The Chant of Savant

Thursday 25 June 2015

Kinana: Wananchi si hamnazo


          Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana huwa si mtu wa kuishiwa vituko. Wakati mwingine akiongea mambo huwa unashindwa kuelewa kama anaelewa anachosema au wale anawaambia kama anaamini kuwa wana akili kama yeye. Maana hujiongelea vitu wakati mwingine kiasi cha kuacha maswali kuliko majibu.  
Kwanza, amejitahidi kujionyesha kama kiongozi tofauti na wenzake kwa kutumia muda mwingi akitembelea mikoa na wilaya za Tanzania bila mafanikio. Anachofanya Kinana licha ya kuwa kinyume na bosi wake yaani rais Jakaya Kikwete ni kama suto kwa Kikwete. Wakati yeye akipenda kutumia siku nyingi vijijini mikoani, Kikwete anatumia muda mwingi kwenye majiji makubwa ughaibuni.
          Pili, Kinana huwa anatoa kauli za kujikanganya, kukanganya na wakati mwingine hata kujisuta. Mfano juzi alikaririwa akiwa huko wilayani Ngara akisema, “Msikubali kuyaachia mashamba yenu kabla hamjalipwa fidia. Lazima mpewe mkono kwa mkono na siyo vinginevyo, Serikali haiwezi kutekeleza mradi kama haina fedha za kutosha kuwalipa.” Kinana alikuwa akijibu malalamiko ya wananchi kuhusiana na ardhi zao kutwaliwa bila fidia wakati wa ujenzi wa miradi ya maendeleo. Inashangaza kuwa serikali inayofanya haya ni ya chama anachokiongoza Kinana. Kama siyo kuwahadaa wananchi –sijui wachague chama chake –ni nini wakati ana uwezo wa kwenda kuongea na wenzake wakalipa hiyo fedha ya wananchi?
          Pia Kinana akiwa wilayani Kyerwa alikaririwa akisema, ““Hakuna haja ya kutumia ‘pasipoti’ kuhudhuria harusi au msiba wa ndugu yako aliye nchi jirani, itoshe kutumia vitambulisho.” Je ni lini Kinana akawa waziri wa mambo ya Ndani au ya Uhusiano wa Afrika Mashariki? Je anapotoa amri kama hii haingilii mamlaka ya waziri mhusika ukiachia mbali kusahau kuwa anaweza kuwahadaa wananchi asijue kuwa wengi wanajua msimamo wa Tanzania kuhusiana na uhuria wa kuvuka mipaka yake kwa nchi jirani? Inakuwaje Kinana anapingana na msimamo wa nchi kwa kutaka kutoa ruhusa kwa jambo ambalo bunge halijaridhia? Je hapa Kinana alilenga kuonyesha ujinga wake au jeuri yake kama siyo kuchanganya na kuingilia mamalaka ya wizara husika? Je Kinana aliongea haya kutafuta mtaji wa kisiasa na kuonekana anawajali wananchi wakati matatizo yanayowahangaisha yamesababishwa na serikali ya chama chake?
          Sehemu nyingine Kinana alipoonyesha usanii ni pale alipokaririwa akiwa wilayani Muleba akisema, “Uchangiaji wa mafuta ya Mwenge ni wa hiari, si kuwalazimisha wananchi na kusababisha Serikali kutoaminiwa na mkichangisha fedha hakikisha Mwenge huo unafika kwa wananchi wa eneo husika.” Kwanza, watendaji wengi vijijini wanatumia mbio za mwenge si kuchangisha pesa ya mwenge tu bali kujipatia chao ukiachia mbali kuwanyanyasa wananchi. Na hilo si kwamba Kinana halijui. Analijua sema anawafanya watu wapumbavu tu. Pili, ukidurusu kauli ya Kinana kwenye kipengele kinachosema, “mkichangisha fedha hakikisha Mwenge huo unafika kwa wananchi wa eneo husika” haelezi utaratibu unaopaswa kutumika kuchangisha. Na kwanini kuchangisha kana kwamba mwenge ni muhimu hivyo? Kwa mtu ambaye angetaka kuwasaidia wananchi tokana na mateso wanayopata na wizi wanaofanyiwa, angewakataza kuchangia mwenge.  Lakini unaposema mchangishe na kuhakikisha mwenge unafika kwa wananchi husika una maanisha nini kama hakuna shurti na wajibu fulani?
          Pamoja na Kinana kuwachukulia kama watanzania hasa wa vijijini na mikoani ni kama hamnazo, alipata habari yake mjini Bukoba alipotakiwa aeleze ni lini Meli ya MV Victoria meli pekee wanayotegemea wakazi wa mkoa huo kuwaungisha na sehemu nyingine za nchi kwa njia ya majini, alijaribu kujikanganya hadi wakamzoea. Ndipo alichukia na kukaririwa akisema, “Suala la meli itakuja lini sijui, ila kama mnataka niseme uongo nitasema kama hilo ndilo litanisaidia kutoka hapa salama, ila watakapokuja wakubwa zenu waliowatuma waambieni walete hiyo meli kwa sababu kila kitu kinakwenda kwa mipango. Rais alitamka msubiri sasa kama mmepewa elfu kumikumi ili mje mharibu mkutano haya.” Kumbe kwa Kinana wanaompinga wamepewa elfu kumi kuja kumpinga na si kupinga hoja zake zisizo na majibu au tuseme mashiko kwa kero za wananchi? Je Kinana anaweza kutoa ushahidi kuwa waliomzomea walihongwa elfu kumi? Je walihongwa na nani na kwanini linin na wapi? Je kauli ya rejareja kama hii haimuonyeshi Kinana kama mtu anayeamini katika kutoa na kupokea rushwa? Kama aliweza kuwaamuru wananchi waingie nchi jirani kwa vitambulisho tofauti na sheria ya nchi, alishindwa nini kuamuru hao waliotoa, kupokea rushwa na kutaka kuvuruga amani wachukuliwe hatua kama siyo usanii na kuwadhalilisha wananchi?
          Tutamalizia na kauli ya mwenzake, Katibu wa Itikadi na Unenezi wa CCM taifa Nape Nnauye aliyeongea utumbo kana kwamba wananchi ni wapumbavu wasiojua kupambanua. Alikaririwa akiwa wilayani Ngara akisema, “Katiba ni mradi wa wanasiasa kugawana madaraka. Ipite au isipite wakubwa hao watakuwa Dar es Salaam wakigongeana glasi huku wewe ukishuhudia kupitia runinga. Tuwaache wao waendelee na suala hilo na sisi tufanye ya kwetu.” Nnauye alikuwa akongelea vurugu zilizozuka wilayani mle wakati wa kujadili katiba mpya ambayo hata hivyo iliuawa na CCM. Ni kam alikuwa anawambia kuwa “nyinyi mlie tu” tukiamua hamna cha kufanya bali kushuhudia tukitanua nanyi mkiendelea kuumia.
          Kwa ufupi ni kwamba wapinzani wanapaswa kuzitupia macho ziara za Kinana na Nape za mara kwa mara mikoani huku wakichambua hoja zake kwa makini. Kwani anawanufaisha na kujibomoa bila kujua. Maana kauli zake nyingi humuonyesha kama anayewafanya wananchi hamnazo wakati wanazo.
Chanzo: Dira Juni 25, 2015.

2 comments:

Anonymous said...

Ukitaka kujua kwamba aslimia kubwa ya wapiga kura wanamushkeli na ubongo zao angalia Lawassa wanavyompigia chapuo kwa kuanzia tuu...huo udhamini unavyoendelea.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon usemayo yana ukweli. Watu wetu wasipobadilika wataishia kuliwa na kulalamika kila baada ya uchaguzi mkuu.