Tuesday, 23 June 2015

Kijiwe chasikitika kutoagwa


          Baada ya munene kuanza kujivinjari ughaibuni na kidosho chake na marafiki, washirika, wapambe, ndugu, na waramba makalio wake, Kijiwe kimestuka na kuonyesha hasira zake dhidi ya ujidhalilishaji, na udhalilishaji huu wa kujitakia.
          Mpemba ndiye analianzisha leo. Anaamkua na kusema, “Jamani mmesikia kuwa jamaa yetu Njaa Kaya kenda zake Ulaya na ugabacholini kuwaaga utadhani sie tuliomchagua hatuna thamani? Huyu jamaa kaingiliwa na nini yakhe?”
          Kanji kaguswa pabaya! Anakwanyua mic na kulalama, “Pemba veve nafanya mbaya sana bwana. Kama kuu nakwenda Bombei aga veve nahusu nini? Veve taka aage mke yako?”
          Mpemba anajibu mapigo tena akiwa anaonyesha kuchukia kidogo. Anasema, “Tuheshimiane Kanji kabla sijakuita gabacholi bure ingawa wote wale wale. Kwani kosa langu nini yakhe au kusema ule ukweli nionao kama npiga kura wa kaya hii?”
          Mgosi Machungi naye hajivungi. Anakula mic, “Hapa azima tiambizane ukwei tena ukwei mtupu. Kama aivosema Ami anachofanya jamaa yetu ni udhaiiishaji wa kujitakia. Kwanini aage ughaibuni wakati sisi tiliompa kula atiache kana kwamba hatina thamani? Oh tate nane hii si haki waahi.”
          Msomi Mkatatamaa anakatua mic, “Mie sishangai. Kimsingi, huyu  jamaa  hakuwa rahis wa kaya bali rahis wa ughaibuni aliyekesha na kushinda kwenye pipa akienda kuzurura hadi akaitwa Vasco da Gama. Ukisikia utumwa wa kujitakia utokanao na kutojiamini na ukoloni mamboleo ndiyo hivi. Sijui atakapotundika jezi atazurura vipi na kutanua bure. Heri, akawaage hao aliowafurahisha na kuwafaidi kuliko sisi aliotuudhi na kutusikinisha. Aende mwana kwenda tu.”
          Mijjinga anakatua mic huku akiweka ki-sumsung chake mezani ili kila mtu akione kilivo cha bei mbaya, “Nakubaliana na wasemaji wote waliotangulia. Heri akitoe lau njuluku zetu zipone. Maana alivyozitumia kwa kutanua na kuzurura hukuk akiwapa tafu mafisadi wenzake mwenzenu sina hamu. Heri atokomee mwana kutokomea tunusuru heshima na njuluku zetu au vipi?
          Kapende, kama kawaida yake anakandia, “Hakuna haja ya kumshangaa wala kumlalamikia jamaa. Kama aliendesha kaya kwa kubomubomu, kwanini asiwashukuru washitili wake? Isitoshe, asipokwenda kule kupewa ten per cent yake mnadhani atakula mafi yake baada ya kustaafu?”
          “Mkuu unakosea. Atakuwa analipwa mabilioni ya kustaafu baada ya kutuchuuza. Huoni Tunituni Ben anavyozidi kuchana utadhani anataka kujaa kwenye ramani ya kaya?” Anachomekea Mipawa.
          Mheshimiwa Bwege anakatua mic huku akimtazama Sofia Lion aka Kanungaembe ambaye anaonekana kutopendezwa na mada ya leo. Anakula mic, “Mijitu isiyoridhika hata ikilipwa matrilioni bado itataka mengine.  Lazima jamaa akaage ili wamkatie kitu kidogo ili baada ya kutundika jezi lau apate pesa ya kuzururia kama kawa. Kosa tunalofanya ni kudhani kuwa tunapochagua mafisadi wanageuka kuwa wenzetu au marahis wetu. Wenzenu wanatafuta ulaji ili wakale na hao mabwana zao wanaowaaga wakati wakitusaza sisi.”
                    Sofi kapata mwanya na sababu. Anakwanyua mic, “Siku zote nawambia. Mtakufa bure kwa vijiba vya roho. Mlitaka awaage nyinyi na majungu yenu? Kwanza, hawaamini mnaweza kumdhuru licha ya kuweza kumzomea.”
          Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea Sofi, “Walitaka azomewe kama Kinamna alivyozomewa na akina Nshomile baada ya kuleta rongorongo kuhusiana na meli yao na kucheza makidamakida na uhai wao siyo?”
          Msomi anaamua kurejea, “Mie nadhani jamaa amejivua nguo kutuonyesha tulivyokuwa tukifanya makosa tukidhani yeye ni bosi wakati ni kibaraka wa hizo kaya anazokwenda kuaga. Sitashangaa kusikia akisema eti anakwenda kumuaga Obamiza wakati hamtaki hata kumuona. Hata hivyo, tusishangae wala kulalamika sana. Kama mzee Mchonga alikuwa na hatukuona wasaudia kuja kuhani msiba wake lakini yeye kwa kimbelembele na kiherehere chake akijitia kwenda kule eti kuhami msiba wa falme lao. Anadhani jamaa wanamjali wala ku-appreciate kujipeleka kwake? Mie nadhani jamaa anatafuta per diem zaidi ukiachia mbali kutanua mara ya mwisho kwa kodi za wachovu aliowasaliti na kuwachuuza.”
          Mijjinga naye anarejea tena, “Usemayo profesa Msomi ni kweli tupu. Nadhani hapa kuna somo kubwa kuwa next time watuchague sisi wenye rekodi ya kutopenda kuzurura wala kuabudia wageni. Hii tisa, kumi ni atakaporudi utamuona amezungukwa na magabacholi na mafisadi wakimpa zawadi kwa kuwawezesha kutuibia mchana kweupe. Mie wala sishangai wala kuona ajabu. Huyu ni wa hovyo hivyo kama anavyoonyesha. Ama kweli mwanaharamu ni mwanaharamu hata umtie kwenye chupa shurti ainua kidole!”
          Mzee Maneno naye hataki kupitwa. Anakula mic, “Nadhani sisi kama wapingaji wa kweli lazima tujiandae kutumia mazabe yake haya kuwakaanga wenzake wanaokaangana wakitaka kuchukua ulaji tena ili watuuze utumwani kama siyo kutuchinja. Kaya inatuhitaji kwa sasa kuliko wakati wowote ndugu zanguni.”
          Kapende anadakia mic, “Hapo umesema mkuu.  Lazima mwaka huu mzee mzima aingie ikuu na kuipiga deki huku akiwanyongelea mbali mafisadi na jamaa yetu akiwemo bila kumsahau Tunituni.”
          “Wewe umeua!” Anachomekea Mchunguliaji aliyekuwa akisoma gazeti.
          Kijiwe kikiwa kinanoga si tukasikia kelele za mdege wenye mafua ukirejesha aibu yetu. Tuliondoka haraka haraka kwenda barabara ya Uindependence kumzomea jamaa akifika na msafara wa walaji na wezi na mafisadi wenzake!
Chanzo: Tanzania Daima Juni 24, 2015.

No comments: