Monday, 6 April 2015

Mmeamua kuua utunzi na uchapishaji wa vitabu siyo?


Mtunzi maarufu Shaban Robert aliyesahaulika pamoja na mchango wake wa kipekee katika tasnia ya utunzi
 
Naandika makala hii kwa masikitiko makubwa sana. Moyo wangu unasononeka kutokana na jinsi elimu ambayo hapo zamani ilikuwa ufunguo inavyonajisiwa na kuharibiwa bila sababu za msingi wala ulazima. Inakera na kuumiza ajuaye Mungu na waathirika wa kadhia hii ya kutengenezwa na watu wachache wasio na uzalendo kwa maslahi binafsi tena ya muda mfupi.
Hivi karibuni serikali imekuja na kile ilichokiita sera mpya ya elimu kwa taifa. Hata hivyo, ukiangalia yaliyomo kwenye sera husika unadiriki kusema si sera kitu. Japo sera husika ina mapungufu mengi, hakuna lililostua wengi kama kusema kuwa tangia sasa wanafunzi watasoma kitabu kimoja kimoja kila darasa. Ili iweje? Kwanini kitabu kimoja? Je tuna uhaba wa vitabu au kuna tatizo jingine. Wahusika hawakutoa majibu wala sababu za maana za kuua na kuidhalilisha elimu kiasi hiki.
Inashanga kuona wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inayosimamiwa na mtu mwenye shahada ya uzamivu (PhD) Shukuru Kawambwa –ambaye kimsingi anapaswa kujua umuhimu wa elimu –kukubaliana na kupitisha madudu haya. Je mnapotumia kitabu kimoja, kitapatikanaje bila tenda ya kukitunga kutolewa kifisadi kama ilivyozoeleka? Je hao watunzi na wachapishaji vitabu mmewaweka kundi gani katika biashara hii ya maarifa? Je wahusika wamezingatia maslahi ya taifa au maslahi yao na watu wao ambao watateuliwa kutunga vitabu tena kwa kubabaisha ili wapate tenda na kutoa vitabu vya hovyo ilmradi wao wapate chao?
Siamini kama busara iliyotumika ina mantiki au kuzingatia mahitaji ya taifa hasa wakati huu ambapo dunia inashuhudia ushindani mkubwa kielimu. Nashangaa, wakati Tanzania ikipitisha balaa la mwanafunzi kusoma kitabu kimoja, binti yangu wa darasa la kwanza hapa Kanada kwa mwezi anasoma si chini ya vitabu thelathini vya watoto ambavyo hupewa akaja navyo nyumbani na wazazi wakamsimamia akawasomea wakamkosoa na kumsaidia alipokwama na baadaye kuandika mapendekezo yao, na udhaifu waliogundua ili walimu wamsaidie. Je huyu unaweza kumpambanisha na mwenzake aliyesomea kwenye sakafu halafu akasoma kitabu kimoja?  Je kwanini wakubwa wametenda jinai hii au ni kwa vile wana fedha na fursa ya kuwapeleka watoto wao ughaibuni wakapata elimu bora ili wanaporejea wawatawale wajinga wa kutengenezwa na sera kama hii?
Kusema ule ukweli ni kwamba siku hizi elimu, watunzi na wachapishaji wa vitabu wametiwa kitanzi sijui ili iweje. Siku si chache tutaanza kununua vitabu hata vya Kiswahili Kenya na Uganda kana kwamba Kiswahili si lugha yetu. Mfano wa karibuni ni kwamba nilitoa kitabu changu cha pili kiitwacho NYUMA YA PAZIA. Tokana na ujinga, upogo, kujuana, ufisadi na woga vilivyotamalaki nchini, nililazimika kukichapisha nchini Cameroon ambako hawajui hata neno moja la Kiswahili.  Kwa kujua thamani ya elimu, kitabu husika kimo mbioni kutafiriwa kwa kiingereza ili waone jinsi ya kukitumia mashuleni na vyuoni. Hapa maana yake ni kwamba unapokataliwa hapa jaribu pale. Je hata hivyo, ni wangapi wana uwezo wa kufanya hivyo?  Baada ya kugundua janga linalokabili elimu, watunzi na wachapishaji nchini, nimechukua uamuzi mwingine. Kwa sasa nimeamua kuandika vitabu vya Kiingereza tena vya elimu ya juu baada ya kugundua kuwa nchi yangu haina uchungu na elimu wala sanaa ambayo imegeuka matusi ya nguoni na kienyeji. Hata hivyo, unategemea nini unapokuwa na viongozi wanaoshabikia kughushi na kuzawadiwa shahada kama shada la maua?
Hata hivyo, hebu tuuangalie ukweli hata kama unakera na kuuma. Hivi, unategemea nini kwenye nchi ambapo kila mtu anaweza kuukata kirahisi bila kutumia maarifa zaidi ya jinai? Unategemea nini toka nchi ambako viongozi wa juu kama vile mawaziri wanaghushi sifa na shahada za kitaaluma na hawawajibishwi, kushtakiwa wala kuona aibu huku wakiendelea kufanya madudu? Je wahalifu kama hawa wanaweza kuona umuhimu wa elimu wakati wana sifa uchwara ambazo hawakuzitolea jasho? Kwao elimu si bora sawa na utajiri hata kama unatokana na njia chafu kama vile ufisadi, rushwa, wizi, ujambazi, utapeli, miahdarati hata kudhalilishwa.   Hata hivyo, tuwe makini na tayari. Vizazi vijavyo vitatulaumu na kutudharau kama kizazi kibovu ambacho hakikutumia akili wala uzalendo katika kutenda mambo yake. Sishangai kuyasoma haya wala sitegemei hawa manyang'au wanaweza kubadilika. Hata hivyo wana shida gani wakati wanaiba fedha ya umma na kusomesha watoto nje ya nchi kwa kodi za wannchi wanoawahujumu kwa shule za kata ambazo mimi huziita shule za kataa elimu?

Tumalizie kwa kuwataka wadau wa elimu nchini kupinga juhudi hizi zisizo na tija kwao na taifa la kutaka wanafunzi wasome kitabu kimoja jambo ambalo litawanyima fursa ya kupata maarifa zaidi na uwezo wa kupambanua na kuchambua mambo kisomi. Kwanini tunarejesha taifa nyuma hata kuliko kabla tulipoachwa na mkoloni? Kutumia kitabu kimoja mashuleni – licha ya kudumaza akili za wanafunzi – ni kuhujumu na kuua watunzi na wachapishaji wa vitabu jambo ambalo si jema kwa mustakabali wa taifa. Serikali haiwezi kuruhusiwa kujifanyia inavyotaka wakati ipo madarakani kuwahudumia – si kuwahujumu wala kuwatumia wanachi – bali kuwatumikia kwa namna wanavyotaka. Hapa lazima tuseme wazi kuwa kutumia kitabu kimoja – licha ya wahusika kuchemsha – wameonyesha upungufu wa hali ya juu tena wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi. Nadhani hiki kitakuwa kichocheo cha kutowapa kura kwa vile wanaonyesha wasivyojali maslahi ya taifa bali maslahi yao binafsi kama ilivyoonyeshwa hapo juu.
Chanzo: Dira ya Mtanzania.

2 comments:

Mbele said...

Mara kwa mara, napata wazo kuwa sisi tunaowapigia kelele wa-Tanzania kuwa wajijengee utamaduni wa kununua na kusoma vitabu tumekuwa ni sauti iliayo nyikani.

Tunafahamu maana na umuhimu wa kusoma vitabu. Tumezunguka sehemu mbali mbali duniani tukaona wenzetu walivyo, na tunaona wazi jinsi Taifa letu linavyojichimbia kaburi, na tunapiga kelele kuokoa jahazi.

Lakini hakuna ushahidi kuwa tunasikilizwa. Tumekuwa ni sauti iliayo nyikani.

Hata hivyo, ni wajibu wetu kuendelea kupiga kelele, maana sisi ni kama mtu ambaye amemwona simba mkali, karibu na kijiji, akawa anahangaika na kupaparika kuwatahadharisha wanakijiji wenzake.

NN Mhango said...

Kaka Mbele nakushukuru kwa mchango wako. Usemayo ni kweli. Sauti yetu ni ya mtu aliyeko nyikani ingawa mbuzi tunayempigia gitaa hachezi wala hataki kusikiliza. Kama usemayo, hii isitukatishe tamaa. Maana kuna maisha baada ya sisi. Kesho kwetu ni muhimu kuliko leo hasa ikizingatiwa kuwa tumekuwa na ujasiri wa kusema, "Hii siyo' ili kuokoa taifa letu toka kwenye mikono ya vihiyo na wahalifu wasioona mbele kama jina lako. Hata hivyo, naamini. Iko siku ukweli utasimama na kutuweka huru wakiwamo wao. Hii ni kadhia na balaa la kuwa na watawala vipofu wanaotumia matumbo kufikiri badala ya vichwa wakiiba na kula kwa mikono na miguu tena bila kuiosha wala kuangalia mbele wala nyuma.