The Chant of Savant

Saturday 20 June 2015

Mlevi anawaletea sifa za rahis mtarajiwa.

Baada ya kuwaletea sera nitakazotumia kuwala –sorry –kuwatawala, leo –kama nilivyoahidi –nakuja na sifa za anayepaswa kuwa rahis wenu. Nafanya hivyo kutokana na kugundua kuwa wenzangu wamekuja na janja ya kujipa ujiko kwa kujiwekea sifa za rahis kulingana na sifa zao. 
Japo kujipigia debe si jambo jema –hasa –kutaka sifa zako ziwe ndizo vigezo vya kumpata rahis, sina jinsi. Nami nacheza mchezo kama wanvyoucheza. Wakifanya rafu nami nafanya kweli. Hivyo, hapa chini ni sifa ambazo zinapaswa kuzingatiwa katika kumpata rahis ajaye. 
Kwanza, awe mvuta bangi na mpenzi wa kanywaji. Maana kwa kushiriki mambo haya kunamuweka karibu na walevi kiasi cha kufanana nao na kujua matatizo yao. Kwa jinsi kaya ilivyopigwa na kupigika, kuhujumiwa na kuhujumika inahitaji mvuta bangi ambaye atakomesha vimbelembele mafisadi na mafisi ima kwa kula nao na kuwazidi kete au kuwasukumizia lupango kama nilivyoonyesha kwenye sera zangu tangulizi. 
Pili, awe mzee na mwenye afya yenye kutia shaka ili asikae madarakani hadi akang’ang’ania kama akina Nkurumbwiza wanaosumbuliwa na ujana kiasi cha kutaka wazeekee kwenye ulaji kama akina YM7 na ving’ang’anizi wengine. Hapa lazima niongeze n aka-sifa kadogo yaani shurti mhusika awe na kichwa chenye mvi nyingi au kipara kama uwanja wa ndege. Hapa akina mama wasio na vipara mnisamehe. Maana  nisipotoa sharti hili bi mkubwa anaweza kunizidi kete tukagombea ulaji mwishowe tukabwagwa au vipi? 
Tatu, asiwe bingwa wa kughushi hasa shahada ili aweze kutumia ubingwa wake wa kughushi kuwatambua na kuwazidi kete wawekezaji wanaotumia mikataba kuizidi kete kaya. Lazima awe na PhDs zaidi ya moja. Bahati nzuri mimi nina karibu kila kitu tena ambazo si heshima almaaruf honoris causa au za kupewa kama peremende. Nitakwenda hivyo hivyo. Pia mhusika asiwe mtu wa kubebwa na jinsia, ukoo, atokako au kabila lake. Mimi nakidhi vyote kwa vile huwa sibebwi zaidi ya kupata kanywaji na bangi na kufyatuka. Hivyo, mkifanya kosa –sorry –mkinichagua lazima nifyatuke na kuwafyatua wanaowafyatulia vyenu kifisadi. Nitawakamata hadi kuku wao. 
Nne, awe bingwa wa kutoa ahadi za kweli na za uongo kama vile maisha bora kwa wote, kutafutia ajira vitegemezi na vijana hata kam anamaanisha vitegemezi vyake na si walevi wote. Kimsingi, ni kwamba awe ni bingwa wa kuongopa ili wawekezaji na wachukuaji waone vigumu kumdanganya bingwa wa kamba, sanaa na urongo. Mimi ni bingwa wa Nyanja hii hasa ikizingatiwa ninavyomfunga kamba bi mkubwa na kuondoka na uchache wake wa mboga kwenda kupatia kanywaji. 
Tano, awe bingwa wa kuhonga kwa kumwaga mshiko hata kama atataoa mshiko wake kwa kila amuonaye akisingizia ni mchango wake na marafiki zake asiopenda kutaja majina na kiasi walichomchangia. 
Sita, awe amewahi kuachika yaani kutimliwa serikalini baada ya kula kwa pupa. Hii itamsaidia kutia adabu apatapo ulaji kwa kuhofia atafanyiwa kitu mbaya baada naye kufanya kitu mbaya kwa njuluku za walevi. Mna habari kuwa mimi nimewahi kuachika sana hasa baada ya kupiga kanywaji na tu bangi nikamtandika makonde bosi gabacholi pale nilipogundua halipi kodi. 
 Hivyo, mnaweza kuona nilivyo na uchungu na walevi na wachovu hadi kuwa tayari kumwaga damu kitumbua changu na kusulubishwa ili niwakoe.
 Saba, apende utawala wa sheria ili asije akapinda sheria au kukwepa kuwafunga mafisadi wenzake. Kimsingi, ngurumbili asiyependa utawala wa sheria anaweza kuipinda na kuwaruhusu washikaji zake kuanzia yule wa bedroom hadi vitegemezi kutumia unene wake kutengeneza njuluku haraka na kinyume cha sheria. 
Nane, awe tayari kutaja utajiri wake na jinsi alivyoupata hata kama kufanya hivyo kutasababisha majambazi wamtembelee ili nao wahomole na kutanua kama yeye. Asifanye kama Njaa Kaya ambaye alikaa miaka kumi ulajini bila kutaja utajiri wake kwa kuhofia kuulizwa maswali mengi ya kichokonozi. Pia awe tayari kuzungumzia kashfa zinazomkabili ili walevi wasimstukie wakampiga chini. 
Tisa, asiwe ni mkabila anayependa kujisifia kwa kabila lake hata kama ukweli ni kwamba mhusika hana asili ya kabila analojivunia kama wengine tunaowajua. 
Kumi, asiwe na kiherehere cha kutaka ulaji hata kama hana sifa. Mwenzenu kwa nilivyokaa kwenye ulevi na uvuta bangi sina kiherehere wala kimbelembele kama wale viherehere na vimbelembele wa Njaa Kaya na Makorongo Nyenyere. Sijawahi kutumikia umma nikatimuliwa zaidi ya kutimliwa na gabacholi tena si kwa kutenda kosa bali kuwatetea walevi na wachovu wenzangu. 
Kumi na moja, awe na jina kubwa hasa la baba au mama yake. Hapa ndipo naua. Maana mjina wangu Dk, Profesa, Alhaj , Maalim, Ustaadh, Maulana, Father, Askofu, Papa, Luteni Kanali Mpayukaji Msemahovyo wa Waambie wa Wapashike si jina dogo ati. 
Kumi na mbili, lazima mhusika awe hana urafiki wala ukaribu na wanaoondoka kwa vile lao litakuwa moja ingawa kwa sasa wengi wanajifanya kuwarushia madongo wakiwatuhumu kwa uchafu, uzembe, upendeleo na kila mazabe wakati walikuwa kwenye kitanda kimoja wakifanya ka-nchezo kale kale ka kuwala jamaa zangu waliwa. 
Leo sitachonga mengi. Ila nawaonyeni enyi walevi. Nani aliyawaroga kuambiwa kuwa fisi hata akivaa ngozi ya kondoo anaweza kuwa kondoo hadi mkaamini.kwani hao wanaowatapeli na kuwageuza mabunga hawakuwekwa mbele zenu mkiona? Mti mwema utaujua kwa matunda yake. 
Shauri yenu mtaliwa mkijiona kama mtaamini kila sifa. Tangu lini anayechumbia akateua sifa za muoaji asijivutie kwake?
Chanzo: Nipashe Juni 20, 2015.

No comments: