Saturday, 9 May 2015

Mlevi anusurika kufa kwa madawa ya kichina

  • Chinese-herbalist-008.jpg
          Baada ya kaya yetu kuhalalisha haramu ya sera holela chini ya kisingizio cha ruksa na biashara huria si matapeli wengi waliingia kayani kiasi cha kuhatarisha maisha ya walevi. Hata bangi tunayovuta na ulabu tunaopiga mwingine unaagizwa toka nje utadhani hatuna zana hizi.
Juzi si ngiri ikapanda. Kwa vile mahospitali yalikufa zamani yakabaki kuwa vyanzo vya madawa kwa famasi zinazomilkiwa na madaktari na wafanyakazi wengine wa hospitali za umma, niliamua kwenda kwa mchina kupata dawa.  Niliamua kwenda kwenye tiba mbadala hasa kwa kuogopa kwenda hospitali nikatolewa upepo wa kuomuona daktari utadhani ni kidosho mzuri mzuri. Mie si mshamba kiasi hicho kuibiwa mchana wakati ni njanja. You know what. Mganga niliyemwendea si mchina. Mganga mwenyewe hata Kiswahili hakimanyi ukiachia mbali kuonyesha wazi alivyo msanii zaidi ya tabibu. Hata hivyo simlaumu hasa ikizingatiwa kuwa hii kaya ni ya wasanii watupu kuanzia wazito hadi wepesi. Hamuoni wanavyofanya usanii wao kwenye kila jambo hadi hata kwenye elimu? Hayo tuyaache.
Alinipa dawa zenye maandishi ya kichina huku akijitahidi kunifafanulia kwa kichina. Mara nǐhǎo, hǎo jiǔ bú jiàn wǒ hěn hǎo, hiinnhoo, huuunhiii, heeiieye, guo feng hua nung kong huuunhaaniii kom. Mswahili na kichina wapi na wapi? Basi shida mwanaharamu. Kwa vile lisirikali lilishanitoa kafara ilibidi nipwakie hii midawa ya kichina. Kufika nyumbani, bi mkubwa akanichemshia maji na kuchanganya na kunipa ninywe. Punde si punde si nikasikia sauti za radi na ngurumo tumboni mwangu. Wacha niendesha hadi nidhani nitanonihino utumbo!
Baada ya kukutwa na ya kunikuta nilijiuliza maswali bila majibu. Je inakuwaje hawa wajalaana wanawaruhusu wajalaana wa kichina kuja kutupa midawa ambayo hata maelezo yake hatujui? Je ni ufisadi na ujinga wa wanene wetu? Bila shaka hapa kuna mtu amehongwa kitu kitu ili hawa matapeli waje kufanya biashara yao. Kwanza siamini kama biashara wanayofanya ni ya hii midawa ya kufanya mtu aendeshe kama mkangafu. Huenda kuna biashara nyingine hasa ikizingatiwa kuwa kaya yetu ina tembo na faru wengi. Hayo tuyaache. Kama twiga wanauzwa hai tena mchana, kwanini wajamaa wasifanye vitu vyao? Waduwanzi ndio waliwao au vipi?
Hebu tuzidi kujiuliza hata kama ni kibangi bangi na mma mma. Je mswahili anaweza kuuza miti shamba yake uchina asizuiliwe au hata kubaguliwa kama jamaa zangu wa dukani ya Huarang pale Ursino street? Sijui nao hii kesi yao ya racism-cum-apartheid-cum –dihumanization imeishia wapi?  Je tunawaamini vipi hawa watu tena ambao baadhi yao wanatubagua wazi wazi?
