Saturday, 25 April 2015

Mlevi kuanzisha kanisa ili anunue Boieng


          Baada ya kugundua kuwa jina la bwana God linalipa, basi mzee mzima nasukuti kuanzisha kanisa la Upendo, Furaha, Uzima Fanaka na Utajirisho, Kupitia Ombi (UFUFUKO). Katika kuhakikisha napata njuluku toka kwa walevi na wachovu waliokata tamaa kiasi cha kuamini kila anayewaingiza mkenge kwa kisingizio cha kutatua matatizo yao, nitahubiri utajirisho wa chap chap bila kulazimika kuingia kwenye jinai kama EPA, Richmonduli, escrow an MWAPORC inayonukia kule kwa akina waja leo waondoka leo Mwambani.
Ili kupata njuluku ya kutosha, nitawalenga akina mama ambao bila shaka ni wengi kayani. Nitahubiri jinsi ya kuimarisha ndoa, kupata mtoto na kupendwa na waume zao ili wawachune vizuri. Si utani. Kama huzai au umechelewa kuzaa we njoo kwangu utapata mapacha idadi unayotaka hata kama ni kuzaa kumi kwa mpigo. Hakuna lisilowezekana kwangu.
Kama haitoshi, nitauza CDs zangu zenye mahubiri yangu ya urongo na ukweli bila kusahau maji upako, vitambaa vya baraka na kanda zangu za video nikihubiri. Nitawaingiza mkenge watakaopwakia huduma sorry hujuma yangu kuwa ninafanya miujiza ambayo haijawahi kufanywa na yeyote.
Naona yule anatikisa kichwa akidhani hii ni mipango ya bangi asijue wapo wengi ambao wameishaula kirahisi kama marais kwa kujificha nyuma ya neno la bwana. Nani mara hii amesahau kuwa kidhabu mmoja kule Nigeria aitwaye TB Joshi sasa ni bilionea wa kutupwa tokana na kuwaingia mkenge wajingawanjinga wasiojiamini? Pale Kenya yupo rafiki yangu Vickie Kanyare anayehubiri radioni na kwenye runinga huku akipanga matapeli kutoa ushuhuda wa uongo radioni na kwenye runinga ili kuwavutia wajinga? Kwani hapa Bongo hawapo? Mbona wengi tena wengine walitumia huu usanii hata kuupata uheshimiwa. My friend Get Rwakatarehe hupo hapa? Wengine wameula hadi wakanunua hata vyelikopta na kuishi kwenye mahekalu huku wachovu makapuku na wajinga wanaowachuna wakitembea hadi kanda mbili kuwakatikia wakingojea miujiza uchwara. Hapa my friend Jose Gwaijimama utakuwa unanipata vilivyo au vipi?
 Kwa vile kaya hii ni ya walevi mazezeta na washirikina, lazima utumie ujinga wao kupiga njuluku au vipi? Najua mwezi wa kumi lazima nitaukata kama sina akili mbaya hasa pale nitakapoanza kuhubiri kutenda miujiza ya kisiasa ambayo inawabadili wapiga kura kukupigia kura ya kula hata kama hawakupendi. Ukija kwangu utapendwa hata na ndege watake nao kukupigia kura ili ule dezo kama wengine ukiachia mbali kuitwa mhishimiwa hata kama u muishiwa au MPig kama wawaitavyo jamaa zangu wa kaya ya Nyayo pale jirani. Nilishasema tangu zamani. Huna haja ya kwenda Bwagamoyo au Sumbawanga wakati mtume mwenyewe wa walevi nipo na nimepata ufunuo toka kwa mwenyewe top. Usiende huko unakotakiwa uwapelekee mifupa ya wenye ulemavu wa ngozi na ndevu za bibi yako na mkojo wa kuku. Kwangu ni rahisi kupata hata urahisi, uhishimiwa hata kuteuliwa ukuu wa mkoa na wilaya. Huna haja ya kufanya kazi chafu kama vile kuwashambulia akina mzee Jose Waryuba ndiyo uteuliwe ukuu wa wilaya. Uhitaji kupoteza njuluku kwa makanjanja wajifanyao diaper aka nepi kujikomba kwa wakubwa wakiwatungia vitabu vya kipuuzi vya kuwasifia au kuandika makala za kuwasifu magazetini wakisaliti taaluma yako na kuzika heshima na utu wao. Njoo kwangu uokoe njuluku yako na kashfa na aibu ya kulipa fadhila baada ya kuupata ukuu kwa njia haramu kama yule jamaa yangu Jambazi Kuu (JK). Uhitaji akina Makondokonda wala Rweyependekezamu na matapeli wengine kama hawa. Uhitaji akina Bagendagenda wakutungie vitabu ambavyo hata ndege akisoma anajua ni njaa kujikomba na utapeli.
Kwa wanasiasa habari hii ni njema kuliko zote. Kama una mshiko wako unaweza kutumia jina langu kununua chopa ya kupigia kampeni zako.  Wafanyabiashara wanene wanene njoo kwangu niongeze utajiri wenu. Nafanya miujiza kweli. Guess what. Ni simple. Kwa vile dhehebu langu litakuwa linapewa misamaha ya kodi kwa vitu nitakavyoingiza kayani, basi njoo kwangu tuongee. Dili lenyewe liko hivi, unatumia jina langu kuagiza mali zako. Zinapita bila kutozwa kodi. Wewe unanikatia cha juu unatajirika nami natajirika. Kwani kuna mbaya kuibia kaya ya mazoba?  Je huu si muujiza kweli? Huna haya ya kusumbuana na kutolewa upepo na maafisa wa TrA wakitaka chao. Mie nakutoza kidogo tena nakuombea biashara zako ziongezeke kama mchanga wa bahari. Njoo upate muujiza wako.
Wanafunzi mashuleni na vyuoni hamna haja ya kuteswa na walimu na maprof uchwara. Wala wazazi hamna haja ya kununua pepa feki kama walivyofanya magabacholi huko Ugabacholini hivi karibuni kiasi cha kuwa kivutio kwenye mtandao. Njooni kwangu nitawaombea mshinde mitihani yenu. Wazito vihiyo wanaotaka waonekane wasomi hamna haja ya kuhonga vyuo viwape shahada za dezo wala kuingizwa mkenge na vyuo feki vya ughaibuni. Njoo kwangu niwapige dua mpate shahada zenu kimiujiza.
Kwa vile ulimwengu wa sasa ni wa sayansi na teknolojia, huna haja ya kuja kanisani kwangu kutoa fedha. Wewe tumia M-pesa tu na fedha ikishaingia nipigie simu nianze kukuombea uondokane na matatizo yako. Wale wala rushwa na mafisadi wanaoogopwa kutolewa upepo na Takokuru, njoo kwangu nitawadhibiti Takokuru. Kama wameishapata habari zako za kukwepa kodi au kula rushwa nitakuombea dua wakusahau na wakikuona wakupende uendelee kupeta na kutesa. Wauza bwimbwi, hamja haja ya kutolewa upepo uwanja wa ndege. Njoo kwangu niwapige na dua ya kuwafumba macho hao mafisi wa uwanjani waliotajirika kishenzi kwa kuwatoa upepo. Lo! Kumbe muda umekwisha hivi!
Wajinga ndiyo waliwao. Nisipowala mimi mjanja wataliwa na matapeli uchwara na wajinga wenzao. This is a man eats man country of No Brainland.
Tumalizie na yetu uliye mbinguni kwa kizulu baba :
  Baba wethu osezulwini
 Maliphathwe ngobungcwele igama lakho.
 Umbuso wakho mawufike.
 Intando yakho mayenziwe emhlabeni njengasezulwini.
 Awusiphe namhla isinkwa sethu semihla ngemihla.
 Usithethelele izono zethu
 Njengoba nathi sibathethelela abasonayo.
 Ungasingenisi ekulingweni
 Kodwa usisindise kokubi.
Chanzo: Nipashe April 25, 2015.

2 comments:

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,ukweli umeniacha hoi maana hii dili kweli ni dili ya kutengeneza njuluku za kumwaga katika ulimwengu wa wajinga ndio waliwao!Hakikia ni ukweli mchungu sana na unatia hasira za kupindukia mpaka moya unapata majereha yasiyiopona,akili kushindwa kuelewa kwanini katika kaya za kiafrika vipofu,viziwi na mabubu ni wengi mno kiasi cha kukatisha tamaa.Mwalimu Mhango mpaka lini hali hii itaendelea?kwa nini na sisi tusiwe na ushujaa wa kuwachukulia hatua watu hawa kama walivyochukuwa wenzetu watu wa ulaya ushuja wa kuwarudisha ha wa watu wakabaki katika kiza la kanisa lao na kuwapa nuru na mwanganga wananchi wao wa Kaya?Je unajua sasa makanisa ya ulaya yamefilisika kuhudhuriwa na waumini hata wahubiri na hatimae wamewalenga wahubiri wa kaya zetu za ulimwengu wa tatu kuja kuhubiria waumini wachache waliobaki ambao wanahudhuria kanisa kama kujiliwaza kwa kupata utulivu wa kiroho na wala sio kuibiwa kama wanavyoibiwa waumini wa kaya zetu?

Nadhani ungewaongezea pia kwa kina mama watasa waje walale na wewe na sio kuwaobea na kwa nguvu ya Roho mtakatifu utawapa watoto na uwenda wengine wakawa wanalelewa na Roho mtakatifu mwenyewe wakjiunga na wewe baba mtu katika kuwakwapua mandondo hawa.Ukweli hali inatia huzuni lakini ndio ukweli uliopo ardhini.

NN Mhango said...

Anon sijakuchekesha wewe pekee hadi mimi mwenyewe nimejichekesha hasa niliposoma ujumbe wako. Kuna haja ya kuwaandama hawa jamaa ili kila mtu awaogope kama ukoma. Kwa ufupi ni kwamba kupitia ucheshi ukweli mchungu unatoka na wao wakisoma wanasonya hata kama hawatakuwa na la kufanya. Hao watasa natamani wawe vigori si vizee ili niwape dawa mujarabu.