Tuesday, 14 April 2015

Viongozi wa kiroho waroho na matajiri wachunguzwe

  • Wolf in Sheep's Clothing
Wimbi la viongozi waroho wa kiroho kutokea kuwa matajiri wa kutisha inatia shaka.  Hali imefanya wengi kuona umuhimu wa serikali kuwachunguza hata kufuta misamaha ya kodi wanayopewa wakaitumia kujitajirisha binafsi. Haiwezekani mtu anayefanya kazi ya kuhubiri tu anunue helkopta kwa mfano kusiwe na namna. Wapo waliojitahidi kutetea uoza huu kwa kusema kuwa baadhi ya wahusika wanapata sadaka ipatayo shilingi za kitanzania zaidi ya milioni 500. Ukichunguza mali walizo nazo, matumizi, matanuzi na utapanyaji wao na muda ambapo walianza biashara yao hii ya uroho mtakatitu, hupati jibu wala hakuna uhusiano. Hata kama ingekuwa hivyo, kwanini watu wachache wawatumie wengi kitapeli na kujinufaisha huku wakifaidi misamaha ya kodi?
Wengi wanashangaa kusikia kuwa taasisi za kidini ziondolewa misamaha wasijue hii misamaha imetokana na serikali za ukoloni zilizokuwa zikitumia dini kama vyombo vyake vya upelelezi. Nadhani watanzania wanahitaji huduma bora kuliko dini. Je hawa wasio na dini za kimamboleo si wanaibiwa kwa kuruhusu misamaha isiyokuwa na sababu wala ulazima? Ni kipi cha mno hizi dini nyemelezi zinacho kustahiki kupewa misamaha ya kodi? Nadhani watanzania wanahitaji mkate kabla ya neno. Hivyo, kila anayefanya biashara au shughuli ziwe za kiroho au kutoa huduma lazima alipishwe kodi vilivyo.
Kuendelea kusamehe kodi madhehebu ya dini kumetengeneza matajiri wa kutisha wakati serikali na watanzania wakiendela kuwa maskini wa kutupwa. Wakati wengine wakimilki ndege binafsi na majumba ya kutisha, serikali yetu inashindwa kuendesha shirika lake la ndege. Watanzania wanaokamuliwa wanaendelea kuhangaika huku matapeli wachache walioruhusiwa kufanya jinai yao tokana na uzembe wa mamlaka wakiendelea kutesa. Siwezi kushangaa kukuta mabilionea wengi wa kidini wakiwa hata nyuma ya biashara haramu ya mihadarati ukiachia mbali kutumia misamaha ya kodi kufanya biashara nyuma ya pazia.
Kwanza, inashangaza wanaopata huu mfano wa kuwa matajiri wakati Yesu wanayedai kumhubiri alikuwa maskini wa kutupwa. Wanadhani kuwa kama Yesu angetaka utajiri angeshindwa kuupata? Lakini aliukataa kwa kuogopa kuwaibia wafuasi wake na watu wasio na hatia.
Inashangaza kuona na mamlaka zetu zinaendelea kufanya mambo kizamani na kwa mazoea. Huwezi kumwacha mtu anayetembelea ndege binafsi au magari ya bei mbaya kama Hummer na Humvee aishi bila kulipia kodi vitu hivyo. Hapa Kanada anapoishi mwandishi, ukinunua kitu cha starehe au kisicho cha lazima kama magari, mahekalu hata mavazi ya bei mbaya, unatozwa kodi kweli kweli ili kodi hiyo kupelekwa kwenye huduma za lazima za jamii kwa wananchi. Inashangaza serikali inayoombaomba inavyoweza kushuhudia matapeli wachache wakiwachuna watanzania na kutokea kuwa matajiri wa kutosha huku nchi yao ikiendelea kusuasua.
Pamoja na kushuku utajiri wa haraka tukiwasakama wauza unga, washirikina wanaoua mazeruzeru ili kupata utajiri wa haraka, tunapaswa kuwageukia wanaojiita viongozi wa kiroho ambao wanaonyesha kuwa viongozi wenye uroho na si viongozi wa kiroho. Inawezekanaje mtu alale kwenye jumba la mamilioni wakati wale anaowakamua wanatembea kwa miguu asiwe fisadi hata kama anajifanya kutangaza neno la Mungu? Kimsingi, hawa hawana tofauti na waganga wa kienyeji wanaowadhalilisha na kuwaibia watu wetu maskini na wajinga na washirikina ambao wanaamini kuwa matatizo yao yanaweza kutatuliwa kwa maombi na miujiza badala ya kujituma na kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa.
Ujinga kweli ni mzigo. Inakuwaje watu wanaodanganywa na matapeli kuwa wanaweza kuwaombea au kuwapa dawa ya utajiri wanawatakisha fedha wasijitendee hiyo miujiza na kupata hiyo fedha wanayotaka watoe?
Tunapaswa kujifunza kitu kimoja kuwa kwenye masuala ya fedha na uchumi hakuna kuaminiana wala kubebana kama ilivyo kwa mataifa ya kiafrika ambayo bado yanapoteza fedha nyingi kwa kusamehe kodi kwa madhehebu ya kidini na NGO ambazo mwisho wa siku hutumia vibaya fursa hii kwa wahusika kujitajirisha. Kama siyo ufisadi wa viongozi wetu wa juu, ni rahisi kupambana na waovu hawa. Kwani, kutokana na ulimbukeni na wakati mwingine ujinga wao, hawafichi hata huo utajiri wao. Wanafanya hivyo, ima kwa kujua wazi kuwa mfumo unaotawala una udhaifu au kwa vile wanakula na wakubwa.
Hatuwezi kuendelea na ujinga huu tukafika mbali kama taifa. Lazima kila mtanzania bila kujali cheo wala itikadi yake atangaze alivyopata utajiri wake. Lazima serikali zitoke usingizini ziwabane wananchi wote walipe kodi badala ya kuruhusu taifa kuwa shamba la bibi ambako matapeli wa nje na ndani hutumia na kujitajirisha huku watu wetu wakiendelea kuteseka na umaskini. Kama tutakuwa makini na wasioendekeza ujinga tukawa wakali vya kutosha, hatuna haja ya kwenda nje kujidhalilisha kuombaomba. Sijawahi kuona mchungaji au askofu au waziri hapa Kanada akiendeshe Hummer au kuwa na ndege yake binafsi asiandamwe akaeleza alivyopata utajiri wake.
Sheria ya Kanada inatamka wazi kuwa yeyote anayeishi kwenye nchi hii awe raia au mgeni lazima kila mwisho wa kazi ajaze fomu za marejesho ya kodi. Hili linafanyika kwa wakanada na wageni hata wafanyabiashara na madhehebu ya dini ili serikali kuweza kukadiria mapato na matumizi yake. Tanzania nani afanye hivyo wakati wakubwa ndiyo wanaongoza kukwepa kodi na kushirikiana na matapeli kuhujumu taifa?
Inatosha kuzitaka mamlaka za Tanzania kubadili mfumo na tabia zake dhidi ya madhehebu ya dini hasa haya ya kuzuka zuka na viongozi wake kujipachika vyeo vikubwa vila kuvisomea wala kustahili. Imetosha. Wote wenye ukwasi unaotia shaka wabanwe waeleze walivyoupata wakishindwa au kugunduliwa kuwa waliupata kwa kuwatapeli, kuwahadaa au kinyume cha sheria na utaratibu wafilisiwe.
Chanzo: Tanzania Daima April 15, 15.

2 comments:

Anonymous said...

Huu ni ukweli mchungu sana kuona matapeli hawa wa kiroho baada ya kuwahudumia kondoo wao imegeuka kondoo wao kuingizwa machinjioni kila siku.kwa upande mwingi wahenga walisema "wajinga ndio waliwao"hawa makondoo wanaokubali kupelekwa machinjioni kila siku kwa nini hawalioni hili kwamba wachungaji wao ni matapeli wa kiroho tu?Mbona matapeli hawa wa kiroho hawawajengei shule,zahanati,kuwachimbia visima au kwa lugha nyingine kuwahakikishia kwamba wanawahudumia kondoo wao.Mana hata wafugaji upeleka wanyama wao malishoni ili wafaidike nao zaidi sasa hawa matapeli wa kiroho mbona hawapeleki kondoo zao malishoni zaidi ya kuwakamua na kuwabana tu?
kwa upande mwingine ni wazi kabisa kwa utajiri wa hawa matapeli wa kidini kuna biashara nyingine wanaifanya nyuma ya pazia na hiyo inajulikana na serikali yetu na inawezekana hata baadhi ya viongozi wa serikali na matajiri mafisadi wanafaidika kupitia matapeli hawa wa kiroho kwa biashara hizo za haramu na ndio mana wanafumbia macho kwa maovu yao ya kiroho wanayofanya.
Mhango,kiongozi yoyote yule wa dini ambae dunia ameiweka mbele kuliko maisha ya mbinguni hawa ni mbweha tu amejivisha ngozi ya kondoo.waangalie viongozi wa dini ya kibudha wa kihindu walivo na wanavyoishi utakuta wana tofauti kubwa na hawa matapeli wetu wa kiroho wa ukiristo au uisilamu wamekuwa ni makupe wakubwa tu wasiobanduka katika miili ya wafuasi wao.

NN Mhango said...

Anon nakupongeza kwa mchango wako mkubwa ambao sitapenda kuuharibu kwa kuongeza maneno yangu. Ila nakubaliana nawe kuwa serikali imo kitandani na hawa washenzi na matapeli wawe wachungaji wahubiri wa mihadhara au mashehena.