Tuesday, 21 April 2015

Ajali za Barabani: Kijiwe Chaishukia Sirikali


          Baada ya mheshimiwa Bwege kupoteza ndugu zake kwenye ajali iliyotokea huko Rufiji hivi karibuni, Kijiwe kimekaa kama kamati kutoa shinikizo kwa lisirikali likomeshe jinai hii ya kizembe na ya kujitakia kama jamii.
          Mheshimiwa Bwege baada ya kupokea salamu na michango ya rambirambi toka kwa wanakijiwe analianzisha, “Jamani, hali ya ajali za kujitakia za barabarani zitokanazo na mfumo wa kishenzi na wa kifisadi zitatumaliza tusipochukua hatua. Ni juzi tu nimepoteza ndugu zangu watano kwenye ajali ya barabarani. Mwaka jana mke wangu alipoteza ndugu watatu kwenye ushenzi huu huu. Jamani tufanyeje ili tunusurike?”
          Mbwamwitu anaamua kujibu haraka, “Tumuulize Pombe Makufuri anayejinadi kwa kuchapa kazi wakati ni wale wale. Hapa waziri hawezi kunusurika. Maana anajua chanzo cha ajali za mara kwa mara lakini hataki kuchukua hatua.”
          Sofia Lion aka Kanungaembe anadakia, “Acheni uvuvi wa kufikiri jamani. Sasa waziri anahusikaje na ajali kama siyo uzushi na kukosa la kusema ukiachia mbali kutaka kuwabebesha wengine lawama?”
          Msomi Mkata Tamaa aliyekuwa akisoma gazeti lililokuwa likizungumzia ajali ya kutisha ya mabasi, analiweka pembeni na kutia guu, “Dada yangu Sofi inapaswa uelewe kuwa waziri ndiye anahusika na sera na sheria za barabarani. Asemayo Mbwamwitu ni kweli. Maana waziri anajua kuwa chanzo cha ajali za barabarani hapa kayani ni barabara zenyewe. Nakumbuka, alishaambiwa kuwa barabara nyingi zimepungjwa ukubwa ili mafisadi wapata chao. Je nani unataka ashughulikie kadhia hii kama si waziri anayehusika na ujenzi wa barabara?”
Mijjinga aliyekuwa akisoma gazeti baada ya Msomi kuliweka mezani, analiweka pembeni na kubusu mic, “Sofi una matatizo ajuaye ni Mungu. Yaani unashindwa kuona vitu rahisi kama hivi au unajifanya tu?”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anadakia, “Mpe vipande vyake. Amezidi kujifanya na kujitia tia wakati hajui kitu. Anajifanya msemaji na mtetezi wa lisirikali chovu na ovu linalonuka utadhani kuna kitu anapewa au kulipwa.”
Mijjinga anaendelea, “ Hapa hakuna cha kutwisha watu lawama. Wanazistahili. Hata hivyo, wana bahati. Maana, kaya hii isingekuwa ya wachovu na woga waziri kama huyu angepigwa chini haraka sana ili wenye uwezo wachukue nafasi yake na kufanya kazi vilivyo.”
Mpemba anaramba mic, “Yakhe msemayo ya kweli ati. Hivi, hawa waniotaka tusilaumu sirikali wataka tunlaumu nani?” Anamgeukia Sofia na kusema, “Dadangu sasa naanza amini kuna kitu kimekuingilia wallahi. Maana sikutegemea kama ungeweza tetea waovu tena wakati huu tunipoomboleza vifo vya ndugu zake ndugu yetu Mheshimiwa Bweeege. Hivi hawa walopoteza maisha wangekuwa nduguzo ungewezayasema haya uniyosema?”
“Mpe vipande vyake. Hebu yakhe mpe dozi huenda atatosheka aache mapenzi ya kibubusa.” Anachomekea Mipawa.
Mgosi Machungi anakula mic, “Tinamishangaa dada Sofi. Japo shiwezi kusema kuwa ameiingiwa na kitu fulani, sasa naanza kuamini. Si bue. Naona timuuize da Sofi yeye anadhani suuhu ya tatizo la ajai ni nini?” anamgeukia Sofi ambaye anaonekana kuudhika wazi.
Kanji anaamua kumuokoa mshikaji wake Sofi. Anakwanyua mic, “Dugu zangu samehe yeye hapana jua ile natetea.” Anamgeukia Sofia na kusema, “Dada yangu nini naingilia veve dugu yangu? Mbona nyuma haikuwa hivyo dada yangu Sofi? Nini napewa tamu hivyo na sirkali mpaka natetea kila kitu?”
Kijiwe hakina mbavu jinsi Kanji anavyoongea maneno yanayotafsiriwa tofauti na alichokusudia.
Kapende aliyekuwa akitikisa kichwa anaamua kutia buti, “Ndugu zangu, msimshangae Sofi. Wapo wengi kama yeye wenye mapenzi ya kibubusa kiasi cha kushabikia maafa ya wenzao. Kama alivyouliza Ami, hivi hawa wahanga wangekuwa nduguzo ungeyasema haya unayosema au ni kwa vile hawakuhusu? Kama hawakuhusu sisi wanatuhusu na isitoshe leo hawa kesho hujui atakuwa nani hasa ikizingatiwa kuwa sisi wachovu hatusafiri kwa madege kama wao wanaosimamia maafa yetu.”
Msomi anarejea, “Nadhani tuachane na Sofi na kumtumia salamu waziri mhusika kuwa arekebishe uoza wa kupunguza upana wa barabara na kuzijenga chini ya kiwango. Nadhani kaya yetu ndiyo yenye barabara finyu kama vijia vya panya duniani kutokana na kutawaliwa na walaji, walafi, mafisi na mafisadi. Mbona hatusikii hizi ajali kaya jirani kama si ukweli?”
    "Yakhe hawa watu wajue sana hili tatizo. Maana wakisafiri wao hufunga barabara ili wasikutane na vichaa wendao kasi wakawanyotoa roho," Anachomekea Mpemba.
Mijjinga anakatua mic, “Nadhani tatizo jingine ni wenye mikangafu kutoihudumia ukiachia mbali kuwafanyisha kazi madereva kwa muda mrefu bila mapumziko. “
“Kaka umesahau wazee wa mabao yaani wale nyangenyange wa barabarani. Wanawatoa watu upepo na kuacha wapakie abiria wengi watakavyo badala ya kuangalia uwezo wa magari.” Anachomekea Mipawa.
Mgosi anarejea, “Usemayo ni kwei tupu. Juzi nikitoka Ushoto niishuhudia taafiki akipokea bahasha toka kwa konda wa basi aiyekuwa amepakia abiia kupita kiasi. Kwei hawa nao ni chanzo cha ajai.”
Kapende anampoka Mgosi mic na kuongeza, “Chanzo kingine ni mwendo kasi. Tatizo na suka wetu wengi wanadhani kukimbiza magari ndiyo ufundi. Juzi nilishuhudia abiria wakimshangilia muuaji aliyekuwa akikimbiza gari utadhani alitaka lipae. Hawa nao ni wa kutupiwa jicho.”

Kijiwe kikiwa kinanoga si vipanya (daladala) viwili vikavaana katika kuwahi kugombea abiria. Ilibidi tuwahi kuokoa majeruhi hasa baada ya kuona gari likianza kutema moshi. “Ama kweli ajali zitamaliza wengi tusipowajibisha wakubwa wanaohujumu miundo mbinu.” Aljisemea Mzee Maneno.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 22, 2015.

No comments: