Tuesday, 7 April 2015

Andamaneni kumshawishi Lowassa asigombee


          Baada ya baadhi ya wanasiasa kuanzisha “usanii” wa kuwanunua wale baadhi ya wanasiasa wamewaita wachovu na wachumia tumbo kujifanya wanaandamana kuwashawishi wagombee urais, nimeijiwa na wazo mbadala. Je wanaweza  kujitokeza wananchi wenye uchungu na nchi wakaandamana kwenda kwa wahusika kuwataka wasigombee kwa vile hawafai na kama wanafaa kwanini wasifuate utaratibu wa kawaida wa kutamka wenyewe bila kudengua kuwa wameshawishiwa wakati wanautaka urais kwa udi na uvumba?
Hivi karibuni, mbunge wa Monduli Edward Lowassa –waziri mkuu aliyelazimika kuachia ngazi tokana na kuhusishwa kwenye ya Richmond –alitoa mpya. Alionekana akiwa na makundi ya walioitwa “mashehe wa Bagamoyo” japo wenzao waliwakana. Baadaye, alionekana na kundi lililojiita wanafunzi wa vyuo vikuu. Wengi walishangaa wahusika walivyopatikana au kuchaguliwa kwenda kufanya kazi chafu na ya kuwadhalilisha ukiachia mbali kukiuka kanuni. Chama Cha Mapinduzi (CCM) –kuchelea madhara yanayoweza kukikumba kutokana na mchezo huu –kilipiga stopu sanaa hii ambayo nayo itashindwa muda si mrefu. Je kweli wahusika wanapendwa hivyo au ni “pochi” lao? Je wahusika –watumiaji na watumiwa –wanapendana au ni kutumiana tu? Je rais anayetokana na ghilba kama hii anaweza kulifaa taifa hasa wakati huu linapohiji mtu safi, mchapakazi, mzalendo ili alitoe kwenye uoza na udhalili lililomo?
Tunadhani kiongozi anayewatumia wenzake kufikia malengo fichi hatufai; hana sera wala ajenda kwa ajili ya taifa. Kama anaweza kuwatumia waroho wachache akafanikiwa, si atalitumia taifa kwa faida zake fichi? Wengi wanashangaa kwanini Lowassa anapoteza muda kuwanunua watu wa kujifanya wanamuunga mkono na kumtaka awe rais kujibu tuhuma lukuki za ufisadi na kujilimbikizia mali nyingi kinyume cha sheria na maadili ambazo zimemkabili kwa miaka mingi?
Wengi wangedhani: Lowassa angejisafisha bila kutumia mbinu ya kukusanya wachovu kuonyesha anapendwa ingeingia akilini zaidi. Je hawa wanaoonekana kwenye picha na Lowassa ni nani? Mbunge wa Bumbuli (CCM) Januari Makamba analo jibu kama alivyokaririwa na vyombo vya habari akisema, “Huu utaratibu wa kuratibu watu, kuwasafirisha, kuwapa posho na ubwabwa waje kukuomba kugombea ni michezo ya kuigiza ambayo ni aibu kubwa.” Makamba anamaanisha kuwa Lowassa aliwahonga na kuwanunua wahusika madai ambayo hayajakanusha.
Makamba aliongeza, “Ni aibu sana kutumia shida na njaa za watu kisiasa. Ni aibu sana kukusanya vijana na wazee wa watu na kuwapangia viti na mahema na kuwapa pesa na kuwapiga picha. Ukiona mtu anatafuta nafasi ya uongozi kwa ujanja na ulaghai, ujue atatawala kwa ujanja na ulaghai.” Makamba anamwonyesha mhusika kama mtu mlaghai asiyefaa kuwa rais ajaye wa Tanzania. Kwa vile Makamba ni mgombea aliyekwisha taja wazi –bila “kushawishiwa” kuwa angependa agombee urais, anaweza kuchukuliwa kama mshindani wa Lowassa. Je tukimpima Lowassa tunapata nini? Wengi wangependa kujua mantiki ya Lowassa –mfano –kuendelea kulipwa posho na marupurupu ya kustaafu uwaziri mkuu wakati hakufanya hivyo. Je huu si ulaghai ukiachia mbali kuwa uhujumu wa taifa? Inakuwaje huyu anayejifanya anapendwa na ana uchungu na taifa hakuona hili kuwa ni kulihujumu taifa? Nadhani hili ni kosa na kasoro kubwa inayotosha kufanya hata chama chake kisimpitishe. Lakini chama chake kitalionaje hili wakati ndicho kinachounda serikali tawala iliyoridhia wizi huu wa mchana wa fedha ya mlipa kodi?  Wapo wanajiuliza: Kwani lazima Lowassa; watanzania wengine wenye sifa na udhu wamekwisha? Kwanini Lowassa anakimbilia Ikulu badala ya kujisafisha? Tunakumbuka maneno ya baba wa taifa Marehemu Mwl Julius Nyerere kuwa tuwaogopeni wanaokimbilia ikulu. Kwani ikulu ni patakatifu pa patakatifu pasipohitaji kukaliwa na watu wachafu, walaghai na wasaka tonge.
Wengi wanashangaa anapopata jeuri Lowassa ya kutaka agombee urais wakati alipaswa kufunguliwa mashtaka kwa kulihujumu taifa kupitia kashfa ya Richmond? Ushahidi? Kitendo chake cha kujiuzulu ni ushahidi tosha kuwa alishiriki kikamilifu katika kulihujumu taifa. Je rais anayeweza kulihujumu taifa tena bila kuwa rais, akiwa rais atalifanya nini? Tieni akili ili baadaye msijejuta na kuchekwa kwa kushindwa kuyapima na kuyatathimini haya. Kwa ufupi, rais atokanaye na kushawishiwa na watu aliowanunua –kwa njaa zao kam alivyodai Makamba –hatufai kama taifa lililomo msambweni likitaka mtu safi na madhubuti wa kuliondoa kwenye uoza na uovu lilimo.
Wakati wa kumwambia Lowassa kuwa aache “maigizo’ kama alivyomtaka mwenzake umefika. Kwa vile ameishaambiwa na kuonywa na wenzake tena wanachama wa chama chake, basi tusisitize na kuongeza  hapo kwa kumtaka Lowassa aache dhihaka na matusi ya nguoni na kuwatumia watu wenye njaa kwa ajenda zake za kisiasa. Hata hivyo, inachekesha kidogo; ikizingatiwa kuwa Lowassa alitangaza nia zaidi ya mwaka uliopita. Sijui hawa “wanaomshawishi” agombee walikuwa wapi na wana mantiki gani wakati mhusika alishafanya hivyo muda mrefu kiasi cha kupewa hata adhabu na chama chake? Walikwina? Au ndiyo kujikanganya na usanii wenyewe anaosema Makamba?  Kam ainawezekana kuandamana kumshawishi Lowassa agombee basi inawezekana kufanya hivyo kumtaka asigombee. Je kwanini wananchi wasiandamane kumtaka Lowassa asigombee?
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 8, 2015.

No comments: