Friday, 15 May 2015

Mlevi alazwa kwa mstuko wa usafi wa escrow

 
          Baada ya kuzinyaka kuwa watuhumiwa wakuu na wengine mizigo kusafishwa na wenzao, nilipatwa na shambulio la moyo kiasi cha kukikimbizwa hospitalini ambako niliishia kumuona daktari na kuwekewa drip za maji na kuamriwa kurejea home.
Kama si kurejea home na kupata kanywaji na bangi huenda sasa ningekuwa past tense. Maana nilivyostuka sina mfano. Hivi nani hapa anamdanganya nani? Ajabu na walevi nao wamepokea sanaa hizi kwa upole na vicheko utadhani hawatalizwa zaidi kwa kutengenezewa mi-escrow mingine tena mikubwa kuliko huu wa akina Rugemalayer, Singasinga na Njaa Kaya. Hapa lazima tuseme ukweli kuwa wahusika waliowasafisha wenzao huenda wameogopa kumwagiwa mtama wao na kuishia kuumbuka. Hata hivyo, wajue. Kuna siku tutachenchiana kiasi cha kuchimbika bila jembe. Kuna siku patakuwa hapatoshi hasa baada ya kugeuza kaya shamba la bibi. Heri kufa kuliko kuendelea na upuuzi ambapo mipapa inaibia kaya na kusafishana huku walevi wakizidi kunukishwa na kuchafuliwa na ukapa na umaskini. To be open and frank, I don’t subscribe to these sanaaz za kusafishana.  Kama jamaa hawa ni safi na si mizigo basi ni uongo wa aina yake sawa na kusema kuwa mamba hana meno. Kama wezi ni safi, kwanini wasafishwe na wenzao badala ya pilato? Wapelekeni kwa pilato walale lupango ushahidi utolewe uone kama hawatanyea debe.
Kwa lugha rahisi, escrow si wizi bali ujasiriamali ambapo walio nyuma yake ni mashujaa wa kustahiki kupewa nishani za kuendeleza kaya. Mnamgeuza nani bwege hapa? Tubuni kabla ya kiama chenu kufika hasa pale nitakapowahamasisha walevi kuwavamia popote mlipo na kuwapondaponda na michupa ya gongo kabla ya kuwachoma kwa misokoto ya bangi. Huu nao eti unaitwa utawala wa sheria wakati ni wizi wa mchana.
Kaya yetu imegeuka ya vibaka, mibaka na majambazi. Mchovu akiiba kuku anafungwa maisha wakati mibaka ikibaka mabilioni ya escrow inasafishwa! Kibaka akibakua kidani anachomwa moto wakati mipapa ikichoma mafuta kwenda Ulaya kujaza akaunti zao ughaibuni.
Kinachokera ni pale mibaka hii mijambazi kuita mabilioni vijisenti au hela ya ugolo wakati tunanyotolewa roho na ukapa wa kutentenezwa na wana hizaya hawa waja laana wakubwa. Mshindwe na kunyong’onyea.
Wajua? Nilipopatwa na shambulio na moyo bi mkubwa alinicheka baada ya kupata nafuu baada ya kupata msokoto na mchupa wa gongo. Guess what. Alinishangaa kwa kutegemea nguruwe aone uchafu wa ngiri au ngamia amcheke nundu ng’ombe.  Kusema nilijiona bwege kama wachovu na walevi waliogeuzwa mabwege wakabwegeka kweli kweli wasikengeuke wala kujivuvumua hasa wakati huu wanapoliwa mchana kweupe bila kuona hata aibu ukiachia mbali kuhisi uchungu.
Hakuna waliponiacha hoi wahalifu hawa kama kudharau mjengo uliowa tia hatiani wahusika kiasi cha kuamuru watimliwe.  Ina maana waheshimiwa waishiwa ni waongo na wambea wakubwa wanaowanea wenzao wivu tena wivu wenyewe wa kiume? Tell me please. Je mama kipaza sauti binti Microphone wa kucheza makidamakida anageuka mamba awararue hawa ngiri na nguruwe au naye atanywea baada ya kupozwa na chochote kitu? Je waishiwa wanaokabiliwa na kibarua cha kurejea kwa wapika kula ya kura nao watajinasua na kashfa hii ya kuwadhalilisha na kuwaonyesha waongo vipi? I am still waiting to see. Ama kweli ukishangaa ya escrow utaona ya Sefui! Yaani baba zima linaamka na kusimama na kutangaza bila aibu kuwa nguruwe ni kiumbe msafi kuliko sungura na njiwa!
Go tell it to the bird Sifui hata kama unawafua wachafu wenzio.  Hapa hakuna cha usafi bali usafishanaji ambapo mmesafishana kwa vile wote ni wachafu na mmenufaika na wizi huu. Hata ndege hawezi kuamini "ukweli" huu kuwa wahusika ni watu safi. Je kama ni safi kwanini mliwafukuza kama hakuna kitu kimefichwa au kufanyiwa uchakachuaji ili kulindana na kuepuka kuumbuana? Sijui kama waziri tena Muongo aliyedaiwa kubeba mabunda ya fedha kwenye magaunia kweli ni safi. Hapa nadhani tunachopaswa kujiuliza ni: Je alipopakia mabulungutu ya njuluku kwenye mabox na magunia alikwenda kugawana na nani au alitumwa na nani kama si wanene wote? Je huyo Ngurumisha wa ikuu naye ni safi wakati ushahidi uko wazi kuwa alikatiwa akalegea?
Je inakuwaje ikuu ijifanye mahakama wakati kuna mahakama tena tunazoambiwa ni huru wakati kilichofanyika ni kuziingilia na kuzinajisi kiasi cha usafi, integrity and impartiality vyake kuwa kwenye shaka? Haiwezekani hata kama nafikiri kilevi mtuhumiwa huyo huyo awe mshitakiwa, mwendesha mashitaka na hakimu haki ikatendeka. Wahusika ni sehemu ya utawala. Kwanini utawala huo huo uwe ndiyo umechunguza na kutoa hukumu kama si kulindana? Wangejua nina PhD katika sheria, criminology and penology, investigation, constitution, na madude mengine mwengi wasingefanya waliyofanya.
Ukiachia mbali Muongo, hakuna waliponiacha hoi kama kumsafisha hata A Liar Kim Maswiswi. Nadhani wafanye haraka wawasafishe na akina Rugemalayer na Singasinga hata Annae Kajuamlo Tiba-Ijuka haraka sana.
Hebu tuwe wakweli kidogo japo kwa nukta moja. Hivi kweli akina Emmy Nchimvi aliyegushi shahada ya uzamivu si mizigo kweli? Mbona madai ya umizigo wao yalitolewa na wazee wa chata akina Andaraman Kinamna na Nipe Mapepe Ninaye? Ina maana hawa vigogo wa chata na chata lao ni waongo wa kutupwa? Je hapa mkweli ni nani kati ya watuhumiwa wanaowasafisha watuhumiwa wenzao na wabwabwajaji wa chata? Hapa kweli ni kasheshe tena kasheshe kweli kweli! Yaani tumejirahisi na kuamua kugeuza kaya chaka la majambazi kirahisi hivi! Ama kweli alijisemea mzee Mchonga kuwa ikuu imegeuzwa kuwa genge la wezi. Msinichukie wala kunichukulia mihatua. Haya si maneno yangu. Ni maneno ya Mchonga mwenyewe. Nani kama Mchonga ajitokeze tumuone na kumzodoa.
Ama kweli kama wahusika wamesafishwa basi wamesafishwa kwa majitaka. They are still stinkingly dirty and guilty.
Tuonane wiki ijayo wapendwani.
Chanzo; Nipashe Mei 16, 2015.

3 comments:

Anonymous said...

nani mchafu anamsafisha mchafu nani wanamahesabu hasi ukijulimsha hasi Jawabu ni....! Au tuite Hiyo ndiyo hadithi hadithi yenyewe, utaumu.......!

NN Mhango said...

Sefue anayewakilisha serikali chafu inayotaka kuwasafisha wachafu wenzake ndiyo walengwa. Kimsingi, hili dili ni la Kikwete mwenyewe anayepaswa kusafishwa kwenye tanuri kule Segerea. Kisheria, anayepaswa kumsafisha mtuhumiwa ni mahakama na si ikulu. Iweje wachafu wanaohitaji utakaso wawatakase wachafu wenzo wakati wote wanahitaji utakaso

Anonymous said...

Salaam Mwalimu Mhango,
Ningesoma habari hii ya neno kusafishwa kwa maana ya kumtoa mtu mchafu sehemu ambayo alipofanya machafu yake ingekuwa ni furaha kubwa kuona kwamba serikali tunayo ambayo inaamka wakati wa karibu na uchaguzi kwa kutuziba macho na midomo.Lakini kusafishwa kwa watu hao na ikulu yetu ambayo imegeuka si takatifu tena ili hali bado wanaendelea kunuka hata ukiziba pua na mdomo bado utasikia uvundo tu, hizi sio habari njema kabisa.Swali linalojiuliza lenyewe hapa ni kwamba je nani anamsafisha nani,ikiwa wote wapo katika pipa linalonuka?kuna hali ambayo kila siku inazidi kuijjenga katika akili yangu kwamba hawa tunaowaita viongozi wetu wanaijua sana saikolojia ya wananchi wao kwamba ni watu wa kuwaburuza tu kwa njia zote ambazo zinazostahiki kuwaburuza wananchi hao ni wananchi mabwege ambao wanakubali kudanganyika mchana kweupe.Iweje leo nchi iwe ina sheria na kanununi ambazo zinabaki katika makaratasi tu?Viongozi hawa wanajua kwa uhakika kabisa kwamba nchi ni miliki yao,sheria zipo mikononi mwao na madaraka ni mali yao binafsi.
Mwalimu Mhango,hali halisi kwa jinsi inavyoendelea tangu kuingia kwa awamu ya pili inanifanya kuwa na mshaka hata kwa hivi vyama vya upinzani tulivyokuwa navyo nimefikia kuamini kwamba na wao wanayanyemelea madaraka wakiyapata tu hali hii itaendelea kubaki pale pale sina uhakika kabisa kwamba upinzani utapofika madrakani watakuwa na uwezo wa kumuwajibisha kiongozi yoyote yule wa CCM aliefuja madaraka kwa kutumia ofisi vibaya, na kutumia vibaya mali na rasilimali za nchi.Je Mwalimu muhango,unadhan itakuja siku wasimamishwe mahakamani viongozi wa awamu ya pili mpka ya nne kwamba wameizamisha nchi na kujitajirisha wao wenyewe na familia zao?Je unadhani itafika siku kwamba mikataba yote mibovu iliyosainiwa na CCM itarudiwa upya na hata kubatilishwa?Je unadhani kuna siku pesa zetu mabilioni ya mashilingi ambazo leo hii zinaitwa ni za ugoro na vijisenti tu tutarudishiwa wenyewe?
Mwalimu Mhango,si kwamba mimi nimekata tamaa lakini naona viongozi wetu waliopo madarakani na wa upinzani wote ni sawa na sarafu moja tu japo ina nembo tafouti katika sura ya sarafu hiyo lakini itabakia ni sarafu ile ile tu hakuna mabadiliko.Mabadiliko ni lazima yasimamiwe na wananchi wenyewe kwa kusuka au kunyoa lakini je viongozi wetu wana hofu na wananchi hao kwamba itafika siku moja watawageukia tu?Nina mashaka na hilo kwani viongozi hao wanalala usingizi mnono na ndoto kubwa za kuzidi kujitajirisha na bila ya kuwa na hofu yoyote na wananchi wao.
Natamani kama neno kusafisha lingetumika katika maana ya kuwaondoa wachafu wote wa kaya kuliko kutumika kuwarudishia heshima yao ya uongozi na kisiasa ili wazidi kulindana wenyewe kwa wenyewe na kuendelea kupeana vyeo wenyewe kwa wenyewe siku za usoni na watoto wao na kuzidi kutukandamiza, kutudharau na kututesa kwa umasikini,ujinga na maradhi.