Tuesday, 26 May 2015

Kijiwe chalaani ndoa ya dini na sias


          Hivi karibuni wanakijiwe walichukia nusu ya kuanza kuandamana hata kabla mkuu sijatoa ruhusa. Baada ya kushuhudia ndoa iliyofungwa baina ya viongozi wa kiroho na mafisadi ya kisiasa yanayokwenda kumwaga pesa eti kuyachangia, kimekaa kujadili aina hii ya ufisadi.
Mgosi Machungi ndiye mwanzilishi wa mada leo. Anakwayua mic na kusema, “Hivi mimeona jinsi mafisadi wanavyoingiia hata dini kiasi cha kutichanganya? Tinaambiwa dini na siasa havichanganyikani wakati wao wanavichanganya.”
“Hebu rudia. Eti wanaiingilia dini? Unamaanisha nini na wanaingiliaje dini na kupitia wapi?” Mbwamwitu anauliza huku akitabasamu.
Mgosi anamrushia gazeti na Mlevi lenye kichwa kisemacho, “Fisadi Afunika AR.”
“Kumbe unaongelea haya mauzauza ya chama twawala ya makamu wa Rahis kumtuma fisadi Eddie Luwasha amwakilishe kwenye kudhalilisha mahekalu ya God na kutoa hongo kwa viongozi waroho wa kiroho! Sasa nimekuelewa endelea.” anachomekea Kapende.
Kabla ya Mgosi kuendelea, Mpemba anakwanyua mic na kulalama ile mbaya, “Hivi kweli nyumba ya Subhanna yawezachangiwa na wenye dhambi hasa wezi, wauza unga na malaya wa kisiasa kama chama twawala? Wallahi kama waja wangefufuka, bila shaka Sayyidina Umar ibn Al-Khattab angechinja ntu hapa tena hadharani.”
 Mipawa anakubaliana na Mpemba, “Nyumba ya namna hii bila shaka itakuwa chafu na yenye wingi wa madhambi kiasi cha kutoweza kutoa msamaha wa dhambi.” Anapiga funda mbili tatu na kuendelea, “Hata dua zinazoombwa mle huwa hazifiki kwa mujibu wa sisi maulamaa. Ukisikia ukafiri ndiyo huu.”
Mzee Maneno anauliza swali, “Je hawa wanaochangia kuelekea uchaguzi walikuwa wapi?”
Msomi Mkatatamaa anaingia kwa usongo na kusiliba kwa sana tu, “Je hiyo fedha ni halali au ni ya unga, ujambazi na ufisadi? Ni jambo la hatari kwa wachovu kutegemea misaada badala ya kujengewa mazingira ya kujitegemea. Wawezesha wajenge makanisa na misikiti kwa fedha yao halali badala ya fedha chafu na ya fedheha. Kaya haiwezi kuendeshwa kichokoraa na ikawa kaya. Rahis anaombaomba, mashehena wanaombaomba, wachunaji nao kadhalika.”
“Msomi tafadhali usinilize mkanicheka. Huoni kila kitu kayani kinategemea michango na misaada ya kipumbavu tena ya wale wanaotuibia tukiona? Hata hao wanaojifanya kumwaga mabilioni wameyapata kwa kununuliwa na jamaa hawa hawa ambao ni maarufu kwa kuchangia kila kitu kuanzia michezo na kila kitu wakati wakikwepa kulipa kodi na kufanya biashara nyingi haramu. Nadhani mnawajua,” Anazoza Mheshimiwa Bwege huku akimkata jicho Kanji.
Kanji naye anakula mic, “Mimi kwisajua yote tasema hindi. Siyo hindi yote natoa ruswa au kwepa kodi au pewa samaha ya kodi dugu yangu. Hindi nyingine sikini ya Mungu kama veve dugu yangu.”
“Hayo wayasema wewe. Mimi sijataja mtu vinginevyo ajitaje mwenyewe. Ukiona anayelalamika jua yule yule.” Anazoza Mheshimiwa Bwege.
Mijjinga ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Kisesa anaamua kula mic kwa fosi, “Ukiona viongozi wa duni wanafunga ndoa na wanasiasa ujue hivi vitu vinachanganyikana. Ubaya ni pale wanasiasa watakapopata watakacho wakaanza kuwageuka wenzao wa dini kiasi cha kulete hali tete kayani.”
“Hawa wanatumiana tu hakuna mwenye mapenzi na mwenzake,” Mbwamwitu anarusha kimondo.
Sofia Lion aka Kanungaembe aliyekuwa kimya muda mrefu anaamua kunyaka mic, “Kanji huna haja ya kujitetea. Ni kuwadharau tu. Watasema  mchana usiku watalala huku mkiendelea kufaidi maisha bora kwa wote wenye kujibidisha. Halo halo!”
“Sofi acha kujichamba. Kama maisha ni kwa wote inakuwaje wewe hatuoni huo ubora zaidi ya kujigongagonga?” Mchunguliaji anaamua kumtolea uvivu Sofi.
Kapende anachomekea, “Mpe dozi yake hadi azimie.” Sofi anamkata jicho la hasira na kugeuka upande mwingine akisonya.
Mpemba anaamua kurejea kwa chati, “Mie wallahinaona huu licha ya kuwa wizi na ni ufisadi wa kisiasa unolenga kueneza ugaidi baadaye. Kwanini hawa wachanganya dini na siasa wakati watwamba sie tusifanye hivo?”
Mipawa anabuna mic, “Leo wamo kitanda kimoja wakiangusha vicheko. Baada ya kugeukana utayasikia wakitishia usalama wa kaya. Hawana maana hao wala ndoa ya kudumu nakwambia.”
Mgosi anaamua kukatua mic, “Waahi hawa mashehe na wachungaji wanaojiahisi kwa wanasiasa si mashehe wala wachungaji kitu bai mashehena na wachunaji. Wanachuna mabuzi ya kisiasa na kujaza matumbo yao ambayo ni shehena bila shaka.”
Mbwamwitu anampa tafu Mgosi,“Hii pwenti nimeikubali. Kweli, machangu wa kisiasa wanawahonga machangu wa kidini kwa uroho wao halafu wanajitia watu wa sir God. Mshindwe na mnyong’onyee mnaochangisha fedha chafu kujenga hekalu la baba yangu.”
Kapende anaronga tena, “Hivi kweli Kanisa au Msikiti unaweza kuchangiwa na mafisadi kama Ewassa kweli? Mbona mnatutia midole machoni na kututukana matusi ya nguoni?”
Msomi naye anarejea kwa chati, “Afunike asifunike lazima kwenye urahis afunikwe. Anapoteza muda wake hasa ikizingatiwa kuwa afya yake kimwili na kisiasa ni ugogoro mtupu. Nani anataka recycled rais kwenye ikulu akaibe na kujineemesha zaidi? Nani anataka rais mgonjwa ambaye atatumia muda na fedha nyingi kwenye matibabu? Hapa kuna haja ya kukpia afya za wanaotaka kugombea urahis.Hivi walioshindwa uwaziri mkubwa watauweza urahis kweli?”
Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita fisadi Luwasha mmoja. Wacha tumtoe mkuku!
Chanzo: Tanzania Daima Mei 27, 2015.

2 comments:

Anonymous said...

Sisi wanafunzi wa darasa la pili mwanzoni mwa miaka ya themanini, tunaweza kusema wale wapiganaji vijiji viwili pale wapiganaji wa kijiji kingine walipoelemewa na vita, waliamua kujificha chini ya manyasi...walipokanyagwa na jeshi pinzani. Mmoja wapo aligunia hivyo akafahmika wapi amejificha na mwingine akafuatia kwa kusema kwa sauti angali akiwa amejificha na nukuu Bora mimi sikusema....! naishia hapo.

Anonymous said...

Salaam Mwalimu Mhango,
Tukisoma historia ya uovu wa kanisa katoliki katika historia ya ulaya ya kuwanyanyasa waumini,wananchi,wasomi,wafalme na hata wapinzani wa kanisa hilo,tunafika katika karne ya 15 tunakuta kwamba wanachi wa ulaya wakiongozwa na wasomi wa bara hilo na wapinzani wa kanisa hilo wanalitolea uvivu na kulitoa kanisa kujiingiza katika mambo ya dola na siasa na hatimae Bara la ulaya likachomoka kwa kasi kubwa sana kuelekea katika maendeleo ya kielimu,kijamii,kisiasa na kiuchumi kwa kutumia uhuru wa kufikiri na sayansi na teknolojia hadi hii leo.Naam,kanisa lilitupiliwa mbali na athari yake ikabaki kanisani tu na nje ya kanisa wakajishugulisha na huduma za kijamii si zaidi wala pungufu.Lakini makanisa hayo yalipoingia katika ulimwengu wa tatu yakarudia tabia yake ile ile ya kujiingiza katika mambo ya dola na siasa baada ya nchi hizo za ulimwengu wa tatu kutoka ktika mikono ya wakoloni.

Mwalimu Mhango,kama unavyojua,kwa kuisoma historia ya watawala wa kiislamu katika nchi za kiisilamu na viongozi wao wa kidini,unakuta ndoa hii ya dini na siasa imefanikiwa sana na kutia fora,kwa viongozi wa nchi hizo kuwatumia viongozi wa kidini kila kukicha na viongozi hao wa kidini kuwa tayari kutoa huduma zao za kuwatetea viongozi hao hata kama ni madikiteta,mafisadi na wakandamizaji wa wananchi na hafanya hivyo hata kwa kupindisha maandishi takatifu ya Bwana Mungu tumeona matetezi ya viongozi hao wa kidini wa nchi hizo wakiwatetea akina Sadati,Mubaraka,Ghadafi,Saddam,Assad baba na mtoto na wafalme wote wa nchi hizo za kiisilamu(kiarabu)pamoja na viongozi hao wa nchi hizo kupata upinzani mkubwa wa Muslim Brotherhood lakini viongozi hao wa kidini walibaki kuikumbatia ndoa yao na wanasiasa wao.Tofauti ya kuizingatia kati yetu sisi na wao ni kwamba wengi wa wananchi wao ni wa dini hiyo hiyo ya kiisilamu kwa hiyo unakuwa ni mchezo waTom na Jerry tu.Lakini kwetu sisi ambao tuna dini tofauti swala la ndoa ya dini na siasa ni jambo ambalo halistahiki kupewa nafasi kwa aina moja au nyingine.

Mwalimu Mhango,unakumbuka vizuri sana Mwalimu Nyerere alivyotumia wakati wake katika kupambana na janga hili.Hakutoa nafasi kabisa ya kusogeleana kati ya dini na siasa mpaka kufikia kufunga ndoa kama tunavyoona hivi sasa.Na kwa vile wananchi wetu wamekuwa ni walevi wa dini wanasiasa wamejua wapi pa kuingilia ili waweze kufanikiwa kile ambacho wanachokitaka nacho ni kufika madrakani kwa kila njia kufa kwa Mwalimu Nyerere ndio wamepata nafasi ya kuanzisha ndoa hiyo ya dini na siasa kwa kwa viongozi wa dini ni nafasi yao ya kupata ulaji kwa pande zote mbili.Lakini kwetu sisi ndoa hii inatupeleka pabaya kwa kuhatarisha amani,usalama na umoja wa nchi hata kama wanasiasa wanadhani wanaweza kuikabili hali hiyo,kwani kura zitazopigwa kwa kupitia mstari wa dini moja au nyingine au dhebu moja au jingine ni hatari sana na hawa wana dini kuingilia katika siasa kwa kuwahimiza waumini wao wapige kura kwa kumchaguwa wanaompendekeza wao ni janga la kitaifa.Namalizia kwa kukuuliza Mwalimu Mhango kwa nini wakati wa Mwalimu Nyerere hali hii haikuwepo na viongozi wa dini zote walibaki makanisani mwao na misikitini mwao?Dini ni swala la mtu binafsi yeye na anachokiabudu hata kama anaabudu jiwe ndiyo dini yake lakini nchi ni ya wote bila ya kujali dini au itikadi ya mtu.Tafadhalini wanasiasa na viongozi wa dini imefika wakati wa kuivunja ndoa hiyo kwa usalama,amani na umoja wa taifa.Hatutaki itufikie hali kama ya Afrika ya Kati,Iraq,Syria,Boko Haramu,Al Shabaab na leo hii Yemen Bwana Mungu apishie mbali na atulinde,