Sunday, 14 June 2015

Hongera Makongoro na Membe

          Hivi karibuni waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (MNNUK) Bernard Membe alikaririwa akiwaonya watanzania kuwachunguza wanaotangaza nia ya kugombea urais. Membe aliyasema haya wakati akizindua Tamasha la Ulamaa la Qaswida katika shule ya Benjamen Mkapa akitangaza siku chache bada ya kutangaza nia ya kugombea kadhalika.
Membe alikaririwa akisema, “Wachujeni viongozi wanaotangaza nia ya kuwaongoza, muwapime kama wana maadili ya kutosha, wapimeni kama siyo wala rushwa.” Asemayo Membe ni ya msingi japo kuna mengine ya muhimu aliyosahau au kuyaacha maksudi kwa vile yanamgusa. Hivi karibuni wizara yake iligundilika kulipa mishahara na marupurupu na pango la nyumba kwa maafisa wake waliostaafu kwenye balozi zetu nje. Kashfa hii iliibuliwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa fedha za serikali (CAG). Hivyo, tukianza na Membe, kama ameshindwa kusimamia wizara moja na fedha za umma, hiyo nchi ataiweza?
          Baada ya wanachama wengi vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangaza nia ya kugombea, vituko vingi vimeibuka. Kila anayesimama kuongea anajiwekea vigezo vya urais kwa kuangalia sifa zake. Mfano, Edward Lowassa aliyetikisa sana hivi karibuni, alikaririwa akisema, “Kuamini kama una uwezo na shauku, hakuna budi kwenda sambamba na uwezo wa kusimamia yale unayoyaamini. Na kwangu haya mawili ni dhahiri. Nina ari, nina shauku na nina uwezo, kama rekodi yangu inavyothibitisha.” Je ari na shauku ya mhusika vinatosha kweli kuwa vigezo safi vya mtu anayefaa kuwa rais? Ajabu ya maajabu ni pale Lowassa anaposema, “kusimamia yale nayoyaamini”. Je kama mhusika anaamini kwa mfano katika ndoto na upuuzi nacho kiwe kigezo jamani? Kituko alichotuachia Lowassa ni kujipa sifa zote za kuwa rais lakini akasahau au kuficha au kukwepa kuongelea kashfa ambayo imemuandamana maisha yake yote ya Richmond. Bila shaka hapa kuna namna.
          Vituko vinaendelea kuonyesha watangaza nia walivyofilisika kiasi cha kujivuana nguo japo ni ukweli. Makongoro Nyerere hakubaki nyuma. Alikaririwa akisema, “Kosa la Rais Kikwete ni kuwapenda sana marafiki zake. Kwa bahati mbaya baadhi ya marafiki zake hao ni vibaka. Kibaka ni kibaka tu hata akipewa gari la Serikali na kupeperusha bendera ya Tanzania, bado ataendelea kuwa kibaka tu.” Wengi wanajua aliowalenga. Maana, baadhi ya vyombo vya habari vilitaja wazi wazi majina ya wahusika mmojawapo akiwa Lowassa. Gazeti moja la Kiswahili litolewalo kila wiki lilibeba kichwa cha habari tangulizi: Makongoro: Kina Lowassa wadokozi. Ajabu hawa ndiyo mkongwe wa CCM Kingunge Ngombale-Mwiru aliwapigia debe kuwa wanafaa. Je tatizo hapa ni njaa, uzee au chama kibovu? Jibu analo Makongoro aliyekaririwa akisema, “CCM kinaugua maradhi ya kukaa madarakani kwa muda mrefu na dalili za maradhi hayo ni kuteua wagombea bila kujali matakwa ya wananchi.” Kwa lugha nyepesi ni kwamba CCM imeisha, imeishiwa. Wanachoweza kufanya wanachi hasa wapiga kura ni kuistaafisha lau ikapumzike.
Je Kingunge alisukumwa na nini hadi akajivua nguo hadharani? Acha Makongoro ajibu, “CCM hivi sasa ina makundi. Kila mgombea ana timu yake na msingi mkuu wa timu hizi ni fedha na wanaojiunga nayo wanafuata fedha. Leo hii nikiwa na hela hata walioko kwa wagombea wengine wananifuata.” Ama kweli penye udhia penyeza rupia walijisemea wahenga!
          Kinachonogesha ngoma ni kuona makada hawa vigogo wa CCM wakiinanga CCM na mwenyekiti wake wazi wazi wakionyesha wazi ilivyochemsha. Membe alikaririwa akisema, “Uongozi wa heshima ni ule wenye maadili. Viongozi bora ni wale watakaochukia vitendo vya rushwa kwa nguvu zote, jamii imechoka kushuhudia vitendo hivi vinavyonyima haki.” Kwa maana nyingine ni kwamba Membe anakiri kuwa chama chake kimeua maadili na kuanzisha madili huku wananchi wakiporwa haki zao na viongozi. Je Maneno ya Membe ni uongo? Makongoro anajibu, “Wapo waliotangaza nia ambao wanajinasibu kununua nyubma Dubai na sehemu kadhaa huko Ulaya na kwingineko. Wasijidanganye kwa sababu wakiharibu huku na kukimbilia huko watambue watakuwa wakimbizi tu. Hapa ndipo petu sote.” Je hawa ni akina nani? Je ni wale aliowaita marafiki wa Kikwete ambao anawapenda sana kuliko wananchi? Jibu unaweza kulipata kwenye maneno ya Lowassa aliyewahi kusema kuwa urafiki wake na Kikwete haukuanzia barabarani. Je watu wa namna hii wanalifaa taifa au wataliuza zaidi?
          Kwa vile Makongoro ameamua kuweka mambo hadharani kwa kuingia moto huu wa urais, kuna haja ya kumtaka ataje majina ili asionekane mmbea japo maneno yake yana ukweli.
          Kama kuna masomo nimejifunza tokana na utangazaji wa nia ni:-
Mosi, CCM kweli imeishiwa na hairekebishiki wala kusafishwa na wala haiwezi kupona kipindi hiki vinginevyo yatokee mambo mawili, mosi, miujiza na pili, uchakachuaji.
Pili, ni kwamba mjenga na mjengua nchi ni mwananchi. Kwa sasa, wanachofanya watangaza nia ni kuizika CCM kabisa. Kwani, kama upinzani utazingatia maneno yao na mazito waliyoyaibua na kuyafikisha kwa wananchi kwa ustadi, CCM kwishinei (kwisha). Maana, hakuna anayewajua CCM kama wanavyojuana. Hivyo wasemayo si siasa bali ukweli usiopingika.
Hongereeni Makongoro na Membe kwa kuweka mambo hadharani na kutufumbua macho.

 Chanzo: Tanzania Daima Juni 14, 2015.

2 comments:

Mbele said...

Hii makala imeanika vizuri uozo ulivyo katika suala hili, kwa kutumia kauli za wahusika wenyewe (kwa ki-Ingereza wanasema "from the horse's mouth").
Januari Makamba, mtangaza nia mmojawapo wa CCM, katika kuhutubia mjini Songea siku chache zilizopita, alishauri kwamba watangaza nia wenzake katika CCM waache kuchafuana, waache kutupiana matope. Alisema wakumbuke kwamba, mwisho wa yote, atakapopatikana mgombea, watatakiwa kumnadi. Akauliza watawezaje kumnadi mtu ambaye tayari wameshamtupia matope na kumchafua?
Kwa mtazamo wa juu juu, huu unaonekana kuwa ushauri wa busara. Lakini kwa undani wake, ni balaa jingine, kwani ujumbe ni kuwa watangaza nia wasimwage madhambi yao hadharani. Makamba anachosema, hata kama hakukusudia, ni kwamba wananchi wasielezwe uozo wa watangaza nia.
Ninahitimsha kwa kukubaliana nawe Ndugu Mhando kwamba CCM ni janga.

NN Mhango said...

Kaka Mbele nakubaliana na jicho lako la pevu la kuweza kuyadurusu na kuyatafakari waliyosema. Nakubaliana nawe kuwa Makamba amegundua jinsi wanavyovuana nguo na kumwaga mtama kwenye kuku wengi. Sisi yetu macho na masikio kuona watavuana nguo kiasi gani na kwa faida ya nani. Nadhani wapinzani wamepewa nchi vinginevyo nao wafanye uzembe. Kaka jina langu ni Mhango si Mhando.