Saturday, 4 April 2015

Mlevi kugombea "urahisi" kidizaini

  Nitahakikisha nawaingiza mjini walevi ili niwatwishe mkenge.  Maana nikishaingia ikuu kwenye ulaji rahisi na wa dezo kwangu, familia yangu na marafiki na waramba makalio yangu, nitawaacha solemba. Hata wakichukia wakataka waandamane na michupa yao ya gongo ili wanitie adabu hawatanipata. Nitajizungushia walinzi, mabaunsa, ma-body guards na waramba makalio wawazuie. Najua wakifanya kosa wakaja ikulu kudai tunajuana watajutia siku hizo. Lazima wapambe na walinzi wangu wapige kata funua tena kwa kulipwa kodi zao. They’ll regred why they trusted me. Wakija na madai kuwa waliniunga mkono, nitawapa laivu kuwa zile njuluku nilizowapa, ulabu, bangi na mapupu vilikuwa vya kuniwezesha ili nijiwezeshe mimi na watu wangu au vipi?
Nimegundua kuwa ukiwa kwneye kaya ya walevi na wachovu wanaotanguliza njaa wakifikiri kwa matumbo unaweza kuukata kirahisi hivi hivi ukawa rahisi. Kama nilivyowahi kuahidi siku zilizopita, nikiwa rahisi na bi mkubwa anakukwa raisa. Ataunda NGO yake ya MAULAJI yaani Maendeleo, Amani, Umoja Lazima na Ahadi kwa Jamii na Inji. Washikaji zangu wajiandae kutanua kwenye vyeo mbali mbali kama vile ubalozi, uhishimiwa wa kuteuliwa, ukuu wa mikoa na wilaya. Hapa bila shaka patachimbika bila jembe kwa vile na bi mkubwa atataka mashoga na ndugu zake niwape ulaji. Halo halo! Ni ulaji kwenda mbele.
Najua walevi walivyo na tamaa kama ya fisi, wataingia mkenge wangu kwa kujidhalilisha kwenda mitaani kuandamana kuniunga mkono wasijue mie si mwenzao. Wajua kuwa fisi ni kiumbe mroho awezaye kula hata nyama ya mwenzake? Unategemea nini binadamu anapojigeuza fisi eti kisa njaa. Fisi-binadamu ni mbaya kuliko hata fisi. Maana fisi hula nyama ya mwenzie lakini hauzi vizazi vyake japo huvirithisha mchezo ule ule wa tamaa.  Mimi ni bonge la msanii ati. Naona yule anatikisha kichwa akidhani bangi ndizo zinanisukuma kuyasema haya. Utaliwa weye. Chunga sana mimi iko sanii bwana.  Kama veve iko ingia anga yangu mimi kula veve dugu yangu.
Nikishawapa mshiko hawa walevi wachovu na wajinga, nitaita waandishi wa umbea nyemelezi wapige picha kwa sana na kuandika makala za kunisifia ili walevi waingie mkenge niwabamize kinomanoma bila huruma. Najua hapa madhambi yangu kama vile kubaka, kukwapua njuluku za walevi vitasahaulika. Ile kashfa yangu almaaruf kama Richboozers itasahaulika kwa vile walevi hawana bahati ya kujaliwa kuwa na kumbukumbu na wakiwa nazo zinakuwa kama theluji, zinayeyuka baada ya muda mfupi. Kwa akili zao za soda najua wataingia mkenge nami nitakuwa rahisi ili nianze matanuzi na makamuzi hasa kwenda ughaibuni kucheki akaunti zangu na afya yangu au vipi?
Waandishi nyemelezi lazima niwaahidi vyeo hata kama nina mpango wa kukwapa wawili watatu na wengine kuwaacha Solemba. Kwa walevi na wachovu wanavyopenda ulaji wa dezo, bila shaka, wataingia wengi na kuachwa Solemba wengi pia. Najua wameishasahau jamaa na mshirika wangu Jei Kei alivyowaahidi wote ukuu wa wilaya akawapa wachache na wengine wakabaki kusoneka. Pia wengine nitawaahidi usemaji wa ofisi ya rahisi ili wapate motisha na kuukwaa mkenge kirahisi huku wakitelekeza miiko ya maadili ya taaluma yao wachangamkie madili hewa. Hapa lazima ufanye kama mbayuwayu au vipi? Changanya na zako uwakomeshe viherehere waofikiri kwa matumbo badala ya ubongo wakidhani watakutumia wasijue unawatumia na kuwatema kama nepi au tissue ya chooni. Tuache utani. Wakati mwingine huwa nashangaa jinsi ambavyo mja anawez akujigeuza nepi diaper au kopo la chooni akatumiwa asisituke! Ama kweli ujinga ni mzigo mzito na adui yako muombee njaa.
Kwa vile nimeishaunda chama changu ambacho kinaitwa Chama cha Maangamizi (CcM) lazima niangamize njuluku za walevi. Lazima nihakikishe namteua kitegemezi wangu anayefanya kazi pale Benki Kubwa kuwa Gavana wake ili tuchange njuluku.
Kuzidi kuwakamata walevi na wachovu, jitihada zangu za kuusaka urahisi kwa udi na uvumba, halali na haramu nitaziita safari ya matumaini ili kuwatia matumaini wasijue nitawakata maini baada ya kutua sehemu. Lazima kutumia jina zuri hata kama una nia mbaya kama rafiki na mshirika wangu. Kauli mbinu muhimu. Ngoja nifikirie kauli mbinu nyingine. Kwanini nisitoke na KUFA yaani Kuendeleza, Utajirisho, Fanaka and Amani.  Ngoja niondoke na UMIA yaani Uchumi, Maendeleo Imani and Amani. Hapana, wanaweza kustuka. Acha nitoke na FUFUA yaani Fanikisha Uchumi, Fanikisha Amani. Kwa hii nitawapata hata matapeli wanaojiita watu wa God. FUFUA au tuseme Fanya Ufisadi Faidi Utakavyo kwa Amani.
Naona time imekwisha wakuu. Hilo ndilo neno la God.

Maasalaamu tuonane kwenye uchakachuaji ujao na siku nikitawazwa kuwa prezo wenu.
Chanzo: Nipashe Aprili 4, 2015.

3 comments:

Anonymous said...

wewe ropokwa tuu huyo ndie laisi mtalajiwa kama unaye wakoo mtaje

Anonymous said...

hilo ndio chaguo la watanganyika

NN Mhango said...

Anon umetumwa au unajituma na ni changuo la watanganyika wapi kwani umeongea nao wote au ni ile kutafuta riziki hata kwa kudhalilishwa kwenda kumshawishi utadhani anatafutwa mchumba.