Friday, 22 May 2015

Mlevi kumkabili Nkurumbwiza

  • Burundi : le président Nkurunziza appelle à cesser les ...
       Baada ya wachovu wa Urundi kulianzisha wakipinga upuuzi wa mlevi mmoja wa madaraka Pyere Nkurumbwiza kutaka abaki madarakani kinyume cha sheria ili akwanyue zaidi, dunia ilishangaa sana roho mbaya ya njemba hii.
Waurundi walifanya kosa kutaka viranja wa East Africa Calamity waingilie kati wakati nchezo wao ni ule ule. Nani amuonye au kumshugulikia nani wakati nyani wote kazi yao kuiba mahindi? Ukiangalia Bongolalaland, Chama Cha Mang’ang’anizi (CCM) kimekuwa madarakani tangu kikiwa kinda hadi sas kikiwa kikongwe kilichoishiwa si meno bali hata kupofuka na kupoteza kumbukumbu kikigeuka mhimili wa ujambazi, ufisadi na kila jinai
Ukienda pale UG uchafu ni ule ule. Imla wao wa muda mrefu –licha ya kuchanganyikiwa na kudhoofu kimwili na kiakili –bado yumo madarakani akiendelea kuiba na kutanua na genge lake la kikabila.
Pale jirani kwa jamaa zangu wa kunyotoana roho wao kwa wao mambo ni yale yale mchezo ule ule njemba ile ile.
Kwa akina Nyayo ndiyo usiseme. Jitu linachaguliwa kwa vile baba yake alikuwa rahisi ukiachia mbali kupiga kura kikabila. Waulize akina Uhuu Kinyata waliingiaje kwenye maulaji kama si wizi wa kura na ukabila. Je nani awasaidie hawa jamaa walioamua kujitambua na kufanya kweli? Natamani walevi wangu nao wangejitambua hivi na kulianzisha ili kuondokana na huu uoza na ufisi na ufisadi wa genge la mafisadi la Njaa Kaya.
Kimsingi, viranja wa EAC hawana ubavu wa kumwambia Nkurumbwiza asiendelee na mipango yake michafu kwa vile nao ni wachafu tena wengine kuliko yeye hasa ikizingatiwa kuwa yeye si wa kwanza kubadili katiba na kuendelea kuwa madarakani. Waulize akina M7 wametawala vipindi vingapi na wataondoka lini. They have no idea as to when they will relinquish sweet power. Nyani wote wana tabia zinazofanana. Hata hivyo, ni ajabu kwa jeshi kuvunja katiba na kudai linailinda. Kwanini wasiwaache Waurundi waamue wenyewe kwa kuwapa msaada wa kuzuia jeshi na Nkurumbwiza kuendelea kunajisi kaya? Mijitu mingine bwana, linang’ang’ania ikulu utadhani mali ya mama yake. Guess what. Mlevi alizaliwa peke yake.  Hivyo, alipokuwa mdogo aliamini ziwa la mama yake ni mali yake pekee. Hata hivyo, baada ya kupevuka aliachana na mambo haya ya kitoto ambayo yanafanywa na watu wazima tena wanaoitwa rahisi.
Baada ya kuona zali haliishi na wale wanaoonekana kuwa viongozi wakichemsha, Mlevi anajiandaa kutia timu Buja kumpa laivu Nkurumbwiza kukitoa kwa vile wachovu wa kule hawamtaki. Pia hii ni kupinga kutapatapa kwa katibu mkuu wa Un kumteua M7 eti ashughulikie mgogoro aliouanzisha yeye kwa kubadili katiba. Baada ya kumshawishi Bank in the Moon amebatilisha uteuzi wa M7 kwa kuniteua mimi.
 Nitafanya hivyo ili kutuliza hali na kuepuka kuongezeka ghasia kiasi cha kutujazia wakimbizi. Msituletee mbu kwa tamaa zenu ingawa wakubwa wetu wanaonekana kuwa kitanda kimoja na Nkurumbwiza kwa vile wanasifika kwa ung’ang’anizi na wizi wa kura.
Najua kwa anavyochukiwa na kupingwa, bila kuchakachua Nkurumbwiza hawezi kupenya. Sijui kwanini amengoja kiumane wakati kaya ni bora kuliko fisadi mmoja wa maulaji? Amesahau nini ikulu ana anang’ang’ania kulinda jinai gani zaidi ya ufisadi na ufisi?
Kwa vile mlevi ni kidume kisichoogopa mvua radi wala mtutu, nina mpango wa kutia timu kule na kumpa jamaa vipande vyake. Napanga niingie kininja nikiwa nimetinga jezi zangu za karate. Akijifanya hamnazo nitavunja mtu shingo bila huruma. Mdudu mmoja hawezi kujifanya alpha na omega wakati kaya ni mali ya walevi na wachovu. Kama  hawakutaki si uende ukafanya biashara nyingine kwani lazima siasa za urahisi? Si urejee chuoni ukapige lecture na chaki kama ulivyokuwa ukifanya kabla? Kama miaka kumi haikukutosha hata upewe mia haitatosha. Tafadhali bwana Nkurumbwiza. Natoa onyo kabla sijaingia. Kama utaendelea na utoto na uroho huu amini vitakutokea puani. Na ufahamu kabisa kuwa mimi huwa sitishi bali kufanya kweli hasa mibangi na gongo vikishapandisha Mwenembago. Ohooo! Shauri yako utaumia bwana mdogo Nkurumbwiza! Mie siyo kama hawa akina chekacheka wanaokuchekea.
Kama Nkurumbwiza anadhani ninatania basi akaulize kule Burkinabe na Libya nilipokwenda kutia timu hadi mibuyu ikadondoshwa huku wengine wakiuawa kwa kichapo kama vibaka wakati walikuwa mibaka.
Kwa vile mimi ni mpenzi wa demokrasia hata kama ni ya kuazima toka Ulaya, sitakubali ndata au Nkurumbwiza waendelee kuibaka kaya hii kiduchu kama mkoa wa Bongo. Nitahakikisha kinaeleweka na kushuhudia Nkurumbwiza akibwaga manyanga vingine kutachimbika bila jembe na patakuwa hapatoshi kusema ule ukweli.
Haiwezekani waafrika tuendelee kutawaliwa na miunguwatu na wakoloni weusi kana kwamba kaya zetu ni mali zao. Hata hawa waliochakachua katiba ya mzee Jose Waryuba wajiandae. Nikimaliza kutatua mgogoro wa Urundi lazima niwashukie kama sina akili nzuri.
Kwa vile nilipinga kutoa uachama wa EAC kama pipi kwa viichi visivyo na wakubwa wenye adabu, nikimaliza kutatua mgogoro huu lazima niende kwa pilato kupinga uanachama wa kaya zisizofuata demokrasia. Kimsingi, hapa ninachotaka ni kuvunjilia mbali hili genge la EAC ambalo halina maana zaidi ya shoptalk za wakubwa zake. Kama mnataka kufanya kweli basi unganisha bara zima la Afrika ili muionyeshe dunia mlivyojikomboa. Maana hii mipaka na utaifa mnaolingia vilipandikizwa na wakoloni ili kudhoofisha Afrika kwa kuipatia watawala manyag’au iendelee kurudi nyuma. Akina Fredrick Lugard yule bingwa wa Divide and rule and then depart hawapo tena zaidi ya kuwa na Lugard weusi waliojazana kwenye ikulu wakikwamisha muungano wa Afrika. Huwa sipati mantiki ya Afrika kuwa na vipande vya kaya.
Go Nkurumbwiza go
Go never turn back, go
Go Nkurumbwiza go.
Chanzo: Nipashe Mei 23, 2015.

7 comments:

Anonymous said...

Hapa kijiweni kwetu kwa walevi tunataka kuchagua viongozi wa kisiasa ili baadae watunukiwe hadhi ya kifalme au vipi mwalimu!!!?

NN Mhango said...

Mkifanya hivyo mmekwisha. Fanyeni kile wanachofanya warundi hata kama wanazidiwa kete tokana na sapoti Nkurumbwiza anayopata toka kwa wahalifu wenzake kwenye eneo hili walioko mdarakani.

Anonymous said...

Si unafahamu mambo ya ulabu hatujali hata akiwa mfalme wetu hapa kijiweni kwa wealevi kwa busara zetu pombe isipokuwa pombe ikitoka tuu kichwani tutamvurumisha kama mvua ya elininyo kama mwenzake Compaire!

NN Mhango said...

Nawatakia struggle njema ya kuwa-Compaore hata kuwa-Gaddafi wafalme uchwara wenu mliowachagua kwe ulevi.

Anonymous said...

Salaam Mwalimu Mhango,
Ninachokiona mimi katika kadhia hii ya ulevi wa madaraka wa viongozi wetu wa kiafrika hususa katika zone hii ya Afrika mashariki na kwingineko ni kutokana na hali ya kisaikolojia ambayo imeambatana na hawa ambao wanaochukua madaraka au waliokuwa madarakani kwa muda mrefu kwa kutumia demokrasia isiyo sahihi,wizi wa kura,kununua kura kwa kuwaonga walala hoi wa nchi zao au kwa kuwekwa na baadhi ya mataifa yenye nguvu duniani.Hali ya kisaikolojia ya kujiona kwamba wao ni tabaka la wasomi(ELITE) na tabaka hili kwa Afrika daima, na siku zote,uambatana na maradhi mengine ya kisaikolijia ya hisia ya ukubwa,ubwana,kiburi na ubora(SUPERIORITY COMPLEX) na kwa maradhi hayo huwa wanawaona,kuwachukulia na kuwazingatia wananchi wao ni viumbe duni kwa kila upande,na hatimaye huwa wananawachukulia kwa uhakika (FOR GUARANTED).Na hata kuna madai kwamba wakoloni wetu waliwapandikiza hawa ma- ELITES ili wakiyaachia makoloni yao ma-ELITES hawa waendele kuyapigania na kuyatetea masilahi ya wakoloni wao na kuwakandamiza wananchi wao,Mwalimu Mhango,kwa hali hii si unaweza kuyaamini madai hayo? Hatimae ndio hii hali ya unyanyaswaji wa wananchi wa kiafrika na viongozi wao kwa kila secta ya maisha yao kijamii,kisiasa na kiuchumi.Kwani haiwezekani katika karene hii ya 21 tunayoishi na kuwepo na mihimili ya kijamii kisiasa na kiuchumi ambayo ndio kauli mbiu ya dunia,ukiongezea uharaka wa mawasiliano,teknolojia na sayansi ambayo inaifanya hii dunia kuwa ni kijiji kimoja GLOBALISATION).Kumbuka, Mwalimu Mhango,somo la karibuni liliotokea Burkina Faso na nakumbuka uliliandikia somo hili kwa matumaini kwamba itakuwa ni somo kubwa kwa wale wenye uroho wa kubaki madarakani kwa kuvunja katiba,leo hii limetokea Burundi,kesho kwenye Kaya yetu kwa wizi wa kura na kuwahonga wapiga kura masikini na hata kutumia udini na ukabila ili hali CCM ibaki madrakani.
Kwa viongozi wa namna hii kwao wao Demokrasi si haki ya wafrika,haki za kibinadamu na uhadilifu kwa wananchi wao si haki ya waafrika.Mwalimu Mhango,tusisahau somo la historia kwamba wanyanyaswaji wote katika historia ya wanadamu inatakikana dhamiri za wanyanyasaji zihisi aidha nusu dhambi au dhambi kamili ili kuwapa haki zao wanyanyaswaji.Je kwa viongozi wetu wa kiafrika wapo tayari kuhisi nusu au dhambi kamili ili wawarudishie haki wananchi wao?Ikiwa hilo haliwezekani kwao,kwa nini kusiwe na ufumbuzi wa wananchi kuchukua haki yao ya kisiasa kwa kugoma kuichangamkia hii demokrasia "fake"kwa kutoshiriki kikamilifu katika kuwapigia kura viongozi hawa wenye tamaa ya uongozi kwenye uchaguzi mkuu,sawa wananchi wa Burundi wameshatoa salamu kwa rahisi wao kwa kutoka barabarani kilichobaki sasa hata kama mroho huyo wa madaraka ataendelea na ajenda yake ya kuivunja katiba ni juu yao kugomea uchaguzi utakaokuja,hapa nashauri wananchi wenyewe bila ya kujiingiza vyama vya upinzani kama ilivyotokea Sudani kaskazini katika uchaguzi mkuu uliopita.
Je umeona Mwalimu Mhango, kuchekwa na kudharauliwa kwa wananchi wa Afrika mashariki kwamba viongozi wetu hawa wamekutana Tanzania ili kuliongolea swala hili la Burundi?!Je ni kiasi gani cha pesa zilizotumika za walipa kodi wa nchi hizo kwa ajili ya kutubeza na kutuona kwamba sisi wananchi ni mataahira na mandondo!Umefafanua Mwalimu Mhango katika makala hii,lakini wache nami nimalizia kwa kuandika, tangu lini kesi ya kushitakiwa kwa Nyani ikawa mashahidi,mwendesha mashtaka na hakimu ni Sokwe,Ngedere,Komba hata akina Baboons na Magorila wakawa wazee wa baraza???!!!!!

NN Mhango said...

Anon usemayo ni kweli. Hata hivyo, haya mambo nimeyadili kwa kirefu kwenye kitabu changu ninachomalizia kwa sasa kiitwacho AFRICA REUNITE OR PERISH Inshallah kikitoka ukakipata nadhani utasoma mengi na kujibu na kuuliza maswali mengi.
Ubarikiwe tena kwa kuwa mgeni wa mara kwa mara kwenye uga huu.

Anonymous said...

Salaam Mwalimu Mhango,
Ahsante pongezi kwa kazi njema tunakisubiria kwa hamu kitabu hicho.Naam,bado tunaendelea hatua kwa hatua kikosoma hiki cha Nyuma ya Pazia.Nakutakia kila la kheri na wepesi na mafanikio.