Monday, 25 May 2015

Wabunge mabubu wasirejeshwe bungeni


Hivi karibuni vyombo vya habari vimetoa ripoti ya uchangiaji wa hoja bungeni kwa wabunge. Kwa ujumla wabunge wa upinzani wameonyesha kutoa michango mingi tofauti na wale wa chama tawala. Inashangaza kuona mwakilishi wa wananchi anakaa bungeni kwa miaka mitano bila kutoa mchongo wowote wala kuuliza swali au kuuliza maswali machache kana kwamba huko atokako hakuna matatizo. Je wabunge wa namna hii mabubu wanafaa kurejeshwa tena bungeni wakati hawana cha kufanya kule zaidi ya kupata posho kwa kukaa kimya bungeni? Je wananchi wanapomchagua mtu awawakilishe anakwenda kule kuwa sanamu au chachu ya maendeleo kupitia hoja na michango yake?
          Katika makala hii hatutataja majina ya wabunge waliotajwa ima kwa kuchangia sana au kutofanya hivyo kabisa. Cha msingi, ni kuwataka wapiga kura wawapime wabunge wao wa sasa kutokana na kazi zao bungeni na majimboni. Kama mnagundua kuwa kumbe mliyemchagua awawakilishe aliwakilisha tumbo lake kwa kuvuta posho basi msimrejeshe. Maana kufanya hivyo kutawachelewesha wakati wenzenu wakipaa.
          Kwa wanaojua mantiki ya kuwa na bunge ili kuwakilisha mawazo ya watawaliwa, bungeni si sehemu ya kulala, kukaa kimya au kuvuta posho. Bungeni ni uwanja wa vita ya kuwakilisha mawazo na matatizo ya unaowawakilisha. Ni uwanja wa vita ya maendeleo hoja na michango mbalimbali. Ndiyo maana wabunge wamepewa uhuru kikatiba kuongelea jambo lolote bila kuchelea kufikishwa mahakamani.
          Hata hivyo, kuna haja ya kudurusu ni kwanini wabunge wengi hawachangii bungeni. Wapo wanaolala kutokana na kutoiweza kazi ima kwa ugonjwa, uzee hata kutokuwa na sifa za kuwasemea wenzao. Wengine ni watoro tu kama alivyobainisha spika wa bunge hivi karibuni aliyekaririwa akisema, “Kuna wabunge wanatoka na kusafiri bila ruhusa, hivi mkipata ajali huko mtasemaje?”  Ni bahati mbaya spika hakutaja wanakopenda kusafiri. Hata hivyo, inakuwaje mbunge aage jimboni mwaka anakwenda bungeni aishie kupanga safari nyingine?
          Wananchi hasa wapiga kura wanapaswa kutatua tatizo la wabunge watoro na mabubu kwa vile wanawafahamu. Wengi wanaweza kutochangia hata kutoroka bungeni bila woga na badala yake wakahangaika na kutafuta fedha ya kuhonga wapiga kura ukifika wakati wa uchaguzi. Wananchi wanapaswa kukataa kununuliwa na kuishia kuwa wahanga wa jinai hii. Wakija na fedha walizozipata kwa kutumia ubunge na kutumia muda wa bunge kufanya biashara kuleni na wanyimeni kura hasa ikizingatiwa kura ni siri. Vinginevyo, majimbo yanayoongoza kuwa na wabunge mabubu wasilaumu mabubu hawa watakaposababisha waachwe nyuma kimaendeleo. Mbunge ni mshenga wa wananchi kwa serikali.   Hpaswi kuwa bubu au kwenda kuupiga usingizi bungeni kama ambavyo wengi wamewahi kupigwa picha wakiuchapa usingizi bungeni utadhani bungeni ni nyumba ya kulala wageni. Hawa wanaopenda kulala kama vichanga wasipewe kura ili wakalale vizuri majumbani mwao badala ya kuangusha wananchi waliowaamini na kuwapa dhamana ya kuwawakilisha wakaifuja.
          Nadhani kitu kingine kinachowapa wabunge mabubu motisha na kiburi ni ile hali ya kuawa katiba kielelezo iliyokuwa na vipengele vilivyotaka wananchi wawawajibishe wabunge bila kungoja ukomo wa vipindi vyao. Laiti wananchi wangejua kuwa vipengele hivi vililenga kuwakomboa wasingeruhusu kikundi cha watu kuua katiba hii ya ukombozi na kupandikiziwa ya kifisadi wanayoshawishiwa waipigie kura wakati haina maslahi kwao bali kwa kikundi cha walaji wachache.
          Kimsingi, wabunge mabubu ni zao la mfumo mbovu wa utawala uliojikita nchini ambapo mtu akishapata cheo anakigeuza kuwa mali binafsi badala kuwa dhamana. Mtu wa namna hii haogopi chochote kwa vile anajua wale waliofanya kosa wakampa dhamana hawana ubavu wa kumtimua. Hivyo, sehemu nzuri ya kutimua wabunge mabubu ni kwenye sanduku la kura. Nadhani sababu ya wabunge wengi tena wa chama tawala kutochangia ni ile hali ya kujiamini kuwa chama chao kikiwapitisha kitafanya mambo wapiti kama ilivyotokea kwenye uchaguzi uliopita hata kama wapiga kura watakuwa wamewakataa. Hii maana yake ni kwamba wananchi wanapoamini kuwa aliyepitishwa siyo waliyemchagua basi wamgomee asiapishwe kuwawakilisha. Wananchi wanajua mengi. Wanawajua wabunge waliopandikizwa na chama baada ya kushindwa kwenye sanduku ya kura. Wanajua jinsi wabunge wengi wa chama tawala wapo bungeni kutokana na jinai ya uchakachuaji iliyofanyika kwenye uchaguzi uliopita. Mwaka huu wasiruhusu upuuzi huu kuendelea kuwahujumu wakiachwa nyuma kimaendeleo. Hivyo, uchaguzi ujao uwe ni uwanja wa kuwauliza wabunge wao walichofanya cha maana kwa muda waliokaa bungeni wakipiga usingizi, kutoroka na kugeuka mabubu huku wakivuta posho bila stahiki. 
          Hata bila kuandikwa magazetini, wabunge mabubu na vilaza wanafahamika. Kadhalika wabunge machachari na wahangaikaji wanajulikana. Wabunge wanaokwenda bungeni kupiga dili kama wale walioshutumiwa kuomba rushwa serikali za mitaa ili kupitisha mahesabu yao wanafahamika kwa sura na majina. Wahalifu kama hawa hawapaswi kurejeshwa bungeni. Na hii ikifanyika, itatoa onyo na somo kwa wengine wanaopanga kwenda bungeni kuchapa usingizi au kupiga madili.
          Tumalizie kwa kuhitimisha kuwa wabunge mabubu na wavivu wa kujenga, kutoa hoja na kuuliza maswali hawapaswi kurejeshwa kwenye bunge kwenye uchaguzi ujao. Watakaowarejesha wajilaumu badala ya kulaumu wale waliowachagua wakijua hawafai hata kuwa wawakilishi wa nyumba kumi.
Chanzo: Dira.

No comments: