiki kimeonekana
kuwa kichekesho cha aina yake kinachomvua Mkapa nguo kiasi cha kuonekana
kuishiwa mbele ya jamii. Kwani wengi wanauliza: Mbona hakufanya
hivyo yaani kulinda haki za watanzania kwa nguvu zake zote wakati akiwa
madarakani zaidi ya kujinyakulia mali za umma? hata hivyo, hapa
kuna somo kuwa kila chenye mwanzo kina mwisho na ukipewa dhamana ukaifuja
unaishia kuishi kwa aibu, kutegemea kulindwa na hata ghilba na hadaa. Kwa mtu wa
hadhi ya Mkapa, kupayuka si saizi yake achia mbali kuongopa mchana kweupe.
Maskini Mkapa!
Wakosoaji wanahoji: Mkapa anataka
kumdanganya nani wakati siri zake ziko ugani kwa miaka nenda rudi? Hivi Mkapa
anadhani watanzania ni wasahaulifu na mataahira kiasi hicho? Je hapa nani
anajidanganya ukiachia mbali kudanganya? Mkapa hawezi kusameheka bila kuleta
utetezi wake tena unaoingia akilini. Hakuna shaka kuwa sasa Mkapa anahaha kujua
nani atamrithi Jakaya Kikwete ili amhakikishie ulinzi asishitakiwe kwa kashfa
zake na familia yake. akitaka msamaha siyo ajitetee tu bali arejeshe mali za
umma na kuomba msamaha kwa watanzania akikiri kuwa alikosea na kushawishika
kiasi cha kuchafua ofisi waliomwamini kuiendesha kwa niaba
yao.
Wengi
wanashangaa kama kweli wananchi wa Arumeru Mashariki watakubali kugeuzwa wajinga
na wapumbavu ambao wanaweza kuipigia kura CCM kwa kubariki kile kinachoonekana
kwa wachambuzi wengi kama uongo wa Mkapa. Wengi wanahoji: Je Mkapa
anaishi dunia gani ambaye hajui kuwa wananchi hao hao anaowahadaa kuwa
atapigania haki zao kwa nguvu zake zote hadi kufa wanaendelea kukumbwa na
matatizo yatokanayo na uhaba wa ardhi baada ya ardhi yao kubinafsishwa kwa
marafiki na washirika wa Mkapa tena chini ya utawala wa Mkapa huyo huyo.
Amenikumbusha kisa cha Alikwina yaani alikuwa wapi? Mkapa ulikwina ? Badala ya
kujibu hoja vilivyo alikimbilia kujifanya mwanafamilia ya marehemu baba wa taifa
kiasi cha kuwatoa wengine walioamua kumpasulia bomu ambalo limemuacha hoi.
Inashangaza kwa mtu mwenye hadhi ya
Mkapa kukosa kumbukumbu kiasi hiki ukiachia mbali kusema vitu visivyoingia
akilini kama vile. Kwa walioshuhudia au kusikia aibu iliyomkuta rais mstaafu
Benjamin Mkapa wanajiuliza kulikoni.
CCM iliomba kuwepo na kampeni za
kistaarabu na si matusi na uongo. Ajabu CCM hiyo hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza
kuvurumisha matusi ukiachia mbali kusema uongo. Matusi yasiyo na lazima wala
saizi ya Mkap, hata hivyo si kosa la Mkapa. Kwani CCM sasa ni chama
kilichoishiwa kuliko wakati wowote wa historia ya kuanzishwa
kwake.
Watu wanajua ukweliNBC, EPA IPTL
Kiwira Tanesco-Net Group Problems ambazo zilikuwa dhana za utawala wa Mkapa
kujikusanyia pesa binafsi nyuma ya pazia. Nani mara hii Mkapa alivyotishia kila
aliyejaribu kumpa ushauri kwa mfano asiuze NBC? Ni juzi siri ya siri ilifichuka
kiasi cha Mkapa kutuhumiwa kuwa nyuma ya kifo cha baba wa taifa Mwalimu Julius
Nyerere kama ilivyodaiwa na mwanae ambaye naye hajajibiwa na
Mkapa.
Kimsingi, ujio, na maneno na uwepo wa
Mkapa Arumeru Mashariki haukuisaidia CCM bali kuiangamiza. Maana
watu si wapumbavu wala wajinga kama anavyodhani. huwezi kwenda jukwaani
ukahubiri matusi na uongo chama chako kikapewa kura hata kama wapiga kura
wanakupenda au kukipenda chama chako. hapa hapendwi mtu bali haki na maendeleo
ambavyo CCM imeshindwa kutimiza kwa miongo iliyokuwa madarakani zaidi ya kundi
dogo la watu kujihudumia kwa kuwanyonya walio wengi ambao sasa linawahadaa na
kuwafya vipofu na mataahira.
Hivi Mkapa anadhani watanzania
wanasahau athari za kufanyia biashara ikulu ambapo wachukuaji wanaoitwa
wawekezaji walifanikiwa kuiweka nchi yetu mifukoni mwao kwa kuwahonga wakubwa
huku raslimali zetu zikigeuka laana kwetu? Kama amesahau aende Mara, Mwanza,
Shinyanga hata arudi huko Arumeru aone madhara ya sera na uroho wake. Aende aone
watu wake wanavyowanyanyasa watanzania huku wakipora raslimali zao na kuacha
madhara makubwa kiikolojia. Maskini Mkapa hayaoni haya yote. Bado anaotea siasa
za kibabe na urushi za wakati wake ambapo alidai kuwa sera yake ilikuwa uwazi na
ukweli kumbe akimaanisha kinyume kama ilivyokuja kubainika kuwa sera yake
ilikuwa ni uchukuaji, usiri na uongo.
Mkapa anapaswa kuambiwa kuwa aache
kudhani kuwa watanzania ni kama mawe ambayo huwa hayabadiliki wazi wazi ingawa
yanabadilika. Maskini Mkapa. Aibu! Wahenga waliasa kuwa asiyejua maana haambiwi
maana na asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Heri Mkapa angejiendea Moshi, Lushoto
au Mtwara akajipumzikia kama siyo kulowea Upanga kuliko kuzidi kuwachokoza
watanzania aliowadhulumu yeye familia yake na marafiki zake alioshirikiana nao
kwenye makampuni yao ya kuiba Kiwira.
Tumalizie makala hii kw a kumtaka
Mkapa akumbuke maneno haya wakati akitafakari nafasi yake kama rais mstaafu.
“Ndugu zangu msidanyanyike na kuendelea kuwasikiliza CCM miaka yote wameshindwa
kurejesha ardhi ya Meru sasa wanaibuka…..huyo Mkapa alishindwa akiwa rais sasa
amekaa nyumbani akisubiri posho ataweza kumshauri rais awarudishie ardhi
yetu?” Mbunge Israel Natse (CHADEMA) jimbo la Karatu. Mnaweza
kuongeza kuwa: Kwanini Mkapa kama ni jabali kweli hataki kujibu tuhuma za uchafu
aliofanya akiwa ikulu?
Chanzo: Tanzania Daima Machi 21, 2012.
No comments:
Post a Comment