Baada ya kujiuliza maswali haya, niliamua kwenda kwenye maktaba yangu kujisomea lau nipate majibu kama siyo maelezo ya kutosha. Katika pitapita yangu si nikapata kitabu cha mzee Mchonga cha Freedom and Development na Crusader for Liberation. Kusema ukweli nilisoma na kupata mengi hasa juu ya dhana nzima ya kujikomboa kiakili yaani Mental emancipation. Nilichojifunza toka kwa gwiji huyu (Mwenyezi Mungu ameneemeshe na kumpuzisha) ni kwamba tunatawaliwa kijinga kwa sababu sisi ni wajinga. Dawa ya moto ni moto. Ukiwa mjinga unatawaliwa kijinga na wajinga huku kila kitu kikifanyika kijingajinga nawe kwa ujinga wako hutafuti suluhu ya kuondokana na utawala na mambo ya kijinga jinga kwa vile u mjingajinga.
Ili kujitoa katika ujinga niliuliza maswali mengine makali. Je afrika imeishiwa miti ya kutibia madawa ya kiafrika? Je ni wachina wangapi wako tayari au wanatibiwa kwa miti ya kiafrika tena na waganga wa kiafrika? Thubutu! Ukipatwa na kiherehere ukaenda kule na mitunguli yako wanakurambisha shaba wakisema ulikuwa umebeba bwimbwi. Je kabla ya kuja wachina mababu zetu walijitibia na nini? Au ni kwa vile wanene wanakwenda zao kutibiwa India huku wakiacha wachovu wapukutike kama inzi? Kama mitishamba ya kichina ni bab kubwa kwanini wanene wetu wanatibiwa India badala ya uchina? Hapa kunani kama siyo gea ya kutuingizia wakimbizi wa kiuchumi waliotamalaki mitaani wakichoma mahindi na mishikaki huku tukiaminishwa ni wawekezaji wakati ni wachukuaji wa ajira zetu na wakimbizi wa kiuchumi tena wenye kufanya biashara haramu kama vile pembe za ndovu na madanguro kama hawa wa Huarang?
Najua jamaa zangu wa Huarang watakana kuwa si wabaguzi wa rangi kama wenzao wa kigabacholi. Basi kuwaumbua nitapendekeza nimuoe yule kidosho wa Huarang anayesemekana kuwafokea waandishi wa habari waliotaka kujua ni kwanini anabagua waswahili. Loooh! Nimechemsha! You know what. Kutokana na kupiga mibangi nimeanzia stori katikati. Ni kwamba hivi karibuni kule kwenye mtaa wa Ursino kwa wanene, waandishi wa umbea waligundua duka moja la kuuza makulaji ya kichina liitwalo Huarang ambalo haliruhusu weusi kungia mle. Kwa hiyo ukiona Huarang ujue ni makaburu wa kichina waliopo hapa kayani wakilindwa na mafisi na mafisadi wanaonufaika na biashara hii ya dangulo.
Guess what. Wabaguzi wa rangi wana tabia zinazofanana. Hata magabacholi wamekuwa wakiendesha madangulo kwa kisingizio cha kuleta vidosho toka Bombei kuja eti kucheza Bhangra na Mujra. Urongo. Yote hayo ni mandangulo ambapo kwa ubaguzi wao hata madhambi wanafanya kibaguzi.
Kama kaya yetu isingekuwa ya wajinga wajinga ikiliwa na kutawaliwa kijinga jinga huyu jamaa ningemuondolea uvivu nikamshitaki anilipe fidia kwa kupunguz kitambu changu tokana na kuendesha. Pia ningedai fidia kwa maumivu aliyonisababishia ukiachia mbali presha ya kunyotoka roho. Maana alinilisha sumu tena kwa kuniuzia.
Hivyo, ndugu zanguni, ndivyo nilivyonusurika kufa kwa midawa ya kichina. Je ni wangapi wanaonyotoka roho tokana na mchezo huu bila kuongeza wanyama zetu hasa wale wenye vipusa na pembe? Hapa sijagusia ubaguzi wa akina Huarang.
Chanzo: Nipashe Mei 9, 2015.

2 comments:

Anonymous said...

Salaamu Mwalimu Mhango,
Unaposoma vitabu hivi viwili vya Jonh Perkins,
1-Confession of Economic Hit man.
2-The Secret history of American Empire.
Na hatimae ukajaribu kufanya utafiti wa ndani na wa kina wa nini kinachoendelea katika nchi zetu za kiafrika ukiachilia mbali nchi zingine za ulimwengu wa tatu ambapo mwandishi ameweka wazi nini kilichojiri na bado kinajiri katika nchi hizo.Kwa maoni yangu mwandishi ametaka kutuliza dhamiri yake ambayo ilikua inamsuta na kumkaripia kwa maovu na ushenzi ambao unaofanywa na taifa la Marekani,pamoja na uwazi na ukweli huo lakini hali hakubadilika na haitobadilika kamwe.Mwalimu Mhango,maswali yanayojiuliza kwa nguvu hapa ni haya? Je baada ya kufa kwa Mwalimu Nyerere kwa nini madudu yote,machafu yote,ufisadi wote umeibuka kwa kasi sana katika nchi yetu?Je Kwa nini viongozi waliokuja baada ya Nyerere watuongoze kwa falsafa ya "MASILAHI YA FAMILIA YANGU NDIO MUHIMU KWANZA NA MASILAHI YA WANANCHI NA NCHI GO TO HELL?!!!"Kwa nini leo tuwe na wakimbizi wa kiuchumi Tanzania?Kwa nini leo Mtanzania anabaguliwa na kudharuliwa ndani ya nchi yake?Kwa nini mwananchi wa Tanzania hayupo salama kiakili na kisaikolojia?Kwa nini mwananchi wa Tanzania anahisi ni mgeni na hayupo huru katika nchi yake?Wachina,wahindi,waaarabu,waturuki,wazungu na wa Nigeria, hivi wote wana sifa ya uwekezaji?Na kwa nini wengine wanatoka huko wanapotoka na wafanyakazi wao?Hivi watanzania hawastahiki kupata ajira?Kwa nini leo mgeni katika kupata au kupewa ajira anaepewa kipau mbele kuliko mtanzania?Ikiwa leo ndio tumefikia mpaka madwa ya kienyeji yatoke China yalikua ya kweli au fake.wauza uroda nao ni wakigeni,karanga,nyanya mishikikaki inauzwa na wageni,wamachinga ni wakigeni na mengine mengi tu.Je ni kweli hawa viongozi hawajui nini majukumu yao mbele ya nchi yao na wananchi wao?Wametudanganya na kutwambia kwamba hii ni zama za Globalization na sisi tumeitika na matokeo yake ndi haya na kwa bahati mbaya ni umasikini wa watanzazia tuliokuwa nao lakini vinginevyo makampuni ya kuuza Humbuger yangejaa nchini kote na kutuharibia afya ya vijana wetu .Je viongozi wetu ni mataahira kiasi hiki?au ni sisi wananchi ndio mataahira?Mwalimu Mhango, hapa kuna namna moja au nyingine kwamba kuna kitu kimepita na bado kinaendelea kuwepo nyuma ya panzia na viongozi wetu wamekuwa wana sesere tu.Kwa hiyo kama wananchi wa Tanzania sio Mataahira,umeshafika wakati wa kuwakalia shingoni viongozi wao aidha waliokuwepo madarakani(CCM)au wakifanya mapinduzi ya na kukiweka chama kingine madarakani wawe na sauti ya nguvu na kukekemea kwa nguvu na hata kuchukua hatua zinazostahiki kuwaangusha na hata kuwatoa madarakani katika uchaguzi mkubwa au mdogo.Wakati wa kufanywa mataahira,mazuzu,majuha na wajinga umeshapita.Madaraka ni lazima yawe ya watu,kwa ajili ya watu na nchi na wala sio ya watu wachache na mbawana zao wakiwa wa ndani au wa nje.Tanzania hatuwezi tena kupata viongozi kama akina Julius Nyerere,Thomas sankara,Kwame Nkuruma na wengine wenye uchungu wa nchi na wananchi wao. Ni juu ya wananchi wenyewe kuwa na hadhari na viongozi wao kila kukicha.

NN Mhango said...

Anon usemayo kweli na maswali yako ni ya msingi. Kimsingi, japa maswali yako ni mengi, naweza kuyapa jibu moja muhimu kuwa baada ya kun'atka akaja Mwinyi na sera zake za hovyo za ruksa ambayo kimsingi ndiyo mama wa maovu yote unayoona maadili nayo yaling'atuliwa azimio la wahuni akina Malecela la Zanzibar. Baada ya kuua maadili ulijengeka mfumo wa kijambazi ukisimamiwa na majamazi waliozalishwa na utawala mbovu wa Mwinyi. Huyu Kikwete unayemuona na nyang'au wenzake walitengenezwa na Kighoma Malima kwa kumtumia Mwinyi chini ya dhana mfu ya ku-empower waislamu. Naweza kukutajia majina ya watu vihiyo kuanzia majaji hadi wakuu wa mikoa na wilaya walioteuliwa si kwa sababu ya sifa nyingine zaidi ya dini. Wengi nimesoma nao, ni marafiki zangu nawajua nje na ndani.
Kwa hiyo hiki unachokiona ni matokeo ya kukosekana mfumo adilifu wenye maadili ya utumishi wa umma. Huu umekuwa wimbo wangu. Huku Ulaya kiongozi au mwananchi hawezi kuishi bila kujaza mapato yake kila mwaka ili kuona kama yanaendana na kipato chake halali. Ukosefu wa maadili nchini umezaa biashara ya mihadarati, uwekezaji chukuzi unaoongelea wa wachina kuuza mishikaki na hata miili. Ubaguzi iwe wa rangi au ajira unaoona ni matokeo ya kutawaliwa na watu wenye akili za kutia shaka. Wakati wa Nyerere tulikuwa na viongozi na baada hapo walikuja watawala na mafisadi wa kawaida. Ukosefu wa kujiamini kimkakati na kisaikoloji katika hali kama hii hakuepukiki hasa ikizingatiwa kuwa mwananchi halisi hana usalama wala pa kukimbilia anapopata matatizo. Kwa ufupi ni kwamba taifa letu limegeuka la kijambazi na kitapeli.