Tuesday, 30 June 2015

Kijiwe chakutana Simiyu


          Baada ya dada yao Mijjinga na Mipawa aitwaye Rhoda Bujiku kudhalilisha na kuteswa na nesi, walitutonya kama wenzao wanaoheshimika na kuogopwa kayani. Walitutaka tutie timu kule liliko tokea tukio ili kuwalazimisha watawala wetu washenzi kuchukua hatua. Hivyo, minutes za kikao hiki cha Kijiwe zinatokea Mjini Maswa mitaa ya Nyalikungu ambako tulipiga kambi kwa wiki kulaani unyanyasaji huu wa kishetani.
          Mijjinga anaanzisha mada, “Jamani mmesikia aibu ya dada yangu kunyanyaswa, kuteswa na kuaibishwa huko kwetu Usukusini?”
          Mipawa anachomekea, “Kaka umenigusaga pabaya ngwana wetu. Sikujua kuwa bado kuna watu wenye roho za kinyama na washenzi kiasi hiki?”
          “Yakhe mbona mie mwaniacha Solemba? Kwani hili mnoongelea wala sijawapata vilivo wallahi.” Mpemba analalamika.
          Mbwamwitu anadakia, “Ulitaka uwapate vilivo wapi na kwanini mbona Mpemba wataka kulete mambo ya Mpopobawa?”
          “Yakhe una haki ya kuachwa Solemba na usipate pa kutupata japo ukitupata nasi tutakupata au vipi. Anyways, nadhani tumefanya kosa kidogo. Tumeanzisha mada bila kufanya introduction.” Mijjinga anampasia gazeti la Danganyika Kwishnei Leo. Anaendelea, “Hebu soma kichwa cha habari utapata dozi yako.”
          Kabla ya kuanza kusoma gazeti Mpemba anajitetea, “Yakhe acha matusi. Kama wataka dozi weye si useme badala ya kuwasingizia wenzio. Kama wataka sema yakhe.”
          Mipawa anaingilia kati, “Acha niwachomekee kwa mpigo. Kinachogomba hapa si dozi wala nini bali kupataga habari kamili. Si usomage kazeti na kujua anachomaanisha nkwingwa.”
          Mpemba anajibu, “Yakhe nakuheshimu sana. Hivo ngoja nsoma lau nijue anichomaanisha huyu msukuma mwenzio.”
          Mgosi Machungi anaamua kutia timu, “Ami huna haja ya kusoma. Niishasoma hii habai iiyotokea kule Simiyu Maswa ya mjamzito kunyima huduma eti kwa sababu anazaa kia mwaka.”
          “Alaa kumbe. Kama habari ndo hii sina haja ya kusoma gazeti. Kwani bi Nkubwa alinieleza upuuzi na unyama huu wallahi hadi nikashindwa hata elewa inakuwaje kwenye kaya kama yetu haya mambo yanatokea.” Mpemba anajibu.
          Msomi anaamua kukatua mic, “Mnashangaa la mjamzito kunyanyaswa kudhalilisha na kuteswa! Kama umma wote unafanyiwa hivyo, itakuwaje kwa kiumbe mdogo tena wa mashambani kama huyu? Kilichofanyika si kipya. Upya wake ni kwamba vyombo vya umbea vimelipata an kulirusha hewani. Wako wajawazito wengi wanaotendewa mabaya hata zaidi ya haya.”
          Kabla ya kuendelea, Mzee Maneno anamchomekea na kusema, “Si wajawazito wote wanatenzwa hivyo Msomi. Wale wa kisiasa tunaowana na matumbo yao wasiyotwambia ni lini watajifungua wanatendewa vizuri.”
          Msomi anarejea, “Unaongelea wale wazembe wenye viribatumbo vya chumo la ufisadi. Hao achana nao. Tunaongelea wajawazito wa kweli ambao inaonekana sasa hawatakiwi hasa ikizingatiwa kuwa wachovu wanaongezeka kwa kasi ya ajabu.”
          Kabla ya kuendelea, Kanji anatia timu, “Lazima mama zae toto nyingi. Sisi Bombei iko zaa hadi mia.”
          Mchunguliaji anaingilia kati, “Kumbe nave Kanji iko pata mimba na kuzaa toto kama mama! Kanji iko kumbuka kuwa hata hindi hapa nazaa sana ili pate piga kura na kuwa bunge baadaye?”
          “Wallahi hakuna kitu kimeniuma kama kumnyima huduma mjamzito eti kwa vile anazaa kila mwaka. Kwa vile tupo hapa Simiyu, lazima tumtafute huyu nesi tumshughulikie lau aone kuwa kuzaa ni neema. Mie najitolea kumkamata na kumpa mimba ili aone uchungu wa mimba kama hajawahi kujaliwa kuzaa mnasemaje?” Kapenda anaongea kwa uchungu.
          Msomi anakwanyua mic, “Shehe Kapende unakokwenda ni mbali. Tujiepushe kulipiza visasi kwani hakujengi. Huna haya ya kumkamia huyo mpuuzi. Yaani kweli hasira hasara. Yaani unataka umbaki mwenzio bila kujali kama ana miwaya au ni mali ya mwenyewe! Tupunguze hasira ili tuweze kuwasaidia wajawazito na wahanga wengine wa utwahuti na ushenzi huu. Hasira hasara ndugu yangu.” Anakohoa kidogo na kuendelea, “Kaka huna haja ya kupambana na mbwa wakati mwenye mbwa yupo. Hapa nadhani tatizo ni lisirikali wala siyo huyu nesi ingawa naye ni sehemu ya tatizo ambalo ni kubwa kuliko hili tunaloona hapa.”
          “Wakati mwingine tuwe makini tunapolaumu. Sasa hapa lisirikali linaingiaje wakati aliyetenda upuuzi huu ni mpuuzi mmoja?”
          “Nashukuru kwanza umeuona upuuzi ingawa sikubaliani na utetezi wako wa lisirikali. Hujui kuwa kama sheria zingetumika kuwabana wapuuzi kama hawa wachovu wasio na hatia kama dada yetu huyu wasingeumizwa bure?”
          “Yakhe nakubaliana nawe. Twapaswa kuwajibisha lisirikali kwani ndilo liniowapa hawa wapuuzi jeuri ya kufanya upuuzi wao.” Mpemba analalamika.
          Mijjinga anaamua kumchomekea, “Nasikia huyu muuaji aliposikia tunatia ametimkia kusikojulikana kwa kuhofia tusimfanyie kitu mbaya. Nasikia wachovu wenye hasira walitishia kumchoma moto yeye na nyumba yake. Kwanza, nashangaa huyu muishiwa wa eneo hili ni nani mbona hasikiki akikemea lau upuuzi huu? Sijui kama huyu angekuwa mkewe angeweza kukaa kimya huku akikimbiza per diem mjengoni ambako nako hana analofanya?”
          Mipawa anadakia, “Unaualizia muishiwa wa jimbo hili wakati yuko kwenye madili mjengoni? Huyu jamaa ni wa hovyo kuliko yeyote aliyewahi kuwakilisha eneo hili. Hata hivyo, simlaumu. Kwani, anawakilisha tumbo lake mjengoni huku akipiga domo juu ya upuuzi na kuacha mambo ya maana kama haya.”

          Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita mkubwa wa Wilaya. Acha tumtoe mkuku kabla hajaokolewa na wachovu tuisimfanyie kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima Julai 1, 2015

No comments: