Monday, 15 June 2015

CCM imseshikwa pabaya muhula huu

  • Philip Mangula Aunguruma Ilemela na Nyamagana Mwanza
          Hukuna ubishi CCM sasa iko pabaya na imeshikwa pabaya. Yanayoendelea kwenye kuusaka kuteuliwa na chama kwa watangaza nia kumrithi rais Jakaya Kikwete ni ushahidi tosha kuwa chama hiki kiko chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kinapumulia mashine. Chama kimeparaganyika. Hakina hata mtu wa kuweza kuwakaripia wanaovurugana na kuvuana nguo hadharani. Ushahidi wa namna watangaza nia wanavyoshambuliana na kumkosoa rais anayeondoka uko katika kila matamko.  Hawana nidhamu tena. Kila mtu anacheza ngoma yake kivyake na wakati wake.
          Kwa kuchanganyikiwa na kuparaganyikiwa kama walivyo, CCM wamekuwa kama kambale ambapo kila mmoja ana sharubu huku wote wakiwa kwenye kokolo liitwalo CCM ambalo hukumbakumba kila kitu kuanzia samaki hadi mamba na kenge. Japo demokrasia ni ushindani wa hoja ili kuonyesha wapiga kura kuwa mhusika anafaa, kwa CCM si hivyo. Kuna mitandao haramu ya kimaslahi ambayo bila shaka ndiyo itapigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza litakaloizika CCM. Kutokana na mitandao hii ya ulaji, tumeshuhudia hata wale tuliodhani ni wakongwe tena wanafunzi wazuri wa Marehemu baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere wakigeuka nepi za watangaza nia wenye si mabaka tu bali mizigo ya kashfa nyingi tu. Kwa mfano, unajiuliza swali ambalo jibu lake linakuwa gumu. Hivi –kwa mfano –Kingunge Ngombale-Mwiru alikumbwa na nini hadi akampitisha na kupigia debe Lowassa zaidi ya kupinga kile alichowaaminisha watanzania kuwa alikuwa akikipigania? Je ni uzee au njaa au sumu ya mitandao ambapo chama kimegawanyika kwenye vyama vya upinzani vya ndani yaani mitandao ya kimaslahi? Je nani alaumiwe kwa uoza huu zaidi ya mwenyekiti wa CCM rais Kikwete ambaye alianzisha mitandao hii mwaka 1995?
 Rushwa inatembea wazi wazi. Kwa ufupi ni kwamba CCM imekosa mtu wa kukemea. Akina Kingunge tuliowategemea sasa wameishalishwa lilmbwata.
          Hakuna sehemu CCM iliponiacha hoi kama kuja na sifa na vigezo vya kumpata atakayepeperusha bendera. Unashangaa. CCM yenyewe inayoweka hizi sifa au vigezo haina sifa hata moja. Huu naona ni unafiki wa aina yake. Kwa niijuavyo CCM, haina mtu hata nusu mwenye kufaa kuwa rais hata kutokana na yanayozidi kufichuliwa ukiachia mbali kuwa na rekodi mbovu kiuongozi na utendaji. Tangu CCM ilipowekwa mifukoni mwa mafisadi, nadhani ilikufa na kifo cha Nyerere ambaye angalau alikuwa akikaripia.  Ukitaka kujua CCM ilivyoisha na kuishiwa angalia wanavyonangana kwa sasa. Ni kama mchezo wa kuigiza ingawa mwisho wa situ watashikamana baada ya kuhujumiana na kujeruhiana.
          Mtifuano ndani ya CCM ni ushahidi kuwa inapwa na imeisha na kuishiwa bila kusahau kupwaya kwa mwenyekiti wake. Anayejaribu kufurukuta ni katibu mkuu Abdulrahaman Kinana ambaye kila siku yuko kiguu na njia akitangaza chama mikoani. Kwanini sasa wakati wa kuelekea uchaguzi? Hii maana yake ni kwamba CCM iliwatelekeza wananchi kiasi cha kuisahau. Imewakumbuka wakati huu inapotaka kura kutoka kwao. Baada ya kuipata itaanza kula kama kawaida ikiwaacha Solemba.
          Ukimtathmini Kinana na kashfa yake ya kusafirisha vipusa nje, huoni kama ataleta mageuzi wala lolote la maana zaidi ya kula fedha ya chama kwa ziara zisizo na tija.  Sijui kama Kinana –kwa mfano –ana udhu wa kutosha kumwambia mtu kama Edward Lowassa kuwa hafai kwa vile ana kashfa ya Richmond shingoni mwake. Sijui kama Kinana anaweza kumtokea mtu kama Wiliam Ngeleja kuwa alitimliwa kutokana na kuwa mzigo au January Makamba kuwa anatumia jina la baba yake na hana lolote. Sijui kama Lowassa anaweza kumvaa mtu kama Stephen Wassira na kumpa kuwa haaminiki zaidi ya kusaka maslahi kama alivyofanya wakati alipotimkia NCCR-Mageuzi. Kwa lugha rahisi CCM sasa ni kama vyura kwenye dimbwi. Kila mmoja anaimba yangu yangu wakati hana lake.
          Hata karipio la Philip Mangula kuwa wanaotangaza nia wanapoteza muda haliingii akilini wakati chama kimeshindwa kuwazuia. Ukiangalia watu ambao wangeweza kuwa na ushawishi kiasi cha kuleta nidhamu chamani kama Fredrick Sumaye nao wamo wakisaka urais kana kwamba miaka kumi aliyokaa madarakni haitoshi.

          Kwa hali ilivyo ndani ya CCM, kama ikitokea kikashinda uchaguzi ujao basi lazima mambo mawili yatokee kwa pamoja au mojawap. Ima itokee miujiza au wachakachue kama walivyozoea. Kwa walivyo uchi sidhani kama wanaweza kuchaguliwa hata na ndege achilia mbali binadamu tena watanzania.  Maana badala ya kutangaza sera zao, kila mmoja amegeuza sera kuwa yeye. Anajitangaza kwa vigezo vyake uchwara huku akikwepa kujibu maswali muhimu kama ilivyobainika walipokacha mdahalo ambapo mwenyekiti wake Ali Mfuruki alikaririwa akisema kuwa baada ya wahusika kujua aina ya maswali ambayo wangepaswa kujibu waliamua kujitoa kama ushahidi kuwa hawana sera wala mpango wowote wa kutawala zaidi ya maslahi binafsi. Mfuruki alisema kuwa kila mtangaza nia alitakiwa kujibu maswali manne ya uchumi na manne ya utawala bora na utawala wa sheria na ya aina moja. Je watu wanaokimbia hata mdahalo ambao ungewasaidia kuonyesha makali na sera zao wana jipya la kulifanyia taifa? Ama kweli CCM imeshikwa pabaya tena ikiwa haina nguo. Nadhani wakati wa watanzania kuchagua rais toka nje ya CCM umewadia.
Chanzo: Dira Juni 15, 2015

No comments: