Friday, 12 June 2015

Mlevia aota ndoto ya vita ya inzi


          Baada ya kuchapa mma na kupata msokoto nilijilaza kwenye kitanda changu cha kamba. Usiku ulikuwa umeingia. Hivyo, kama ada, lazima nilale mapema lau kutafakari hili na lile. Siku hii sikumsumbua bi Mkubwa bingwa wa maneno. Sikumtakisha cha jio wala chausiku. Niligeukia upande wangu na kuanza kupiga usingi.
          Punde si punde si aliyejuu akaanza kuongea nami kwa kunionyesha maajabu ambayo nami naamua kukumegea lau ujue kuwa kuna ulimwengu zaidi ya huu tuanoishi wa kuchuuzana na kudanganyana. Kwa taarifa yako hatuko peke yetu kwenye vita ya ulaji na kila aina ya tamaa na mazabe. Mara nikaona mainzi manene majike kwa madume yakigombea mzoga uliokuwa umelala bila kujitingisha. Yalikuwa yamehanikiza kuparurana hata kung’atana ilmradi kila inzi lake litimie. Yalikuwapo mainzi mengi madume na machache majike huku yakipigana kwa kila mbinu. Yalikuwa yakipigana huku yakiguguna mzoga.
          Kwa vile mainzi ni mainzi hata yanone vipi, yalikuwa yakila, kutapika, kunya na kuogelea kwenye mzoga hule ule bila kujali kuwa kuna kesho. Maana nijuavyo, mainzi yakishaunajisi mzoga shurti uoze. Hili kwa mainzi yale halikuwa inshu. Inshu ilikuwa kila inzi kupata alichotaka.
          Kabla ya kuendelea kushuhudia huu mtifuano na mnyukano juu ya mzoga niliuliza swali: Je haya mainzi siku zote huishi hivyo? Sauti ilitokea na kujibu. “Hizo ndizo tabia za mainzi sema kwa sasa ni msimu wa kiangazi kwenye ulimwengu wa mainzi.” Jibu hili halikunipa maana ya nilichotazamia. Niliuliza: Una maanisha nini sauti ya asiyeonekana? Sauti ilijibu, “Nilijua hutaelewa hadi nikueleze zaidi.” Kilipita kitambo bila kusikika sauti kana kwamba msemaji aliamua kuondoka ghafla. Mara nikasikia sauti ikisema, “ Katika ulimwengu wa mainzi huwa na msimu wa kiangazi kila baada ya miaka mitano. Hivyo, unapofika msimu huu ambapo ulaji unakuwa juu juu, lazima mainzi yatoane ngeu yakigombea kukusanya mlo ambao utayapeleka kwa miaka mitano.” Niliuliza tena, “Mbona sasa yanakula, kutapika, kunya na kuogelea humo humo?” Sauti ilijibu, “ Hiyo ndiyo tabia ya mainzi. Ni malafi na yasiyoona hata mbele.”
          Kimya kilitawala na nikarejeshewa picha ya  yale mainzi  yakiendelea na uharibifu wake. Yaliendelea kusukumana huku yakipita huku na kule. Ghafla walitokea vipepeo waliokonda. Wanapendeza kwa rangi zao lakini wamekondeana. Kumbe nao walitaka kula kwenye ule mzoga lakini mainzi yalishauchafua kiasi cha kutotamanika ukiachia mbali kuwazuia. Vipepeo walikaa kando wakiangalia kasheshe na mshike mshike wa yale mainzi maneno na machafu yakiendelea kuuguguna na kuchafua mzoga.
          Punde si punde, baada ya kuona mainzi yanataka kutoana roho, inzi moja linaloonekana kuwa mkubwa lao lilipaza sauti na kusema, “Jamani mambo yamebadilika. Mnawaona wale vipepeo.” Lilinyosha mkono kuelekea walipokuwa vipepeo na kuendelea, “Tukiendelea na kujidanganya na kudanganyana hao vipepeo watachukua mzoga na tutakufa kwa njaa.” Mainzi yote yaligutuka na kuacha kufanya makufuru yake ili kusikiliza nondo za mkubwa wao. Aliendelea, “Tusipoweka utaratibu mzuri wa kula, kubalini wenzetu watatunyang’anya hiki kitoweo hata kutushitaki kwa kukichafua kwa kula kilafi bila kunawa, kutapika, kuogelea na kunyea kitoweo.”
          Mara inzi moja lenye kichwa cheupe tofauti na mengine likaamka na kusema, “Mkubwa, naona umezeeka. Maana umekuwa mkubwa kwa viangazi viwili na hali bado ni hii hii ya mtifuano. Naomba unipendekeze mimi kwa inzi wote nipitishwe kusimamia mzoga huu.”
          Kabla ya kuendelea inzi jingine lilipaza sauti na kusema, “Wote watake kusimamia kitoweo na wewe pia? Unadhani ulipokuwa ukinya na kutapika tena madude makubwa hatukuona? Go tell it to the birds, white head huna chako hapa.”
          Mara likatokea inzi kijana na kusema, “Wazee, mimi bado ni kijana na nina nguvu ya kuweza kusimamia kitoweo hiki kisiliwe kilafi wala kuendelea kunajisiwa.” Kabla ya kumaliza kuongea inzi huyu alikunya na kutapika. Ndipo wenzake wakasema, “Wewe acha kimbelembele. Ina maana hivi ndivyo unavyotaka kusimamia kitoweo chetu. Go to hell.”
          Mtifuano uliendelea huku kila inzi akitaka awe msimamizi wa kitoweo. Hata hivyo, inzi ni inzi na inzi wote ni sawa na tabia zao ni sawa. Wakati mainzi yakiendelea kutifuana na kumalizana, vipepeo walipanga mkakati. Waliambizana kuwa wavamie ule mzoga na kuwatimua mainzi kwa nguvu. Wazo hili lilikataliwa na wengi kwa kuogopa kuchafuliwa na mainzi. Hivyo, walikubaliana kuwa waende na kuwalai wale mainzi ima kuuosha ule mzoga au kuondoka ili vipepeo wafanye kazi ile ndiposa wakae pamoja wagawane. Wazo hili lilikubaliwa na pande zote. Ndipo vipepeo wakashinda kuutwaa ule mzoga na kutokomea nao wakiyaacha mainzi yakilaumiana kwa ujinga, uchafu na ulafi wao. Ghafla picha ikatoweka.
          Kabla ya kukurupuka usingizini tazama naona picha ya kunguru wakipigana huku panzi wakijihami. Kunguru kumbe wanapigania haki ya nani awe mkubwa katika kula panzi. Kwa vile wote ni waroho, kila mmoja anataka awe mkuu ili awe anachukua panzi nyingi na kupeleka nyumbani kwake na kula na kunguru wenzake.
          Wakati kunguru wakihanikiza na kutoana macho, naona panzi wakikaa kwenye kikao. Wanakubaliana kuwa sasa wakati wa kuwaadhibu kunguru umefika. Hivyo, wanapendekeza waende kwa binadamu na kuomba msaada wa kuwaangamiza hawa maadui zao. Panzi wanapaa haraka haraka na kutua kwenye nyumba ya binadamu. Binadamu anawauliza, “Nyie panzi, nini cha mno kimewaleta kwangu? Panzi wanasema, tumekuja kukupa taarifa ya mipango ya kunguru. Tumewakuta wakipigana na kutoa maneno mabaya juu yako wakisema kuwa watahakikisha kuku wako hawalei vifaranga. Binadamu aliuza, “Mnasemaje?” panzi walijibu, “tumekuja kukutahadharisha kuwa kunguru wanapanga kuja kuhujumu vifaranga wako na kuhakikisha kuku wako hawaongezeki.” Binadamu aliamka haraka haraka na kusema twende mnionyeshe walipo. Panzi na binadamu waliongozana hadi kwenye kigwena cha kunguru waliokuwa wakiendelea kupigana mateke mitama na makonde. Bila wao kuwa na hili wala lile, binadamu alifungua gunia na kuwafunika nalo na kuondoka nao tayari kwenda kuwafunga kama adhabu ya ubaya wao.
          Kumbe kumekucha! Tafsiri mwenyewe ila usiwaamini inzi na kunguru.
Chanzo: Nipashe Juni 13, 2015.

No comments: