Monday, 27 April 2015

Kufungwa mtoto wa rais somo kwa marais watoto

  • Abdoulaye Wade y Karim Wade
    Rais wa zamani wa Senegal Abdulaye Wade na Mwanae Karim wakati akiwa madarakani
   Kupatikana na hatia ya wizi wa fedha za umma na kuhukumiwa kifungo kwa mtoto wa rais wa zamani wa Senegal, Karim Abdulaye Wade kuna mafunzo mengi.
Kwanza, kila kitu kina mwisho chini ya jua. Maana jinsi Karim na baba yake walipokuwa madarakani walionywa mara nyingi wala hawakusikia cha muadhini wala mteka maji kwa vile madaraka mara nyingi hulevya. Hawakuamini kuwa madaraka yangefikia kikomo siku moja.
Pili, cheo ni dhamana. Hili liko wazi sema watu wengi wanapoyapata hulewa na kujisahau. Badala ya wengi kutimiza dhamana waliyopewa na umma huutumia umma kujineemesha wasijue wengine wanaweza hata huo utajiri waliouchuma kwa kuuibia umma wanaweza wasiufaidi kama ilivyotokea Libya.
Tatu, Afrika inahjumiwa na waafrika wenyewe hasa wanaotumia madaraka vibaya pamoja na wake, watoto, marafiki na waramba viatu wao.
Nne, wakati mwingine usomi wa mtu hauondoi ujinga wake. Rais wa zamani Wade ni profesa tena wa sheria lakini aliyeivuja na kuivunja sheria vibaya. Rejea maprofesa wetu hapa nchini walioboronga hadi wengine kuondolewa kwa kashfa za upokeaji vijisenti na kusimamia wizi wa fedha za umma.
Karim, kama Seif al Islam Gaddafi, alikuwa akiandaliwa kumrithi baba yake. Alipewa uwaziri kwenye serikali ya baba yake.  Alifika pale alipofika si kwa sababu ya sifa nyingine zaidi ya kuwa mtoto wa rais. Je Afrika inao akina Karim wangapi ambao hawajahukumiwa lau kupata stahiki ya jinai walizotenda? Je ni wangapi wamejifunza tokana na anguko hili takatifu?
Baada ya kuondoka wakoloni weupe wakawaachia mamlaka wakoloni weusi, kuwa rais Afrika maana yake ni kwamba ukoo wote unakuwa marais kwa namna wawezayo. Wake za viongozi japo si wote wanaunda kampuni almaaruf NGO na kujipatia utajiri wa ghafla kwa kutumia mgongo wa ikulu. Kulipana fadhila na udugu, kujuana na kulindana vinachukua nafasi kiasi cha kushindwa kutofauti kati yao na genge la wezi. Wengi wa marais wameruhusu wake au watoto au marafiki zao kuwa karibu kila ufisadi unaotendeka kwenye mataifa yao. Mtoto wa rais Congo Denis-Christel Sassou Ngweso anasifika kujihusisha na karibu kila kashfa inayohusisha mabilioni ya dola nchini humo. Mtoto wa rais wa Afrika Kusini, Duduzane Zuma anasifika kwa kushirikiana na familia ya kihindi ya akina Gupta kujipatia utajiri wa kutisha. Ilifikia mahali hata akaruhusu ndege binafsi ya wahindi hawa iliyobeba maharusi kutua kwenye kituo cha kijeshi kinyume cha sheria na hakuna kilichofanyika. Binti wa Zuma, Thuthukile (25) alipewa kazi ya ukuu wa watumishi kwenye Wizara ya Posta na Mawasiliano nafasi ambayo hajawahi kupata mtu kwenye umri huu bila uzoefu wala elimu ya kutosha. Kama haitoshi, mpwa wake Zuma aitwaye Khuhulubuse Zuma anakabiliwa na tuhuma za kufilisi shirika la umma la Aurora ambapo alikuwa ameteuliwa na ndugu yake kuwa mwenyekiti.
 Bado dunia inakumbuka jinsi watoto wa rais wa zamani wa Kenya Moi walivyojitajirisha kwa vile baba yao alikuwa rais.
Karim sasa ni mfungwa baada ya kupatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela miaka sita. Mwezi Machi umekuwa mbaya kwa watawala wa kiafrika. Kwani mke wa rais wa zamani wa Ivory Cost, Dr. Simone Gbagbo alihukumiwa kwenda jela miaka 20 wiki moja kabla ya Karim.
Hata hivyo haya matukio yanatukumbusha kitu kimoja kikubwa kuwa bara la Afrika mara nyingini ni maskini si kutokana na ukosefu wa raslimali wala wachapakazi bali usimamizi na utawala bora. Viongozi wengi wa kiafrika wameruhusu ndugu na marafiki zao kuzihujumu nchi zao kwa kupewa vijirushwa kidogo wakati wanaowatumia wakijiingizia mabilioni ya dola na kuyatoroshea nje huku wakiliacha bara maskini huku watawala wake wakisifika kwa kuombaomba na kukopakopa. Wengine hata hicho wanachoomba hakifikishwi nyumbani zaidi ya kuachwa huko huko ughaibuni kwenye mabenki almaarufu kwa kuficha fedha.
Somo jingine unaloweza kupata kutokana na kufungwa kwa Karim ni kwamba upinzani unaposhinda na kuingia madarakani, uwezekano wa kubadili mambo ni mkubwa ingawa hili siyo mia kwa mia. Nchini Kenya, upinzani ulipoingia haukuwachukulia hatua Moi na watoto wake. Tofauti, nchini Zambia, Fredrick Chiluba na mkewe walichukuliwa hatua za kisheria hadi bi mkubwa kuonja jela. Nchini Malawi mambo yamekuwa nusu kwa nusu kuhusiana na tuhuma zilizomkabili rais wa zamani Bakili Muluzi.
 Tuhitimishe kwa kushauri wahusika watie akili wakijua fika kuwa hakuna kisichobalika chini ya jua. Leo wanakula kwa kujidai wengine hata bila kunawa. Wanatanua kwa msemo wa kisasa, wajue fika mwisho ukifika wanaweza kuishia pakanga. Pia wafahamu kuwa upogo na uroho wao ndicho chanzo cha bara letu kuwa maskini, kukosa usalama na maendeleo. Kuna maisha baada ya kuondoka madarakani. Pia tuwasihi wananchi kuanza kuchukia huu utawala wa kifalme wa kisiasa unaorejeshwa kwa mlango wa nyuma.
Chanzo: Dira.

No comments: