Wednesday, 20 May 2015

Kikwete anapouuza twiga akaahidi kutunza mbwamwitu!

  • Kikwete officiates the release of second pack of 15 wild dogs ...
  • Hotel Strand-Café Lang in Langenargen am Bodensee
 
Rais Jakaya Kikwete ni mtu asiyeishiwa vituko. Wakati mwingine akiongea –licha ya kujipinga hata kujipiga kijembe –wenye kuchambua mambo hushangaa kama anasoma hizo hotuba anazoandaliwa kabla au kusema baadhi ya mambo akiwa anajua uhalisia wake. Maana mambo mwengine anayosema yanamsuta na kumuacha akionekana tatanishi kwa umma unaoyapokea. Hivi karibuni Kikwete aliwaacha wengi hoi aliposema, “Kazi niliyoamua kufanya sasa na baada ya kuacha urais ni kusaidia uhifadhi.”  Kwanini baada ya kustaafu na si wakati akiwa madarakani? Nadhani kama rais alikuwa na nia njema na mali na raslimali za taifa wakiwamo wanyama, angetumia rungu lake kama rais kupambana na ujangili ambao unatishia kufuta baadhi ya wanyama wetu kwenye ramani ya nchi na ya dunia.
Vituko na maneno ya Kikwete yanatukumbusha aliposema kuwa wanafunzi wa kike wanaopoachikwa mimba na vishoka ambao hawashughulikiwi wanaponzwa na kiherehere chao wakati umaskini na ufisadi uliotengenezwa na watawala kama yeye una mchango mkubwa pamoja na sababu nyingine. Je halijui hili au hajajulishwa? Je alionaje kuwa ni kiherehere tu na si umaskini, ugumu wa maisha, ukosefu wa huduma kama vile usafiri kwa wanafunzi, walimu wa kutosha na kutamalaki kwa rushwa ya ngono pamoja na mambo mengine? Je hivyo navyo ni kiherehere au waliovisababisha nao wana kiherehere?
Kikwete aliahidi kutumia muda wake wa ustaafu kuwatunza mbwamwitu. Wengi walidhani –kwa vile wanyama kama Tembo na Faru ndiyo wanakaribia kumalizwa –lau angeanza na hawa ingawa nalo laweza kuwa siasa tu majukwaani kutokana na ukweli kuwa  hakuwalinda vilivyo wanyama hawa wakati akiwa madarakani sawa na alivyofanya kwa vitu vingine kama mikataba ya uwekezaji aliyoahidi angeiweka wazi na kuifumua na kuisuka upya asifanye hivyo. Hata hivyo, wanaomfahamu Kikwete kama mtu mwenye kupenda kusema maneno mengi ya kufurahisha na kutoa ahadi kemkem asitekeleze hata moja hawamchukulii seriously. Yako wapi maisha bora kwa wote aliyoahidi akiingia madarakani au nayo atayashughulikia baada ya kustaafu? Inashangaza mantiki ya Kikwete kuona mbwamwitu ndiyo wa kutunzwa wakati tishio la kutoweka kwao wala thamani yao havilingani na la twinga na faru. Ni ajabu kuwa na uchungu na mbwamwitu ukaachia wanyama walio kwenye hatari ya kutoweka kama tajwa hapo juu watoweke.
  Kama wanyamapori wameteketezwa hadi kuuzwa nje wakiwa hai na hakufanya lolote atajitosa kufanya nini na kwanini sasa baada ya wanyama wenyewe kutishia kutoweka? Ina maana Kikwete amesahau mkasa uliotokea chini ya uangalizi wake na asichukue hatua hapo Novemba 26, 2010 ambapo wanyama wapatao 150 wakiwamo twiga hai walisafirishiwa kwa dege la kijeshi kwenda Qatar? Je alifunga wangapi ukiachia mbali serikali yake kujenga mazingira yaliyomwezesha mtuhumiwa toka Pakistan kutoroka kwa hofu ya kuwaumbua wakubwa waliokuwa nyuma ya ufisadi huu wa kishenzi na kutisha? Kwa mtu mwenye uchungu na raslimali za nchi tukio kama hili lingeonyesha uchungu na ukali wake dhidi ya jinai hii, lakini wapi. Kwanini kufanya hivyo baada ya kustaafu ambapo hatakuwa na madaraka na kushindwa kuwatunza alipokuwa na madaraka?
Kikwete alikaririwa akisema, “Ni aibu wanyama hawa muhimu kwa utalii kutoweka kisha baadaye tuwatafute kwa gharama kubwa… Mimi niko tayari kusaidia wanyama hawa wasipotee.”  Je hao wanyama waliosafirishwa kwenda Qatar wakiwa hai hapo mnamo tarehe hawakuwa wanyama? Kama ni aibu basi mwenye kuistahili na aliyeilete si mwingine ni Kikwete ambaye serikali yake ilishiriki kikamilifu kuwatorosha wanyama huku katibu wa wizara wa wakati ule aliyetuhumiwa moja kwa moja kusuka na kutekeleza uhujumu huu akiteuliwa balozi kwenye nchi moja jirani. Kama Kikwete ana uchungu na wanyama kama anavyotaka aonekane, ilikuwaje akampandisha cheo mtu mwenye kushutumiwa ambaye ukiachia hilo alipaswa amwajibishwe kwa sababu wizara yake ilishindwa majukumu yake kiasi cha kuruhusu wanyama hai wasafirishwe tena kupitia kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Je serikali ya Kikwete inaweza kukwepa lawama kwa hili iwapo hata walinzi wa uwanja wa ndege hawakuwa na uwezo wa kuzuia hao wanyama kutosafirishwa kwa vile ulikuwa ni mzigo wa wakubwa? Je hapa Kikwete ana tofauti na rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye chini ya utawala wake mbuga maarufu ya Loliondo iliuzwa kwa waarabu hao hao kutoka Ghuba? Je huku si kukumbuka blanketi asubuhi kama siyo porojo za kisiasa?
Tumalizie kwa kumshauri Kikwete aache kututia vidole machoni na kutudhihaki kuwa atatunza wanyama wakati serikali yake ilihalalisha ujangili kiasi cha kutisha.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 20, 2015.

4 comments:

Anonymous said...

Salaam,Mwalimu Mhango,
Imenibainikiwa wazi kwamba kwa nchi yetu kumbe uongozi ni kama ulaibu wa pombe ya mnazi,komba atavyonza na kumaliza mzinga na akimaliza ucheza, husinzia,ulala na hata kuanguka wakati mwingi uanguka na bado anaamini kwamba mzinga ni wake kuliko mgema mwenyewe na katika hali hiyo usema chochote kile bila kujali kama atamkasirisha mgema au hapana na hata kama atamkasirisha mgema yeye anajua mzinga ni wake tu.Sasa ebu mwangalie huyu kikwete,mwanzo alisema atajikita katika kilimo mara hii kasema atajishughulisha na utunzanji wa wanyama,sasa kama si ulaibu wa pombe ya mnanzi ni nini?kwa nini alipokuwa madarakani asiyethabitihe hayo kwa vitendo?Kama ulivyofafanua katika makala hii?Wanaongea wasiyoyafana na wanayafanya wasiyoyaongea kwani wanajua tena kwamba watabaki tu kuwa hawana umuhimu wa kitaifa wala kimataifa zaidi ya kuitwa Rais mstaafu wakiendelea kutubeza kwa kula mafao yao ambayo huwa najiuliza kwani wameifanyia nini nchi hii mpaka wawe wanastahiki mafao hayo ya kutisha mpaka kifo chao?Na wakati walipokuwa madarakani ufisadi na wizi ndio ilikuwa sera yao ya utawala?Eh kumbe kikwete amefikia hata kusema kwamba watoto wa kike kupachikwa mimba ni KIHERERHERE chao?!!!Hivi je kama huyo ni mtoto wa kike ni wa kwake atakuwa kweli na ushujaa wa kumwambia kwamba ni KIHEREHERE chako?Ni kweli hapa ile methali ya kwamba aliyekuwa juu amuoni aliyekuwa chini ndiyo anayoifuata kiongozi huyu katika hili,Je kama si kulewa ulaibu wa pombe ya mnazi ni nini mpaka Rais wa nchi kuwa mwenye kutojali na kutofikiria kwamba maneno yake yatapokewa vipi na wasikilizaji wake je kwa nini asilipiganie na hili akistaafu urais kwamba kwa kuwalinda na kuwatetea watoto wa kike wenye KIHEREHERE cha kupachikwa mimba?Mwalimu Mhango,ebu tukubaliane nae kwa hoja ya mjadala kwamba anachongea hajalewa pombe ya mnanzi na ni mkweli kwa hayo anayoropoka,je hizo pesa za kupigania hayo anayoropoka zitatokea wapi?Zitatoka katika mfuko wake au tutaibiwa tena wananchi kwa kodi zetu kwa kufungua taasisi ya Rais mstaafu ya kulinda wananyama na ukulima?Tunajua wazi kwamba baadhi ya viongozi wa nchi zilizoendelea na hususa Marekani na matajiri wao huwa wanafungua taasisi zao kwa kuyapigania yale ambayo hawakuweza kuyapigania walipokuwa madarakani,sasa iwapo kama Rais kikwete atakuwa mkweli na pesa itatoka mfukoni mwake ya kufanya hayo anayoropoka na sio kutuibia wananchi kwa njia moja au nyingine,Mwalimu Mhango, udhani kwamba anastahiki pongezi na kuungwa mkono japo alifeli kutumia rungu lake alipokuwa madarakani?Wache tumpe nafasi ya kufanya hivyo kwani uwenda atatoa ajira kwa wananchi wake na kufanikiwa kwa kampeni zake za kulinda wanayama na hata huo ukulima pia uwenda ataisaidia nchi yake kujitegemea kwa chakula na kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya nchi.Mwalimu Mhango, wache tumsubiri,,tumwangalia na kumfuatilizia kwa makini na tuone, lakini iwapo itakuwa ni ulevi wa pombe ya manazi(madaraka) imemzidi tutamuona pia akichenza,akisinzia na hata kuanguka na ataendelea kuropoka yaliyokuwemo na yasiyokuwemo kama Rais msataafu.

NN Mhango said...

Anon usemayo ni kweli. Ni ulevi wa aina yake kwa mtu ambaye amekuwa madarakani kwa miaka kumi bila kufanya kitu kujiaminisha na kuuaminisha umma kuwa anaweza kufanya kitu baada ya kung'oka madarakani. Huu ndiyo unaoitwa usanii na ufisadi wa kimawazo. Ni uongo uliokithiri unaopaswa kutoaminiwa na kulaaniwa.Kama ulivyobainisha, letu ni kungoja kumuona komba wetu akikata usingizi baada ya kuanguka toka kwenhye mnazi anaodhani ni wake wakati si wake.
Shukrani kwa mchango wako na nadhani wahusika watasoma na kuchukia kama siyo kumfikisha ujumbe mhusika na genge lake. Tumemstukia hata hivyo.

Anonymous said...

Mwalimu Mhango, Nyngeza huyu mh... yupo madarakani katika ngazi ya juu serikalini tangu mwanzoni miaka ya themanini isipokuwa katika!

NN Mhango said...

Anon nimekupata kama amekaa madarakani kwa muda wote huo na kazi yake ni kufanya madudu ukiachia mbali maisha yake binafsi kuwa aibu tupu utegemee nini baada ya kustaafu?